Chakula unachowapa kuku wako kilenge kukupa faida

Saturday January 26 2019

Mkazi wa kata ya Lunzewe,Wilayani

Mkazi wa kata ya Lunzewe,Wilayani Bukombe,Protas  Buhara akiwapatia kuku chakula anaofuga nyumbani kwakwe,mkoani Geita.Picha na Maktaba 

By Clement Fumbuka

Ni matumaini yangu kufahamu maendeleo bora ya wafugaji wa kuku kila mara. Wapenzi na wafuatiliaji wa makala hizi za ufugaji wanaweza kujipatia wigo mpana katika kuboresha au kuimarisha miradi yao kila wakati kwa kusoma na kung’amua ujuzi mbalimbali.
 Tangu tuanze kufahamishana mambo kadhaa katika kuiboresha sekta hii, hatujachoka kudodosa siri za mafanikio katika ufugaji.
Tulianza na hatua za awali kwa mfugaji kujua vitu muhimu kabla hajaanza kutambua masoko ya bidhaa zake na kutenga bajeti ya mradi na kuanza ujenzi wa mabanda na kununua vifaranga wa kuanzia.
Sambamba na hayo hatukubaki nyuma kujuzana aina bora au mbegu bora ya kuku inayofaa kuwekwa shambani kwa mfugaji kulingana na ndoto zake.
Hii ni kwa sababu mbegu za kuku hutofautiana kiuzalishaji wa nyama na mayai. Mwenye ndoto ya kuzalisha mayai, afuge mbegu yenye sifa za kuzalisha mayai mengi. Pia,  mwenye ndoto ya kuzalisha nyama, afuge mbegu inayokua haraka na kuweka uzito mkubwa mapema.
Kuku na chakula
Ujumbe wa leo unahusu matumizi ya chakula cha kujitengenezea na kile cha viwandani. Tunajua kuwa sehemu kubwa ya gharama za ufugaji huenda kwenye chakula.  Wafugaji wa siku nyingi wanafahamu hilo na wale walioanza au wanaotegemea kuanza inabidi wafahamu hivyo.
Kupanda na kushuka kwa chakula ndiyo hupunguza au kuongeza faida kwenye ufugaji. Mbinu mbadala ya kukabiliana na hali hiyo ni kwa mfugaji kutafuta namna ya kupunguza gharama za chakula kwa kujitengenezea chakula chake mwenyewe.
Wakati huo mfugaji anakuwa amelenga mambo makuu mawili; moja kupunguza gharama na kuongeza faida. La pili ni kuzalisha kwa wingi na kwa ubora unaotakiwa kukabiliana na ushindani wa soko.
Katika mambo haya mawili ndipo watu wa viwanda hupata upenyo wa kumuuzia chakula mfugaji, badala ya kujitengenezea mwenyewe, kwa kuwa wafugaji hushindwa kutengeneza chakula bora.
Sifa ya chakula cha viwandani ni ubora wa hali ya juu kuliko kile anachokitengeneza mfugaji. Lakini jambo linalomsukuma mfugaji kujitengenezea chakula ni bei kubwa ya chakula cha viwandani. Huo ndiyo mkanganyiko wa fulani, anatumia chakula cha viwandani na fulani anatumia chakula cha kutengeneza mwenyewe.
Mfugaji ana ruhusa ya kuchagua chakula kinachomvutia kulisha kuku wake. Watu wa viwanda hutengeneza chakula chenye ubora wa kumfanya kuku apate virutubisho vyote kwa kiwango kinachotakiwa kukua na kuzalisha kwa wingi.
Kwa upande mwingine, wafugaji hutengeneza chakula chao wenyewe bila kuwa na uhakika wa kuwapo kwa virutubisho vyote kwa kuku,  matokeo yake kuku hushindwa kukua na kuzalisha vizuri.
Wapo watu walioanza na chakula cha viwandani na kujitoa, wakaanza kujitengenezea wenyewe kwa kukwepa gharama, lakini wapo waliohama kutoka kujitengenezea chakula chao na kuanza kulisha cha viwandani.
Makala haya ni kwa ajili ya wafugaji wote pamoja na wadau wengine wenye mchango katika  ufugaji.
Jambo muhimu kwa mfugaji ni kujua faida yake ikoje anapotumia chakula cha kujitengenezea au cha kiwandani.
Kama unaweza kutengeneza chakula mwenyewe kwa gharama nafuu na  kwa ubora ni vyema. Isitokee mfugaji ukawa na malengo ya kukwepa gharama za chakula cha viwandani ukajikuta umeingia gharama nyingine za kuku kuwa na afya mbovu kwa sababu ya  lishe duni.  Kaulimbiu ya ujasiriamali katika ufugaji wako inatakiwa kuwa faida kwanza. Gharama ni matokeo ya kazi yenyewe; kama kazi ni nzuri hata gharama ikiwa juu faida utaiona.

Advertisement