Inawezekana kulima mpunga nchi kavu

Saturday January 19 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Mpunga ni miongoni mwa mazao muhimu ya chakula nchini.

Uzalishaji wa mchele nchini kwa takwimu za mwaka 2016 ni zaidi ya tani milioni mbili. Tija ya uzalishaji kwa mkulima ni wastani wa tani 1.5 hadi 2.5 wakati katika skimu za umwagiliaji, uzalishaji unaweza kufikia hadi tani sita kwa hekta moja.

Kilimo kilichozoeleka cha mpunga ni kile cha mabondeni, kinachohitaji maji mengi.

Hata hivyo, katika zama hizi za mabadiliko ya tabianchi kumekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa mvua na maji kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kilimo cha umwagiliaji.

Ni muda mwafaka kuanza kuhimiza kilimo kinachotumia maji kwa ufanisi hususan kutumia mbegu za mpunga wa nchi kavu. Aina ya mbegu za mpunga wa nchi kavu ni fursa kwa wakulima wengi zaidi kuzalisha mpunga, bila kulazimika kuhitaji maeneo yaliyozoeleka ya mabondeni.

Kilimo cha nchi kavu

Ofisa kilimo wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Johnson Tillya anasema kuwa kilimo cha mpunga wa nchi kavu ni kile kinacholimwa maeneo yasiyo ya mabonde.

‘’Ni kilimo kinachoweza kulimwa sawa na maeneo yanayolimwa mahindi. Kwa kifupi, mpunga wa aina hii hauhitaji maji mengi,’’ anasema.

Ili kuhimiza kilimo cha mpunga cha nchi kavu, wakala umeanzisha mashamba darasa kwa ajili ya kutambulisha kilimo hicho.

Mashamba darasa hayo yalitanguliwa na mafunzo ya wakulima viongozi pamoja na wataalamu wa kilimo yaliyofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Wakulima cha Mkindo.

Kuhusu mbegu zinazofaa kwa kilimo hicho ambazo zimesambazwa kwa wakulima, Tillya anataja kuwa ni Nerica 1, Nerica 2, Nerica 4 na Nerica 7.

Mkulima mwezeshaji kutoka Kijiji cha Tawa kilichopo mkoani Morogoro, John Teofil anasema Nerica 1 ina uwezo wa kutoa mavuno kilo 1,800 kwa eka, Nerica 2 kilo 1,600, Nerica 4 kilo 2,000 na Nerica 7 kilo 2,000.

Vijiji vinavyoendesha majaribio ya kilimo cha mpunga wa nchi kavu ni Kiloka, Tawa, Kisaki na Dala. Vijiji hivyo vipo Morogoro vijijini katika safu za milima ya Ulugulu.

Makala haya kwa hisani ya mtandao wa wizara ya kilimo

Advertisement