Hiki ndicho kinachosababisha usugu wa bakteria mwilini

Friday May 31 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Siku hizi wagonjwa wengi hasa wa malaria wamekuwa na malalamiko ya kutopata nafuu hata baada ya kutumia dawa za aina fulani.

Dawa ni kemikali au kitu chochote kinachotumika kutibu, kuzuia au kutambua magonjwa ya binadamu au wanyama.

“Nikijisikia vibaya huwa nakwenda kupima, nikiambiwa ni malaria, najua ninywe dawa gani (anaitaja), lakini kuna wakati dawa iliacha kunisaidia nikabadili, siku hizi natumia (anaitaja)” anasema Faraji Rajabu.

Anaongeza kuwa dawa aliyokuwa anaitumia awali ilikuwa nzuri, kwa kuwa akinywa hachoki na pengine hamalizi dozi na anakuwa ameshapona. “Niliizoea na nilikuwa nikiona dalili za malaria nikiinywa naendelea vizuri, bila kunywa dawa za maumivu, lakini hii ya sasa lazima mwili uchemke.”

Malalamiko ya Rajabu ni miongoni mwa yanayotolewa na wagonjwa wengi wakidai dawa wanazotumia zinashindwa kuwatibu ipasavyo ikiwamo bakteria kupata usugu wa kutosikia dawa.

Hali hiyo inasababisha kumtafuta Msajili wa Baraza la Famasi nchini, Elizabeth Shekalage kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa sababu za kuwapo kwa hali hiyo.

Advertisement

Mtaalamu wa dawa azungumza

Katika mahojiano na gazeti la Mwananchi, Shekalage anazungumzia sababu za bakteria kupata usugu, matumizi sahihi ya dawa na wakati gani unaopaswa kutumia dawa.

Mwandishi: Nini kinasababisha usugu wa bakteria katika mwili?

Elizabeth Shekalage: Usugu wa bakteria husababishwa na haya yafuatayo: kwanza, maumbile ya bakteria mwenyewe kutokana na kuishi katika mwili wa binadamu na kuwa na uwezo wa kubadili maumbile na tabia ili aendelea na uhai kama dawa zitatumika kwa muda mrefu kuua bakteria.

Bakteria hujijengea kinga ya dawa hizo kwa kujibadilisha maumbile na kufanya dawa kutokuwa na athari na kutoweza kuwa na madhara kwao

Suala lingine ni kutotumia dawa kwa usahihi. Ili dawa ifanye kazi katika mwili na kuua bakteria inatakiwa itumike dawa sahihi, kwa ugonjwa sahihi, kwa kiwango sahihi na kwa muda wa matumizi sahihi ya dawa hiyo kulingana na ugonjwa uliopo.

Viwango hivyo ndiyo vinaweza kutokomeza bakteria katika mwili. Endapo dawa hazitatumika kwa usahihi, itatengeneza usugu na hivyo kutokuwa na athari na kushindwa kufanya kazi ipasavyo.

Mwandishi: Kuna madhara mtu kunywa dawa zenye gramu nyingi ili amalize dozi haraka?

Elizabeth Shekalage: Ili dawa ifanye kazi mwilini, ina kiwango maalumu (dozi) na muda wa matumizi wa dawa aliyoandikiwa mgonjwa kutumia baada ya daktari kuthibitisha ugonjwa uliopo.

Mtu kunywa dawa zenye gramu nyingi au chache tofauti na kiwango kinachotakiwa kulinga na ugonjwa uliopo kuna madhara kama ifuatavyo;

Upungufu wa gramu (dozi), kutasababisha ugonjwa kutokupona kutokana na kutotumia kiwango sahihi cha dozi kwa vimelea vya magonjwa na kutachangia kwa usugu wa dawa husika.

Kuongeza gramu (kuzidisha dozi) kunasababisha kuongeza kiwango cha dawa ambacho haitakiwi kwenye mwili hata kama ni kwa ajili ya kutibu ugonjwa, na kiwango hicho kuwa ni sumu kwenye mwili (toxicity).

Kuzidisha dozi kunasababisha kuongeza kiwango cha dawa ambacho hakitakiwi kwenye mwili na huleta madhara ya figo, ulemavu na hata kifo.

Mwandishi: Iwapo mgonjwa amepewa dawa ya siku saba, akanywa baada ya siku nne akapona, akiiacha atapata madhara yoyote kiafya?

Elizabeth Shekalage: Kama nilivyosema awali, ili dawa iweze kufanya kazi na kuponya inatakiwa itumike kwa usahihi ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda wa matibabu husika.

Mgonjwa anatakiwa asikatishe dozi, kama umeelekezwa kutumia dawa kwa muda wa siku saba, unatakiwa kukamilisha siku zote. Kukatisha dozi, kuna madhara ya usugu wa bakteria.

Kwa kuwa husababisha ugonjwa kutopona, ingawa mgonjwa anaweza kupata nafuu na kuhisi amepona lakini baada ya muda ugonjwa unaweza kurudi upya na hata kuwa na nguvu zaidi kuliko awali.

Lingine ni kuongezeka kwa gharama za matibabu, kwa kuwa kutahitajika gharama kutibu ugonjwa ambao kama ungeweza kumaliza dawa katika muda uliowekwa ungeweza kupona kabisa. Mwandishi: Je, kuna madhara iwapo dawa mfano ya malaria unayoandikiwa na daktari unaijua na ukajihisi una dalili za ugonjwa huo, ukainunua na kuinywa?

Elizabeth Shekalage: Taratibu za tiba zinaelekeza kutokutumia dawa kabla ya kufanyiwa uchunguzi na kubainisha ugonjwa utakaohitaji tiba ya dawa.

Hata hivyo, yapo magonjwa madogo madogo (minor aligments) ambayo zipo dawa zisizohitaji cheti cha daktari.

Mgonjwa anaweza kwenda kwenye famasi na kuhudumiwa na mfamasia.

Kwa kesi ya malaria, inashauriwa mgonjwa akijihisi dalili za malaria aende kwenye vituo vya kutolewa huduma za afya, akafanyiwe uchunguzi na iwapo atabainika kuwa ugonjwa huo, ndipo apatiwe tiba.

Lakini kumekuwapo na mazoea ya Watanzania wengi kuhisi dalili za malaria na kutafuta dawa na kuanza kunywa pasipo uhakika kuwa dalili hizo ni malaria au la. Si kila homa ni malaria.

Mwandishi: Nini kifanyike kuepuka usugu wa dawa?

Elizabeth Shekalage: Suala la kuepuka usugu wa dawa ni suala mtambuka linalogusa sekta mbalimbali kama vile afya, kilimo, mifugo, uvuvi na jamii kwa ujumla kwani maeneo haya kuna matumizi ya dawa ambayo yasipotumika kwa usahihi basi yanakuwa na madhara kwa binadamu.

Suala kubwa ni elimu, endapo wananchi wanatakiwa kuelimishwa kuhusu matumizi sahihi ya dawa katika maeneo yao na kukumbushwa madhara yanayoweza kutokea iwapo dawa hazitatumika kwa usahihi. Vilevile, wataalamu waliopo kwenye sekta hizi kuhakikisha maelekezo wanayotoa yanaeleweka na yanazingatiwa.

Watumiaji wa mwisho wa dawa pia kuhakikisha wanazingatia maelekezo ya wataalamu.

Advertisement