USHAURI WA DAKTARI: Fahamu ukweli kuhusu kurefusha uume

Wanaume wengi wanatamani kuongeza urefu na upana wa maumbile yao ya uzazi, kutokana na kuathirika kisaikolojia kunakowafanya waamini mabadiliko hayo huongeza uwezo wa kumfikisha mwenza kileleni.

Vilevile, wanaume hawa huamini maumbile hayo yanayoleta msisimko kupita kiasi wakiwa nayo wataonekana marijali na watawavutia wanawake walionao.

Wanafanya hivi kwa kukosa uelewa kuwa msisimko na kilele cha tendo la ndoa unatokana na ujuzi binafsi, kwa kutumia akili na viungo vya mwili kuleta na kuongeza msisimko baina ya wenza walio tayari.

Wasichokijua ni kwamba kinachotakiwa ni kuwa na uume wa wastani kuliko mkubwa uliopitiliza unaoweza kuwasababishia maumivu wenza wao, jambo litakalofanya mwisho wa siku wasifurahie tendo hilo na kuongeza uwezekano wa kupata hofu kutokana na ukubwa huo.

Laiti kungelikuwa na njia salama za kunenepesha na kurefusha maumbile katika huduma rasmi za afya, gharama za kuchangia matibabu zingekua maradufu. Kwa sababu wanaume wengi wanaodhani wana maumbile madogo ya uume wangemiminika kwenda kutibiwa tatizo hilo.

Mamlaka za ndani na kimataifa kama vile Wizara ya Afya, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Shirika la Afya Duniani (WHO) na vyuo vikuu vilivyobobea kufanya utafiti kikiwamo Havard, hakuna mahala ambapo wamepitisha na kupendekeza dawa au kifaatiba kwa ajili ya huduma hiyo.

Watu wanene kupitiliza, shina la uume lililo chini ya kitovu humezwa na mafuta na nyama zilizorundikana hapo, hivyo kupunguza urefu wa kiungo hicho muhimu kwa tendo la ndoa.

Zipo njia chache ambazo jumuiya za kimataifa na mamlaka za afya wanakubali kuwa zinaweza kusaidia angalau kuongeza urefu, lakini usiozidi nchi moja, njia hizo ni pamoja na kupunguza unene.

Hivyo, kupunguza unene kwa njia ya vyakula na mazoezi inakubalika. Vilevile kwa njia ya upasuaji kwa lengo la kupunguza mafuta ya eneo hilo inakubalika pia.

Vitu vinavyotumika kiholela kunenepesha na kurefusha uume ni pamoja na vidonge, sindano, virutubisho, mashine maalumu, upasuaji wa kupandikiza, vifaa vya mazoezi ya uume, mafuta ya kupaka uumeni na mitishamba.

Vitu hivi vinauzwa kisiri katika baadhi ya maduka ya dawa, kwa njia ya mtandao, kutembezwa mtaani au matangazo kwenye magazeti na vyombo vingine vya habari.

Lakini, kati ya hivyo nilivyotaja, hakuna vinavyofanya kazi kwa ufanisi na kukidhi vigezo vya kitaalam kupitia vyombo vikubwa vya matibabu na uthibiti wa magonjwa ikiwamo WHO.

Kwa sababu hakuna utafiti wa kisayansi kuthibitisha ubora, ufanisi na usalama wa vifaatiba hivyo au njia zilizopendekezwa ingawa ni kweli, vipo baadhi ambavyo kwa muda mfupi, vinaweza kukusaidia lakini vikikuacha na madhara makubwa hapo baadaye.

Madhara hayo ni pamoja na kupungua au kukosa kabisa nguvu za kiume, kuchubuka uumeni, kuvunjika kwa misuli sponji ya uume, madhara ya nerve na kupata maumivu sugu wakati wa kujamiana.

Taarifa zinaonyesha wanaume wengi hujikuta wakinasa na kununua vifaa hivi kwa sababu ya kuathirika kwao kisaikolojia ambako huongeza shauku iliyopitiliza ya kuongeza maumbile.

Ukidadisi unakuta wengi wao hawajawahi kwenda kwenye kituo cha huduma za afya au hospitali kwa ajili ya uchunguzi na ushauri. Wengi wanaojihisi wana uume mdogo hugundulika kuwa hawapo chini ya inchi tatu baada ya uume kusimama.