Bashe anamsingizia bure Jakaya Kikwete kuhama kwa Lowassa

Saturday March 9 2019

Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe akizungumza

Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe akizungumza katika mkutano wa kampeni za mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara uliofanyika kwenye Viwanja vya Mwanagati Kitunda, jijini Dar es Salaam. Picha ya Maktaba 

By Luqman Maloto

Edward Lowassa, mgombea urais wa Chadema na Ukawa 2015 amesharejea CCM alikokulia kisiasa. Kufuatia hatua hiyo, Rais wa nne na Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Kikwete akaona ni uungwana kumkaribisha nyumbani.

Kikwete aliandika ujumbe kupitia akaunti yake ya Twitter: “Karibu tena nyumbani. Hongera kwa uamuzi wa busara.” Makaribisho hayo ya Kikwete yakamchokoza Hussein Bashe, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), akamjibu palepale Twitter:

“Ulimdhalilisha. Ulimvuruga. Ulimbebesha mzigo usiokuwa wake. Uliichafua heshima yake. Na 2015 Dodoma wakati wana CCM wanakuomba ukutane naye baada ya mkutano mkuu ulifunga milango. Aliondoka CCM kwa sababu ya kufeli kwa uongozi wako na siyo kwa sababu ya kutofautiana kiitikadi.”

Andiko la Bashe linaonyesha aliposoma tu kauli ya Kikwete palepale aliijibu.

Hapa kuna tatizo la kisaikolojia. Mwanazuoni Dk Matt James, kupitia andiko lake la React Vs Respond kwenye tovuti ya Psychology Today aliliweka vizuri jambo hili Septemba Mosi, 2016.

Dk Matt aliandika kuwa react (onyesha hisia) ni tendo la haraka bila kuushirikisha ubongo. Respond (jibu) ni tendo la taratibu, yaani baada ya kuushirikisha ubongo. Kwa hiyo, Bashe baada ya kuiona kauli ya Kikwete moja kwa moja ali-react. Hivyo basi, alichofaanya Bashe ni reaction, haikuwa response.

Kwa mujibu wa Dk Matt, reaction huwa na msukumo wa kiimani, hisia hasi na hata kutotenda haki. Bashe alikuwa mstari wa mbele katika ‘Timu Lowassa’ katika mchakati wa Uchaguzi Mkuu 2015. Na kwa nadharia, Timu Lowassa humuona Kikwete ndiye kikwazo cha Lowassa kuwa rais.

Ni dhahiri kuwa Bashe angepata muda wa kutafakari, angeweza kuchagua kunyamaza au kutumia maneno tofauti. Kwa vile ali-react, alirusha mashambulizi ambayo kiukweli ni kumuonea tu Kikwete.

Kikwete na Lowassa

Kikwete na Lowassa ni marafiki wa muda mrefu. Hawatofautiani sana namna walivyoanza na walivyopanda kisiasa. Wote ni makada wa tangu Tanu kabla ya CCM. Wote walipita jeshini. Waliitumikia CCM na walitofautiana miaka miwili tu kuteuliwa serikalini.

Wakati Kikwete aliteuliwa mwaka 1988 kuwa waziri mdogo wa Nishati na Madini na mwaka 1990 kuwa Waziri kamili wa Nishati, Madini na Maendeleo ya Maji; Lowassa aliteuliwa kiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, Mahakama na Masuala ya Bunge mwaka 1990.

Mwaka 1995 wakati Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya siasa, Kikwete na Lowassa walikuwa wagombea mapacha katika kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais. Walitangaza nia pamoja, wakachukua fomu siku moja.

Hata Lowassa alipoishia njiani, alimuunga mkono Kikwete ambaye hatimaye alipambana na Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa. Mwaka 2005, Lowassa alikuwa mwenyekiti wa kampeni za Kikwete. Na Kikwete aliposhinda urais, alimteua Lowassa kuwa waziri mkuu.

Lowassa alidumu kwenye uwaziri mkuu kwa miaka miwili tu kabla ya kung’oka kutokana na kutajwa katika kashfa ya mradi wa kufua umeme wa dharura, uliokuwa utekelezwe na kampuni ya Richmond na baadaye ikaonekana haikuwa na uwezo.

Tangu kashfa ya Richmond na Lowassa kung’oka, tayari kulikuwa na minong’ono mingi kuwa marafiki, Kikwete na Lowassa hawaelewani. Kuna visa vingi katikati, lakini kila kitu kilikuwa dhahiri mwaka 2015. Kila kilichotokea, kwa jumla, utaona kwamba Bashe anamwonea bure Rais Kikwete kuhusu Lowassa kwenda Chadema.

Kwa nini Kikwete anaonewa?

Kwanza kabisa, wakati wakimpokea Lowassa, ni kuwa chama hicho tayari kilikuwa na mazungumzo na Lowassa kuhusu kuhamia kwao kabla hata hajakatwa CCM.

Mgogoro wa aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema, Dk Willibrod Slaa kuamua kujiuzulu kwa sababu ya kutokubaliana na uamuzi wa chama chake kumpokea Lowassa na kumteua kuwa mgombea urais, ulisababisha mengi yawe hadharani. Ikagundulika kuwa Lowassa aliwaandaa Chadema wampokee kama angekatwa CCM. Hicho ndicho kilitokea.

Bashe anaposema Lowassa alikwenda Chadema baada ya kukosa nafasi ya mazungumzo na Kikwete, hilo si kweli.

Vinginevyo, Bashe angeanza kukosoa matamko ya Chadema mwaka 2015 kuwa walielewana mapema na Lowassa kutumia chama chao kama mpango mbadala ya kuwania urais. Hivyo, kuhama ulikuwa mpango ulioiva muda mrefu.

Hoja ya pili ni kuwa kufanyika Uchaguzi Mkuu 2015, maana yake Kikwete alikuwa anaondoka madarakani. Angekabidhi urais na uenyekiti wa chama. Kwa hiyo, kama kweli Kikwete na uongozi wake ni sababu, mbona Lowassa angesubiri kidogo tu aondoke? Sababu ya kuhama haikuwa kuudhiwa na Kikwete, bali kugombea urais.

Hoja ya tatu ni kuwa Lowassa mwenyewe hakujua jinsi ya kucheza mpira wake. Joto la Kikwete na Lowassa kutoiva lilikuwa kali tangu Februari 2008 Ripoti ya Richmond iliposomwa bungeni. Na inavyoonekana wawili hao hawakutafutana kuzungumza.

Lowassa aliwahi kusema kuwa urafiki wake na Kikwete haungetetereka kwa sababu hawakukutana barabarani. Upande wa pili kukawa na kutunishiana msuli. Lowassa akiamini angeweza kushinda bila Kikwete kutaka.

Palipo na ushindani huwezi kumlaumu anayekushinda. Lowassa alitaka awe Rais hata kama Kikwete hakutaka. Na ushindani kati ya Kikwete na Lowassa ulikuwa dhahiri 2015. Kama Lowassa aliamua kushindana, huwezi kumlaumu Kikwete kushinda katika mvutano.

Advertisement