Kwa Rayvan kazi zake zote ngumu

Sunday June 16 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kama wewe ni mtunzi na unatunga bila kufikiria huo wimbo unaimbwaje unahitaji darasa kutoka kwa staa wa lebo ya WCB Raymond Mwakyusa maarufu Rayvanny.

Mkali huyo wa nyimbo Zezeta, Chombo, Pochi Nene na Unaibiwa, amesema kuwa anapoandika wimbo, kwanza hufikiria mashairi ya wimbo husika ni rahisi kusikilizwa na namna utakavyoimbwa hautakuwa kelele badala ya burudani.

Amesema ndiyo maana kila muziki anaoandika, anaoshirikishwa ni mgumu kwa sababu anazingatia sana hilo.

“Naogopa sana kumsikiliza mpenzi, shabiki wa nyimbo ninazoimba kwenye kelele badala ya burudani,” amesema Rayvan alipokuwa akifanyiwa mahojiano na Dizzim online.

Amesema kuwa si rahisi kufanya kitu unachotarajia kipendwe na mtu mwingine ambaye hakuwepo wakati unakitayarisha, ndiyo maana kila kazi kwake ni ngumu.

“Ili kujitofautisha na wengine, lazima uumize kichwa, lakini uwafikirie unaowapelekea hicho ulichokifanya tofauti watakikubali, watakuelewa, ndiyo maana napenda kutunga mashairi yanayosikika, ambayo shabiki, mpenzi itakuwa rahisi kwake kuimba pamoja nami,” amesema Rayvan.

Advertisement

“Kutunga wimbo utakaokubaliwa na mashabiki ni kazi, lakini inaweza kuwa si kazi kubwa iwapo utaupanga wimbo utaimbwaje kabla haujatoka, ambapo mtayarishaji na washauri watakuwa na kazi ndogo ya kuuboresha, kuliko kujiandikia kama kasuku,” amesema.

Amefafanua kuwa ana ngoma nyingi alizotunga, ila zinatoka kulingana na uongozi unavyoamua.

“Kwangu nidhamu ni kila kitu, nathamini sana mawazo, mwongozo wa viongozi wangu, kwa sababu mara zote yamekuwa na matokeo chanya.

“Nikifanya kitu bila kuelekezwa najiona kama nimepungua kitu, hivyo ushauri, mwongozo na usimamizi uliotukuka ndiyo ngao na silaha ya hapa nilipo.

“Nimefika nisipopatarajia, lakini naamini kutokana na uongozi nilionao nitafika mbali zaidi,” amesema Rayvan.

Advertisement