Hizi ndizo sababu za matokeo mabovu mitihani ya kitaifa Zanzibar

Tuesday January 15 2019

 

By Alex Malanga, Mwananchi [email protected]

Uhaba wa walimu na madarasa katika shule za sekondari za Zanzibar, vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia shule nyingi za visiwani humo kufanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kitaifa ya kidato cha sita kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2014 hadi 2018.

Hayo yameelezwa na wadau wa elimu, ikiwa ni pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na jumuiya ya walimu wakuu wa shule za sekondari Zanzibar (Juwaseza).

Katika kipindi hicho, kwa mujibu wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), asilimia 48 ya shule zilizofanya vibaya (tano za mwisho) katika mtihani wa taifa wa kidato cha sita zinatokea Zanzibar.

Upungufu wa walimu umechangia kwa mwaka huu mikoa ya Mjini Magharibi, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba kushika nafasi tatu za mwisho za 27, 28 na 29 kitaifa.

Hali ilivyokuwa, mwalimu mmoja katika baadhi ya shule hulazimika kufundisha darasa la wanafunzi 150 ambayo ni zaidi ya mara tatu ya kiwango kilicho wekwa na Serikali.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, SMZ ina uhaba wa walimu 952. Kwa sasa kuna walimu 5,324 wanaofundisha shule 203, huku shule za kidato cha tano na sita zikiwa ni 20.

Kulingana na idadi ya shule hizo, Zanzibar inahitaji angalau walimu 6,276 ili kuweza kuwafundisha kwa ufanisi wanafunzi 114,946 wa shule za sekondari, huku 3,610 kati yao wakiwa ni wa kidato cha tano na sita.

“Tunafanya kila tuwezalo kutatua changamoto ya upungufu wa walimu. Tuna chukua walimu kutoka Nigeria kwa ajili ya kujitolea kufundisha katika shule zetu,” Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Eekondari, Asya Issa anasema.

“Kwa jitihada tunazochukua sasa, tuna kila sababu ya kufanya vizuri katika mitihani ijayo.”

Shule ya Wasichana Ben Bella, iliyoanzishwa 1924 Unguja, Zanzibar ni miongoni mwa shule ambazo zimekuwa zikifanya vibaya zaidi katika mitihani ya Taifa ya kidato cha sita.

Katika kipindi cha miaka mitano Ben Bella inayofundisha michepuo “combinations” za PCB (Fizikia, Kemia na Biolojia), PCM (Fizikia, Kemia na Hisabati) na CBG (Kemia, Biolojia na Jiografia), imeingia mara tatu katika orodha ya shule tano za mwisho katika mitihani ya kidato cha sita.

Mkuu wa shule hiyo, Zainab Mgunda anasema mpaka mwaka jana uwiano wa wanafunzi na walimu ulikuwa, wanafunzi 90 hadi 150 kwa mwalimu.

“Ili kuwe na ufanisi katika ufundishaji inatakiwa darasa liwe la wanafunzi 45, kama inavyoshauriwa na serikali, lakini kutokana na uhaba wa madarasa ilikuwa inatulazimu kuwaweka pamoja wanafunzi mpaka 150,” anasema mkuu huyo.

Anasema walimu wanapata tabu kufundisha darasa lenye wanafunzi wengi kutokana na mchanganyiko wa wanafunzi wenye tabia tofauti.

“Katika darasa kubwa, tabia mbaya za baadhi ya wanafunzi zinaweza kusambaa kwa wengine kirahisi. Kwahiyo darasa lenye wanafunzi wachache linatoa fursa kwa mwalimu kulimudu vyema,” anasema.

“Kitu muhimu katika ufundishaji ni kuwasoma wanafunzi. Mwalimu akiwa na wanafunzi wachache ni rahisi kuwasaidia kitaaluma, pia inatoa nafasi zaidi ya wanafunzi hao kusaidiana.”

Uwiano wa wanafunzi na walimu kwa sasa katika shule ya Ben Bella umeboreka na kuwa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 30, hali inayofanya mkuu wa shule kuamini matokeo ya mitihani ijayo yatakuwa mazuri.

Hii imetokana na baadhi ya wanafunzi kuhamia shule nyingine na sababu nyingine, kutofanya vizuri kwa shule hiyo na sheria kali ambazo zimeanzishwa ili kudhibiti wanafunzi wazembe.

Ben Bella ina walimu 46 wanaofundisha wanafunzi 850 wa kidato cha kwanza mpaka cha sita, huku walimu wa kidato cha tano na sita wakiwa ni 10.

Katika jitihada za kutatua changamoto ya mwalimu mmoja kufundisha darasa la wanafunzi wengi, uongozi wa Ben Bella

una mpango wa kuongeza idadi ya madarasa.

“Tayari tumeshaandika barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mjimkongwe kuomba kibali cha kujenga madarasa katika eneo lililopo karibu na shule yetu. Ametuahidi kufanyia kazi maombi yetu,” anasema Mgunda.

Matokeo ya shule hiyo ya kidato cha sita mwaka huu yaliboreka kwa kiasi fulani, kwani ilijinasua kutoka kwenye orodha ya shule tano za mwisho zilizofanya vibaya.

Ilikuwa ya tisa katika orodha ya shule zilizofanya vibaya.

Katika matokeo hayo, hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la Kwanza. Daraja la pili walikuwa 13, daraja la tatu 74, daraja la nne 13 na daraja sifuri wawili.

Wakati huohuo, licha ya changamoto ya uwiano mkubwa wa wanafunzi kwa walimu, Lumumba, ni miongoni mwa shule za vipaji maalumu, imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita, ambapo mwaka huu imekuwa ya nne kati ya 20 Zanzibar, baada ya shule za Sos, Feza na Suza.

Mussa Mussa, mkuu wa shule hiyo ambayo mwaka huu imetoa mwanafunzi bora wa PCM kitaifa (Tanzania Bara na Zanzibar), anasema kuwa kwa wastani mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 70 wa kidato cha tano na sita.

Lumumba ina jumla ya walimu 27 wanaofundisha wanafunzi 850 wa kidato cha kwanza mpaka cha sita, huku wanaofundisha kidato cha tano na sita (wanafunzi 297) ni 11.

Wanafundisha “combinations” za PCB, PCM, PGM (Fizikia, Jiografia na Hisabati) na BCG (Biolojia, Kemia na Jiografia).

Wanafunzi 111 walihitimu kidato cha sita mwaka huu, huku licha ya changamoto ya uwiano mkubwa wa wanafunzi kwa walimu, wanafunzi 17 walipata daraja la kwanza, 49 daraja la pili, 45 daraja la tatu na hakuna aliyepata daraja la nne wala sifuri.

Kwa mfumo wa elimu ya Tanzania, mwanafunzi anayepata daraja la kwanza, pili na tatu ana nafasi kubwa ya kujiunga na elimu ya chuo kikuu.

“Hatuna upungufu mkubwa wa walimu. Sisi ni miongoni mwa shule zinazojaliwa na Serikali kwani inatuendesha kwa umakini wa kipekee na tunaishukuru kwa mwitikio chanya pale tunapohitaji walimu,” anasema Mussa.

“Kuna mafanikio makubwa ya kitaaluma hasa pale kunapokuwa na uangalizi wa karibu kwa mwanafunzi mmoja mmoja na hicho ndicho tunachofanya.

“Huwa tunawachukua wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo na kuwaweka katika makundi ya wale ambao kiwango chao cha uelewa ni kidogo na baadae tunakuja kuangalia utendaji wao,” anasema.

Mussa anasema walimu wanaomaliza mitaala yao mapema kuliko ilivyotarajiwa pia huwa na mchango mkubwa katika kupata matokeo mazuri.

Katika kuhakikisha wanapunguza uhaba wa walimu, wizara ya elimu imekuwa ikichukua walimu kutoka Nigeria kuja kujitolea.

Katika miaka minne hadi 2015 walimu 50 kutoka Nigeria waliajiriwa.

Pia, SMZ imekuwa ikinufaika na walimu wa kujitolea kutoka Uingereza, Peace Corps-USA, JICA (Japani) na KOICA (Korea Kusini).

Issa anaongeza kuwa kutokana na mradi wa kuboresha viwango vya wanafunzi katika elimu unaofadhiliwa na benki ya dunia upande wa Zanzibar, Serikali imekuwa ikiwajengea uwezo walimu kumudu ufundishaji wa masomo ya Sayansi na Hesabu.

“Tumekuwa tukifanya kila tunaloweza ili kuhakikisha tunawasaidia wanafunzi katika masomo yote,” anasema Issa.

Katibu mkuu wa Zahossa, Fadhil Mshamba anasema kutokana na baadhi ya shule kufanya vibaya walilazimika kuanzisha mitihani ya kujipima kwa wanafunzi wa kidato cha tano kabla ya kuingia kidato cha sita.

Anasema ili kuondokana na changamoto hiyo mwaka 2016 walianzisha kambi kwa ajili ya kujisomea kwa wanafunzi wa kidato cha nne na sita ikiwa ni miezi michache kabla ya mitihani ya taifa kuanza.

“Wanafunzi hawako “serious” (makini) katika kusoma kutokana na utandawazi, lakini kwa sasa inabidi walazimike kutokana na hali halisi ilivyo,” anasema Mshamba.

Amina Said mkazi wa Mtendeni, Zanzibar, ambaye binti yake anasoma Ben Bella, anasema wanafunzi wanatumia vibaya mitandao ya kijamii badala ya kuitumia kujipatia maarifa.

Advertisement