Kila mgogoro wa ardhi una mahakama yake

Muktasari:

  • Migogoro haiepukiki kwenye jamii lakini takwimu za iliyopo kwenye sekta ya ardhi ni mingi zaidi. Wapo wengi wamepoteza haki zao kwa sababu moja au nyingine. Ili jambo hili lisikukute, ni vyema ukafahamu mgogoro wako unapaswa kuupeleka kwenye chombo gani cha haki.

Mgogoro ni hali ya kutoafikiana au kutosikilizana baina ya pande mbili inayoweza kuzua vurugu. Kwenye ardhi tunazungumzia hali ya kutoafikiana, kutoelewana au kutokubaliana jambo kuhusiana na ardhi kati ya pande mbili.

Migogoro husababishwa na mambo mengi ikiwamo umilikishwaji wa watu wawili eneo moja, uvamizi wa eneo, kuvunjwa kwa mkataba wa mauziano kati ya muuzaji na mnunuzi, kuvunjwa kwa mkataba wa upangaji au matumizi mabaya ya eneo yanayosababisha madhara kwa majirani.

Vipo vyombo vya kusuluhisha hivyo jambo la msingi ni kufahamu unatakiwa ikawasilishe katika chombo gani kati ya vilivyopo maana kila mgogoro una mahali pake na kutoupeleka mgogoro wako mahali sahihi inaweza kukufanya ushindwe au uchelewe kupata haki zako.

Hii inaanzia ngazi ya kijiji ambako kuna baraza la ardhi ikifuatiwa na baraza la kata kisha baraza la ardhi na nyumba la wilaya, mahakama kuu na mahakama ya rufaa.

Baraza la kijiji lina mamlaka ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanakijiji, kuitisha mikutano ya kusikiliza migogoro ya ardhi na kusuluhisha. Endapo hutaridhika na uamuzi wa baraza hili unaweza kukata rufaa baraza la la kata ambalo husikiliza kesi za ardhi isiyozidi Sh3 milioni. Wanasheria hawaruhusiwi katika baraza hili.

Baraza linaweza kuamuru urejesheshewe wa umiliki wa ardhi, utekelezaji wa mkataba, zuio, fidia, gharama, au amri yoyote itakaloona inafaa kwa mujibu wa sheria.

Utekelezaji wa amri yoyote inayotolewa na baraza hili ni lazima ufanyike kupitia baraza la wilaya. Ikiwa hujaridhika na uamuzi wake unaweza kukata rufaa baraza la wilaya ndani ya siku 45 kuanzia siku ya hukumu.

Baraza la ardhi na nyumba la wilaya lina mamlaka ya kusikiliza na kuitolea uamuzi migogoro ya ardhi au mali isiyohamishika isiyozidi thamani ya Sh50 milioni na mali inayohamishika isiyozidi Sh40 milioni. Wanasheria wanaruhusiwa kuwawakilisha wateja wao.

Uamuzi wa baraza hili unaweza kutekelezwa na baraza lenyewe au baraza lenye mamlaka sawa au mahakama kuu. usiporidhika unaweza kukata rufaa mahakama kuu ndani ya siku 60.

Mahakama kuu inacho kitengo cha ardhi maalumu kwa ajili ya kushughulikia kesi na masuala ya ardhi. Inaongozwa na jaji na ina mamlaka ya kusikiliza kesi za ardhi na nyumba zinazozidi Sh50 milioni kwa mali isiyohamishika na zinazozidi Sh40 milioni kwa zinazohamishika.

Katika hatua hii pia mwanasheria anahitajika kwa ajili ya ushauri na uandaaji wa nyaraka mbalimbali za kesi ikiwa ni pamoja na kuisimamia kwa ujumla. Mahakama hii ina mamlaka ya kusikiliza kesi zinazoihusu Serikali, kusikiliza rufaa kutoka baraza la ardhi na nyumba la wilaya.

Hata hivyo, mahakama kuu yoyote inao uwezo wa kusilikiliza kesi za ardhi pamoja na kitengo maalum cha ardhi endapo hujaridhika na uamuzi wa mahakama kuu unaweza kukata rufaa mahakama ya rufaa baada ya kupata kibali cha mahakama kuu.

Mahakama ya rufaa ya Tanzania ina mamlaka ya kupokea kesi zote zinazotoka katika mahakama kuu kitengo cha ardhi. Kumbuka, mahakama ya rufaa ndiyo yenye mamlaka ya mwisho ya uamuzi wa kimahakama nchini.

Huwezi kufungua kesi mpya mahakama ya rufaa isipokuwa unaruhusiwa kukata rufaa au kuomba marejeo ya uamuzi katika mahakama ya rufaa baada ya kutoridhishwa na uamuzi aa mahakama kuu.

Hakikisha unafahamu mamlaka ya kila chombo ili uweze kuchukua hatua. Usikubali kupoteza haki zako wakati vyombo vya sheria vipo. Chukua hatua!