Iyobo: Sijawahi kukerwa na maneno maneno

Sunday June 16 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dansa wa Diamond Platnumz (Simba) Mose Iyobo amesema kuwa kuna wakati hata yeye anashangazwa na umakini wa bosi wake kwenye kazi.

Akizungumza na Starehe, Iyobo amesema kuwa wanapokuwa jukwaani, licha ya Diamond kuimba na kucheza pia hutambua nani hajafanya vizuri miongoni mwa madansa wake.

“Ukitaka kujua watu huwa wanakasirika, ukizingua ukiwa jukwaani, utajua Simba hapendi mzaha na kazi yake, hasa ukiamini hakuoni.

“Unaweza kumuona anaimba na kucheza mbele ya wacheza shoo ukajua haoni mnachokifanya, lakini baada ya shoo anajua nani alizingua jukwaani na ukifanya hivyo atakuzingua hadi ushangae, mimi pia huwa nashangaa umakini wa jamaa kwenye kazi,” amesema Iyobo.

Anasema umakini wa bosi wake haujawahi kuwa changamoto kwake kwa sababu anaipenda kazi anayoifanya.

“Ninatakiwa nijiulize swali moja tu, hii kazi imenifikisha wapi, nikipata jibu nakuwa makini zaidi yake.

Advertisement

“Imenijenga kuwa makini kwenye kazi yoyote ninayofanya kwa sababu naona matokeo chanya ya kufanya hivyo.

Kuhusu kashfa na mazengwe kwa wasanii, Iyobo amesema kuwa yeye ni staa na anafanya kazi kwa karibu na staa zaidi yake hivyo kuzungumziwa vizuri au vibaya ni jambo la kawaida.

“Nitabaki kuwa Iyobo, ninatambua ninafanya nini kwenye maisha yangu, pia ninahitaji kufika wapi, hivyo maneno, vijembe, havijawahi kunikera kwa sababu ukiwa staa huwezi kukaa mbali na vitu hivyo, ”anasema Iyobo.

Anafafanua kuwa “Hakuna aliyewahi kunikera na nimejiandaa kusikia, kuona au kuambiwa vitu vya kweli na vya uongo dhidi yangu hivyo hivyo yaani,” anasema.

Advertisement