GOZI LA NG'OMBE: Solskjær ni Big G nyuma ya pazia

Monday January 7 2019

 

Wapo wanaoamini kuwa ukikosa basi ni kuwa umesaidiwa ili uje upate jema zaidi ambalo litakufaa kwa kipindi kirefu na pia kuendana na ndoto zako ama kufikisha malengo yako.

Sio kila mara king’aacho hata kama ni dhahabu basi kimepangwa kunakshi mboni za macho yako na kupednezesha muonekano wako, inawezekana kikawa kimepangawa kwa ajili ya jirani yako.

Pale kwenye jiji la Manchester, wakati huo babu Sir Alex Ferguson akiwa hajapata mvi nyingi, alikumbwa na tatizo la washambuliaji hasa ikiwa kweli kuwa Andy Cole alionekana kuchoka. Akili ya Fergsusson ilikuwa inakimbia kwa kasi na kila alipogusa alionekana kukosa.

Mwaka 1996 kwenye majira ya kiangazi, United iliyokuwa na ushawishi wa Fergie ilimkosa Alan Shearer aliyetua Newcastle, ikabidi safari ifungwe hadi Norway kumtazama kijana mmoja aliyekuwa hafahamiki na mtu isipokuwa maskauti walipata stori za mguu wake kuwa una madini yenye thamani.

Kwenye makaratasi na mikanda ya video aliyoletewa Fergie alikuwa anaonyeshwa kijana mmoja aliyeonekana kuwa mkimya na asiyekua katili, asiyekuwa mjivuni na ambaye wengi wangeweza kujiuliza huyu anamtisha vipi Tony Adams pale Arsenal?

Hata hivyo, jibu la ndio lilikuwa la haraka zaidi kwa Fergie na huyo kijana akatua ndani ya jiji la Manchester. Kijana alifahamika kwa jina la Ole Gunnar Solskjær.

Hapakuwa na mjukuu aliyeona majuto tangu kipindi hicho mpaka Ole anaipa mkono wa kwaheri familia ya Old Trafford, aliweza kuichezea United michezo 366 huku karibu nusu yake yaani 150 akiingia kama mchezaji wa akiba na kufunga jumla ya mabao 126 na 50 kati yake yakifungwa dakika 30 za mwisho za michezo aliyocheza huku, 33 kati yake akiyafunga katika dakika 15 za mwisho.

Ole Gunnar Solskjær alipatiwa jina la Mr Reliable yaani wa kutegemewa kwa namna ambavyo ungeweza kumnyanyua benchi na kuweka kukunyayua kwenye kiti ulichokuwa umekikalia kwa wasiwasi.

Mshale wa saa umesogea kwa kasi tangu hapo na tumeshuhudia mengi kuanzia vita za uwanja wa mazoezi wa Carrington kati ya Pogba na Mourinho mpaka kwa klabu kama Watford kuonekana zinaweza kufika Old Trafford na kupageuza uwanja wa nyumbani.

Washabiki wa United hawakuwahi kuishi hivi na hivyo mahitaji ya mabadiliko yalikuwa makubwa. Mourinho alikuwa amefika katika ncha baada ya marefu yake mafupi ambayo yalikuja na mategemeo makubwa ya kurejesha ufalme hasa kutokana na rekodi yake.

Swali kubwa likawa ni kocha gani anayefaa kuja kuishi katika nchi hii iliyogeuka ya ahadi ambayo Fergusson alionekana kuwa aliishafikisha kwenye kilele cha utawala wa dunia ya soka?

Kwenye vichwa vya watendaji ambavyo naamini hata Fergie alihusika, alihitajika mtu mmoja tu naye ni yule anayeweza kuishi kwa furaha na wachezaji hiki, kocha ambaye anaweza kujenga saikolojia ya wachezaji.

Roy Keane anaufahamu utamduni wa United lakini ni wazi kuwa ni Mourinho wa pili ambaye asingeweza kutizama Pogba akitengeneza nywele. Scholes ameshawasema wachezaji vya kutosha, Ryan Giggs aliondoka bila furaha na mpaka kutizama timu za Taifa.

Inawezekana Carrick angeweza kuingia vyema lakini alikuwa sehemu ya tatizo na inawezekana asingeweza kufanya yaliyofaa huku pia uzoefu kwenye nafasi ya ukocha ukiwa mdogo. Jina peke likawa Ole ambaye amewahi kukalia kiti hicho ijapokuwa hakuwa mwenye mafanikio makubwa.

Bahati nzuri ni kuwa ndoa yake na wachezaji inaonekana kupata Baraka, ukitizama kwa jicho la mbali zaidi unaona kuna mtu nyuma yake wanaishi vyema, namwona Fergie kabisa. Ukitizaa namna Rooney anavyosema alimtumia ujumbe wa mambo ya kubadili unagundua kuwa ni zoezi la wanamanchester United linaendelea.

Ole alikuwa ‘Super Sub’ wa Fergusson akiwa kocha na sasa anaonekana kuwa Super Sub ya Fergie akiwa nyumbani kwake. Kashinda michezo mine ya ligi mpaka sasa na anashinda huku ukiwa unaitizama Barcelona ndani ya jezi nyekundu.

Wachezaji wa zamani wanampenda, wanamuunga mkono na washabiki wanakumbuka mengi hivyo wanamshangilia. Fergusson alimtengeneza huyu akiwa mchezaji, na si ajabu akawa ndio anamtengeneza akiwa nyuma ya pazia.

Big G zake anazitafuna ndani ya Old Trafford, zinafanya kazi bila ya sisi kuona na United inasonga mbele. Inasemekana wanataka kumpa kazi ya kudumu, kazi ya Big G hii.

Advertisement