Kuondolewa kizazi na kukosa hamu ya kujamiiana - 2

Friday May 10 2019Dk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

Kuondolewa kizazi kwa upasuaji, kitabibu hujulikana kama Hysterectomy na hufanyika kwasababu za kiafya au kwa hiari. Uanishaji wa aina za upasuaji huu unategemeana na namna ulivyofanyika na kiungo kilichoondolewa.

Hata hivyo, kuondolewa kizazi hakumfanyi mwanamke wakati wakujamiiana kushindwa kufika kileleni baada ya kupona jeraha la upasuaji.

Kama mwanamke atajihisi hayuko tayari kujamiiana baada ya kipindi kilichopangwa na watalaamu wa afya tangu atolewe kizazi asiwe na wasiwasi, kwa kuwa kila mwanamke ana matokeo tofauti baada ya upasuaji huo.

Ikumbukwe kuwa kuondoa kiungo hiki mwilini kwa mwanamke si jambo dogo, wengi huwaacha wakiwa na huzuni.

Matukio haya humfanya kuwa na shinikizo la kiakili, kuumia kihisia na kumfanya kuwa mwoga kujamiiana, na hiyo ndiyo sababu kubwa ya wao kukosa hisia za mapenzi.

Pia, anaweza kupata matatizo mengine ya kujamiiana ikiwamo uke kuwa mkavu, kutofika kileleni, maumivu wakati wa kujamiiana na kutoka damu mara baada ya kufanya tendo hilo na mwenza wake. Vile vile kuvurugika kwa hisia zao, pia kunachangiwa na kujikita zaidi katika kushikamana na maelekezo ya daktari wakati wanapojiuguza nyumbani. Mfano anaweza kuelekezwa kutumia dawa, vyakula, shughuli asizotakiwa kufanya na mazoezi mepesi ya kufanya. Vitu hivi vinaweza kuhamisha akili yake na asijikite katika hisia za mapenzi.

Kwa wanawake ambao wamefanyiwa upasuaji huu na kuondolewa kokwa za kike (ovary) na nyumba ya uzazi hii itasababisha kufikia ukomo wa hedhi kwakuwa zile homoni zinazoleta mizunguko ya hedhi hazitazalishwa tena. Athari yake ni pamoja na viwango vya homoni za kike kubadilika, hii ina athari katika maisha ya mwanamke kwa upande wa kujamiiana, ndiyo maana tunashauri mwanamke wa aina hii pale anapoona mabadiliko haya kufika mapema katika huduma za afya.

Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu

Advertisement