Faida tano za mazoezi ya kunyoosha viungo

Si sahihi kabisa kiafya kuingia mazoezini ama mchezoni pasipo kufanya mazoezi ya viungo ambayo huwa ni kunyoosha viungo bila kukimbia au kutembea.

Mazoezi haya ni ya msingi kwani yanauandaa mwili kuweza kukabiliana na hali ngumu zinazojitokeza michezo kama vile kujipinda uelekeo hasi, kuvutika kwa nyuzi mvutiko za misuli, nyuzi za ligamenti na tendoni.

Zoezi hili kiujumla linasaidia mwili kukabiliana na mijongeo hasi inayoweza kujeruhi tishu laini za mwili hivyo kumuepusha mwanamichezo na majeraha yasiyo na lazima.

Zoezi la kunyoosha viungo huwezesha misuli ya mwili kupata utulivu na kuwezesha damu na virutubisho muhimu kutiririka kwa wingi katika mifupa plastiki na misuli.

Leo tutaona faida tano za awali za faida za kiafya za zoezi la kunyooosha misuli ya mwili.

Moja ni kuondokana na uchovu hivyo kukufanya kupata utulivu wa kimwili na kiakili.

Kurundikana kwa shinikizo katika misuli huifanya misuli ya mwili kujikunyata hivyo kuleta hali ya hisia za kukakamaa na kutohisi wepesi hivyo kuleta madhara ya kiakili na kimwili.

Kuondoa au kupunguza shinikizo lililopo katika misuli hivyo siku inayofuata unapoomka huwezesha mwili kuwa mpya kiutendaji.

Kumbuka kuwa pale unapoamka na uchovu au kuumwa viungo huweza kukupa hofu pengine unaumwa na magonjwa ikiwamo malaria.

Mazoezi haya yanaifanya misuli ya mwili isibane na kuipa utulivu hivyo kutoa nafasi kwa damu kutiririka kirahisi. Pia mazoezi haya husababisha mwili kutiririsha kemikali mwili ijulikanayo kama Endorphins inayoufanya mwili kupata hisia za furaha.

Vile vile kufanya mazoezi haya kabla ya kwenda kulala husaidia kukupa usingizi mzuri.

Mbili, kusaidia kuweka ulalo sahihi wa mwili, kunyoosha misuli ya mwili iliyokakamaa husaidia kuivuta na kuirudisha katika sehemu yake asilia inayotakiwa kuwepo.

Kunyoosha misuli eneo la chini mgongoni, kifuani na mabega husaidia kuuweka uti wa mgongo katika mpangilio sahihi hivyo kuboresha mkao wake ambao hauleti uchovu wa misuli hii.

Tatu kuimarisha wepesi wa mwili, wepesi huufanya mwili kuwa na utayari wa mabadiliko wakati wowote ikiwamo unaporuka, kukimbia au kujipinda.

Wepesi wa mwili kwa mijongeo hii huupunguzia mwili mzigo kiutendaji kwani mwili utatumia nguvu kidogo kufanya matendo hayo.

Pia wepesi husaidia kuboresha utendaji wa kimwili na kupunguza hatari ya kupata majeraha ya mara kwa mara wakati wa michezo.

Nne ni kuongeza uwezo (stamina) kwani huifanya misuli na nyuzi za tendoni na ligamenti kuwa laini na nyepesi hivyo kuondokana na kukamaa na uchovu . Hii ni kwasababu damu hutiririka kwa wingi maeneo hayo.

Kadiri unavyofanya mazoezi ndivyo pia mwili huchoma kiasi kikubwa cha nishati (glucose) hivyo kuchangia mrundikano wa mabaki baada ya nishati kuvunjwa.

Zoezi hili husaidia kuchelewesha kujijenga kwa uchovu unaoletwa na mabaki hayo kwani damu safi kufika kwa wingi katika misuli na kuyaondoa hivyo kuongeza utimamu wa mwili.

Tano, kupunguza hatari ya kupata majeraha kwani misuli hupokea damu na virutubisho kwa wingi hivyo hii ni faida kubwa kiafya kwani hupunguza vijidonda vya misuli. Vile vile husaidia majeraha ya misuli na maungio kupona kwa wakati.

Kutokana na faida hizi ni vizuri kwa mwamichezo kuyafanya mazoezi haya kama sehemu ya maisha ya kila siku kabla na baada ya mazoezi