Lionel Messi amchanganya dogo wa Tanzania huko Hispania

Muktasari:

  • Maisha yamebadilika na kama milango kwa nyota wa Kitanzania imefunguka maana kila kukicha kumekuwa na nafasi kadhaa ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa nyota hao.

Miaka kadhaa nyuma kulikuwa na ugumu kwa wachezaji wa Kitanzania kupata nafasi za kwenda kufanya majaribio ya kujiunga na klabu mbalimbali barani Ulaya.

Maisha yamebadilika na kama milango kwa nyota wa Kitanzania imefunguka maana kila kukicha kumekuwa na nafasi kadhaa ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa nyota hao.

Hivi karibuni kinda la Kitanzania, Adrian Kitare lilitua Hispania kufanya majaribio ya kujiunga na akademi ya FC Barcelona ambayo inafahamika zaidi kama La Masia. Achana na Farid Mussa na Shaaban Idd Chilunda ambao wako CD Tenerife.

Spoti Mikiki imeongea na Kitare ambaye ametembelea ofisi zetu zilizopo Tabata jijini Dar es Salaam, mara baada ya kurejea na kuelezea mchakato mzima ulivyokuwa hadi akapata nafasi hiyo adhimu ambayo anadai ameitumia vyema.

Kitare anasema kuwa aliyehusika moja kwa moja ni baba yake ambaye siku zote anadai amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha anafanikisha ndoto zake za kucheza soka Ulaya.

“Baba alianza kuniombea nafasi Marekani kwenye kituo chao kidogo, lakini mambo hayakwenda sawa na nikakosa visa, ikabidi tuombe nafasi ya upendeleo Hispania.

“Walitaka vielelezo vyangu kama vile picha na video zikionyesha uwezo wangu, haikuwa kazi kubwa maana tayari video nilikuwa nazo nyingi na nilizitengeneza nikiwa kwenye akademi ya Sunderland ile ya JKYP pale Kidongo Chekundu,” anasema.

Baada ya kutuma video zake, Kitare alikubaliwa kwenda Hispania kufanya majaribio hayo ambayo yalikuwa ni ya wiki moja kasoro.

Alitua Hispania na mara moja akaanza majaribio hayo akiwa na nyota wengine kutoka kwenye mataifa kama Argentina, Brazil, Denmark na kwingineko.

Kitare ambaye anamuda ushambuliaji, anasema alikuwa mchezaji pekee kutoka Afrika na hakukutana na changamoto ya lugha kutokana na waongoza majaribio hayo kuzungumza Kingereza na Kihispania.

“Tulikuwa tukifanya majaribio ya namna nyingi, nadhani hata nje ya uwanja walikuwa wakitupima maana nilikuwa nikiwaona wanarekodi vitu kwenye karatasi zao kipindi ambacho tulikuwa tukipiga stori nao za kawaida.

“Nidhamu na yenyewe walikuwa wakiipa kipaumbele kuna muda walikuwa wakiwatumia vijana wengine ambao wapo nje ya majaribio kwa lengo la uchokozi lakini nilitambua nini ambacho kimenipeleka pale, sina wepesi wa kuchukia kwa hiyo niliishia kucheza na kuachana nao,” anasema.

Kitare ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano, St Mary ya Tabata anasema uwanjani walikuwa wakitazamwa namna ambavyo wanaachia mipira kwa wakati na walivyokuwa wakicheza kwenye nafasi.

Kinda huyo anasema kucheza kwa nafasi ni miongoni mwa vitu ambavyo alikuwa akifundishwa kwenye kituo cha Sunderland kwa hiyo hakikuwa kitu kipya kwake.

“Mjaribio yalienda hivyo kuanzia siku ya kwanza, lakini katika majaribio hayo kuna kipindi tulikuwa tukijigawa na kucheza kupasiana, kilichokuwa kikifanyika ni kwamba timu iliyokuwa inapiga pasi 15 bila ya mpira kuguswa ni bao.

“Lengo nadhani lilikuwa kwenye kuona ni kwa namna gani tulichokuwa tukikifanya cha kucheza kwenye nafasi tunaweza kukifanyia kazi, nilikuwa nikifungua na kuomba pasi na kuachia, sikutaka mambo mengi kwa kupiga vyenga,” ansema.

Kitare anadai walicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya kituo kingine cha FC Barcelona ambao hakuwatambua kama nao walikuja kufanya majaribio au walikuwa ni wachezaji wao ambao wapo kwenye akademi.

Katika mchezo huo wa kirafiki, kinda huyo wa Kitanzania anasema alicheza na kufunga mabao mawili kati ya matano ambayo walishinda dhidi ya vijana wenzao na mwishowe akahojiwa na chombo kimoja cha habari.

Kabla ya kumalizika kwa majaribio, Kitare anasema walipata nafasi ya kumuona nyota wa Barcelona, Leonel Messi kwa mbali akiwa anaripoti kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Hispania maarufu kama La Liga.

“Wenzangu walichachamaa wakagoma kuingia kwenye gari na wakaanza kumshangilia Messi ndipo aliposimama na kutupungia mkono huku akitabasamu baada ya hapo akaondoka ndipo wenzangu walipoingia kwenye gari.

“Nilitamani kumshika mkono kwa sababu ni mchezaji ninaye mpenda ila mazingira hayakuruhusu maana kulikuwa na uzio hata hivyo nilifurahi kumuona,” anasema kinda huyo.

Kitare anasema matarajio yake ni kupata nafasi ya kujiunga na akademi hiyo na kama asipopata atatumia mawasiliano aliyoyapata kwenye majaribio hayo kwa kuangalia uwezekano wa kujiunga na timu nyingine.

Dogo huyo anaweka wazi kuwa wakati alipokuwa akifanya majaribio alipata mawasiliano ya watu ambao walionyesha kuvutiwa na kiwango chake.

“Mzee ndiye msimamizi wangu kwa hiyo ataangalia kipi ni sahihi kwa wakati huo baada ya kutoka kwa majibu,” anasema Kitare mwenye umri wa miaka 17.

Ndoto kubwa za kinda huyo ni kupasua anga kwa kucheza soka la kulipwa barani Ulaya kama ilivyo kwa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anayekipa KRC Genk ya Ubelgiji.