Maalim Seif aanza kulainisha msimamo

Wednesday January 16 2019

 

By Muhammed Khamis, Mwananchi [email protected]

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ni kama amebadili gia angani kuhusu matumaini ambayo amekuwa akiwapa wafuasi wake.

Akizungumza katika ziara ya kichama kisiwani Pemba iliyopata mapokezi yenye hamasa, Maalim Seif alisema bado anaamini kuwa haki ya Wazanzibari ipo na itarejea, ingawaje hajui lini haki hiyo itapatikana.

Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Wete katika mkutano wa ndani uliofanyika Shehia ya Mtambwe.

Kauli hii ni tofauti na ile ya awali ya kujipa matumaini ya muda mfupi, kwamba hata miezi mitatu haingemalizika bila kuwapo mabadiliko ya uongozi Zanzibar.

Maalim Seif amekuwa akitoa kauli hizo tangu mwaka 2015 baada ya kufutwa kwa uchaguzi mkuu aliodai kuwa alikuwa ameshinda. Hata baada ya kuitishwa uchaguzi mpya Machi 2016 yeye alikataa kushiriki.

Wangu wakati huo kila alipopata fursa ya kuzungumza na wananchi amekuwa anasema bado dunia haijawatupa mkono inaliangalia suala la Zanzibar, uchaguzi mkuu wa 2015 kwa ukaribu sana.

Anasema katika kuthibitisha hili ndiyo maana kumekuwa na zuio kubwa la misaada kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kutoka mataifa mbalimbali, sababu kubwa akisema ni kukiuka haki ya wananchi kupitia uchaguzi huo.

Alisema kutotendeka haki ndiyo sababu ya kuizuiwa misaada lakini wapo wanaosema kwamba yeye amekuwa sababu ya kuzuiwa kwa misaada kutokana na ziara zake nje.

Hamadi alisema hahusiki na jambo hili bali mazingira hayo yametokana na haki kupindishwa na kupewa wasiostahiki.

Wanaochoka wakae pembeni

Sambamba na hayo muda wote Maalim Seif katika ziara hiyo alikuwa na msimamo mpya ambao ni nadra kusikika akisema kwamba ‘aliyechoka akae pembeni’ ila wao wataendelea na mapambano ya kudai kile wanachoamini ni haki yao.

Kauli hii ya Hamad huenda imesukumwa na mgogoro ndani ya chama hicho na upande unaomuunga mkono mwenyekiti wa chama anayetambuliwa na ofisi za msajili, Profesa Ibrahim Lipumba

Mkazi mmoja wa Pemba, Hafdhi Ally ambaye alisema kauli za Maalim Seif za hivi karibuni zinafikirisha sana.

Msomi huyo wa uongozi wa biashara alisema ni dhahiri kwamba matarajio ya Maalim Seif ya uwepo wa mabadiliko ya kiutawala hayapo tena, badala yake anajaribu kuwaandaa wananchi kisaikolojia ili kukubali hali hiyo.

Anasema kauli za kiongozi huyo zimebadilika kutoka ‘kesho’ na sasa imekuwa ‘sijui lini’ huku muda ukiyoyoma na watu wanaendelea na shughuli zao, tahamaki uchaguzi mwingine umefika.

Alisema Maalim Seif ni kiongozi mkongwe mwenye kila aina ya mbinu za kisiasa na anachokifanya sasa ni kutumia uzoefu wake kuendelea kuishi kwenye akili za watu.

Hafidhi pia alisema wakati umefika kwa kiongozi huyo kuwa wazi kwa kila jambo kuliko kubaki kuwacha wananchi wakiendelea kuwa na tamaa huku akitambua kuwa hakuna mabadiliko ya kiutawala bila uchaguzi.

Mwanachama wa chama hicho, Rashid Ahmad Awadhi alisema wapo baadhi ya wanachama wanye kufikiria mbali juu ya kauli za kiongozi huyo lakini wanaendelea kuamini kile akisemacho kwa sababu tu hakuna sehemu nyingine ambayo wao wanahisi ni sahihi na CUF imefanikiwa kuwajenga wanachama wake kutokuwa wadadisi.

Advertisement