AFCON U-17: Kamati yaandaa viwanja nane, hoteli tano

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kuwa mkoa wake utapokea ugeni kuanzia wiki hii ikiwa ni maandalizi ya fainali za Afrika kwa vijana.

Alisema hiyo ni fursa kwa vitengo mbalimbali ikiwemo wafanya biashara za hoteli, usafirishaji na hata wafanyabiashara ambao wanaamini kuwa wageni watafanya biashara.

Wakati Makonda akisema hayo, Katibu wa Kamati ya Maandalizi, Leslie Liunda alisema katika mahojiano maalumu kwamba tayari viwanja na hoteli watakazofikia wachezaji na viongozi wa timu zinafahamika.

VIWANJA

Liunda anataja viwanja vitakavyotumika kuwa ni Uwanja wa Taifa na ule wa Azam Complex ulioko Chamazi.

Uwanja wa Taifa utatumika kwa mechi ya ufunguzi ambayo Tanzania itacheza na Nigeria.

Viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya mechi mbali na Taifa, pia Uwanja wa Chamazi, huku vile vya mazoezi vikiwa vya JK Youth Park, Uhuru, Gymkhana, uwanja wa Chamazi (upo pembeni ya uwanja wa mkubwa wa Chamazi) na uwanja wa shule ya kimataifa ya Hopac.

Uwanja wa Taifa umekamilisha sehemu ya marekebisho yaliyoanza baada ya mechi za Simba na AS Vita na Simba kushinda mabao 2-1 na ile ya Taifa Stars na Uganda waliosjhinda mabao 3-0.

Taarifa ya meneja wa uwanja ilisema kuwa uwanja huo hautatumika kwa mechi za Ligi Kuu na utakuwa ni kwa ajili ya mechi zinazohusu Simba kwa kuwa wameutaja CAF kuwa ndio uwanja wao wa nyumbani.

Akielekezea kuhusu ukarabati wa uwanja wa Uhuru kwa mashindano hayo, Liunda alisema; “Uwanja wa uhuru tulitaka utumike katika mechi, lakini CAF walishauri majukwaa ya kawaida nayo yawekewe vitu, kitu ambacho katika bajeti ya ukarabati fedha tuliyopewa haikutosha.

“Fedha hiyo ilitosha kubadili kapeti la uwanja, zoezi ambalo linaendelea kwenye Uwanja wa Uhuru,” alisema Liunda.

Alisema maboresho katika viwanja vyote yanaendelea ambapo viwanja hivyo vitaboreshwa kwa kiwango bora huku Azam wakiukarabati uwanja wao wenyewe, ikiwamo viwanja vitakavyotumika kwa mechi kuwa na vyumba maalumu vya kupimia ‘doping’.

Hoteli zitakazofikia timu

Akizungumzia malazi kwa timu, Liunda alisema, Serengeti Boys na Morocco zitakuwa Ledger Plaza Bahari Beach Hotel, Nigeria na Senegal zitakuwa Sea Scape.

Alisema Angola na Cameroon zenyewe zitakuwa Holiday Inn na Uganda na Guinea zimepangwa kuwa Peacock Hoteli.

“Waamuzi watakuwa Tiffany Diamond Hotel iliyoko katikati ya jiji na viongozi watafikia Hoteli ya Sea Cliff, tunatarajia kuwa na wageni 72 kutoka CAF ambao ni viongozi na wafanyakazi na waamuzi 24,” alisema.

Alisema timu zote zinafahamu hoteli watakazofikia na zinaweza kutuma watu wake kwa ajili ya kuangalia mazingira.