HOJA ZA KARUGENDO : Ninauliza, ninaomba nijibiwe

Wakazi  wa kijiji cha Bugorola wilaya  ya Ukerewe wakifuatilia mkutano wa kuhakiki taarifa za familia maskini ili kuingizwa kwenye mradi wa Tasaf machi 2015. Picha na Jovither Kaijage

Muktasari:

  • Tuliupata Uhuru wa kweli au uhuru wa Bendera? Uhuru wa kujielewa, uhuru wa kuendesha mambo yetu bila kuamuliwa na kushinikizwa na watu wengine?

Nimeamua kuuliza maswali haya, maana ni lazima atokee mtu wa kuyauliza. Haiwezekani tukasubiri miti na mawe kuyauliza. Kila Mtanzania aliyesoma, anayeguswa na uhai wa taifa letu ni lazima ayaulize.

Nimeamua kuuuliza maswali haya maana tunaelekea kujenga utamaduni wa kishenzi, wa kusema “Yakitokea nitakuwa nimeondoka”; wa kuishi leo bila kufikiria maisha ya vizazi vijavyo.

Tunaitaka Tanzania ya leo bila kuweka maanani ya kesho na keshokutwa?

Tuliupata Uhuru wa kweli au uhuru wa Bendera? Uhuru wa kujielewa, uhuru wa kuendesha mambo yetu bila kuamuliwa na kushinikizwa na watu wengine?

Tulipigana kumuondoa mtawala mkoloni na mambo yake ya kikoloni, sheria zake za kikoloni na ubaguzi ili tujenge taifa huru lenye kujitawala, lenye sheria za usawa na kuwaheshimu binadamu wote? Au tulitaka kuondoa mtawala mkoloni na kuendeleza mambo yake ya kikoloni? Tulimwondoa mkoloni ili kujenga taifa na utaifa? Haya ndiyo maswali ninayojiuliza kila kukicha!

Nimeamua kuuliza maswali haya kwa vile tumejenga utamaduni wa kuogopana na kuoneana aibu; wa kutanguliza vyama vya siasa badala ya taifa letu.

Tumejenga utamaduni wa kuwatanguliza marafiki zetu na ndugu zetu badala ya taifa. Ni lazima ajitokeze mtu wa kusema liwalo na liwe. Ni lazima ajitokeze mtu wa kukemea na kuonya.

Kuna rafiki yangu wa karibu ameniambia leo hii Tanzania hakuna wa kusimama na kukemea, maana sote tumetumbukia katika shimo la kuogopana na kulindana, na hasa ugonjwa wa kutisha wa uchu wa madaraka.

Ninauliza maswali haya nikijua wengine wataguswa, wataumia na kuchukia, nazingatia ukweli kwamba baadhi ni rafiki na ndugu zangu wa karibu; sipendi kabisa kuwasaliti, lakini kwa suala la kitaifa niko tayari kumsaliti baba, mama, kaka, dada na rafiki wa karibu. Nauliza maswali haya kwa kutambua kwamba taifa letu limeanza kuyumba.

Ninauliza: Mtumishi wa umma, mfanyakazi wa serikali anaruhusiwa kufanya kazi za chama cha siasa? Mtumishi wa umma anaruhusiwa kuwa mwanachama wa chama cha siasa? Je, maadili ya utumishi wa umma yanamruhusu mtumishi wake kuacha majukumu yake kufanya mambo mengine kama vile ya chama chake na familia yake?

Mipaka iko wapi ya mtumishi wa umma kufanya kazi zake na kufanya kazi za umma?

Kufanya kazi za serikali na kufanya kazi za chama chake? Bila mipaka ya wazi nchi itayumba!

Ninauliza: Muhimu ni chama cha siasa au ni Taifa? Tushughulikie nini, kuendeleza vyama vya kisiasa au kuliendeleza taifa letu la Tanzania? Wenye mawazo yanayofanana, mfano kwa suala wa ufisadi kwa nini wasiungane na kuwa na sauti moja hata kama wanatoka vyama tofauti?

Ninauliza: Ni nani anatupumbaza na kutuaminisha kwamba Tanzania ni nchi maskini? Hivi ni kweli au ni matatizo yaliyo kwenye vichwa vyetu. Iwe vipi nchi tajiri kama Tanzania; ardhi kubwa ya kilimo na ufugaji, maziwa, mito na Bahari kwa wingi wa samaki, misitu yenye mbao na wanyama wa kila aina na madini mengi iwe masikini?