Makosa aliyoyafanya Mwalimu Nyerere yameanza kujirudia

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere

Muktasari:

Ukiangalia historia ya Uhuru wa Tanganyika na baadaye Tanzania chini ya Mwalimu Julius Nyerere, utaona inaanza kujirudia katika utawala wa sasa hata kama siyo kwa kila kitu.

Historia ni mwalimu mzuri katika maisha kwa sababu inaeleza unakotoka na kukuwezesha kujua ulipo na unakoelekea. Tabia ya historia ni kujirudia.

Ukiangalia historia ya Uhuru wa Tanganyika na baadaye Tanzania chini ya Mwalimu Julius Nyerere, utaona inaanza kujirudia katika utawala wa sasa hata kama siyo kwa kila kitu.

Mwalimu Nyerere alipoingia madarakani Desemba 9, 1961 alidumu kwa mwaka mmoja akiwa Waziri Mkuu na ilipofika mwaka 1962 akabadilisha Katiba ya Tanganyika na kuifanya nchi kuwa Jamhuri na yeye mwenyewe kuwa Rais ili awe na madaraka kamili ya nchi.

Kumbuka katika uchaguzi wa mwaka 1958 na mwaka 1960 zilizoshirikisha vyama vingi Tanu ilishinda. Lakini, ilipofika mwaka 1965, Mwalimu Nyerere na chama chake waliamua kuufuta mfumo wa vyama vingi na kuweka madaraka yote chini ya chama kimoja.

Mbali na vyama vya siasa, asasi za kiraia nazo zilidhibitiwa. Kwa mfano, vyama vya wafanyakazi vingi vilidhoofishwa na viongozi wake kupewa madaraka serikalini.

Vyombo vya habari navyo havikusalimika kwani magazeti na redio zikabaki kuwa za Serikali na chama tawala cha Tanu na baadaye CCM.

Mwaka 1967, Mwalimu Nyerere aliasisi na kusimamia utekelezaji wa Azimio la Arusha likiwa na miiko ya uongozi wa umma ambayo pia alitaifisha rasilimali zote za binafsi na kuzifanya kuwa za Serikali.

Kulikuwa na shule, hospitali na mashirika binafsi, yote yakawa ya Serikali. Hatua zote hizi zilikuwa ni utekelezaji wa sera ya Ujamaa na Kujitegemea. Ni sera ambayo haikuzifurahisha nchi za Magharibi zilizoamini katika ubepari.

Licha ya kumshauri mara kadhaa, Mwalimu Nyerere hakubadili mawazo yake huku akionyesha misimamo mikali dhidi ya nchi za Magharibi.

Mwalimu alijikita kwenye ukombozi wa nchi za Afrika ambazo wakati zilikuwa bado hazijapata uhuru. Alitumia hata rasilimali za nchi kufanikisha ukombozi huo.

Kulikuwa na nchi kama Afrika Kusini, Namibia, Msumbiji, Angola na Zimbabwe wapigania uhuru wake walipatiwa makazi nchini.

Wakati hayo yakiendelea, mambo yalikuwa magumu kwa sekta binafsi nchini. Kwa kuwa kila kitu kilikuwa kimetaifishwa, watu wote walijikuta wakitegemea Serikali.

Watu waliothubutu kufanya biashara ya kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi walionekana kuwa wahalifu, walanguzi, wahujumu uchumi. Ndiyo chanzo cha kutungwa kwa Sheria ya Uhujumu Uchumi Mwaka 1984.

Kulikuwa na uhaba mkubwa wa bidhaa na mahitaji muhimu ya binadamu. Kulikuwa na maduka ya kaya, wakati watu wakipanga foleni kununua sukari, sabuni, unga na mahitaji mengine. Bidhaa zikiisha ndiyo imekula kwako.

Miaka ikaendelea mbele, maisha yakaendelea kuwa magumu, mbaya zaidi ni pale Tanzania ilipopigana vita na Uganda ili kumng’oa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Idd Amin. Licha ya Tanzania kushinda vita hiyo, mambo yakaendelea kuwa magumu kiuchumi kwa sababu gharama za vita zilikuwa kubwa.

Kama hiyo haitoshi, mwanzoni mwa miaka ya 1980 ulizuka ukame mkali na kusababisha njaa kali. Kwa hiyo kila kona mambo yalikuwa magumu.

Wakati huo, mashirika ya fedha kama Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) yalimshauri Nyerere kufanya mabadiliko ya mfumo ili kujaribu kunusuru uchumi, lakini aliwakatalia kabisa. Waziri wake wa fedha, Edwin Mtei aliyeonekana kukubaliana nayo alijikuta akipoteza ajira yake. Kosa lake lilikuwa ni kuwapokea maofisa wa WB na IMF na kuwapeleka kwa Nyerere.

Pamoja na misimamo yake mikali, Mwalimu Nyerere aliona jinsi mambo yanavyomuendea kombo kiuchumi. Kwa ufupi huo ndiyo ulikuwa mwanzo wake kufikiria kung’atuka.

Mwalimu aliona hatari inayokuja kama angeendelea kuwa madarakani kama Rais, ilibidi ajiuzulu ili alinde heshima yake aliyoivuna kwa miaka 24. Kweli aliilinda. Mpaka leo Mwalimu Nyerere ana heshima kubwa kitaifa na kimataifa.

Hata alipostaafu, Mwalimu Nyerere alijutia baadhi ya makosa yake na aliandika kitabu kinachoitwa ‘Tujisahihishe’ huku akiwashangaa viongozi waliomfuata kurudia makosa aliyoyafanya, japo aliendelea kuamini katika Sera ya Ujamaa na Kujitegemea na Azmio la Arusha.

Tawala zilizofuata

Walau Rais Ali Hassan Mwinyi alipoingia mwaka 1985 alisawazisha mambo baada ya kuja na sera za soko huria maarufu kama ‘ruksa’. Watu wakaruhusiwa kuagiza bidhaa, mzunguko wa fedha ukaanza kurejea. Ni kama mvua iliyonyesha baada ya ukame.

Ni kweli hata Mwinyi mwenyewe amekiri mara kadhaa kwamba mfumo wake ulisababisha hata wahalifu kuingia na hapo viongozi wa CCM na Serikali wakatumia nyadhifa zao kujitajirisha.

Wakati wa uongozi wa Rais Benjamin Mkapa alijaribu kudhibiti mapato na matumizi ya Serikali. Aliweka nidhamu ya utumishi wa umma.

Rais Jakaya Kikwete naye alirudia kidogo mfumo wa Mwinyi wa uhuru wa kiuchumi na maoni kwa wananchi. Japo kuna malalamiko ya hapa na pale, lakini Kikwete alitoa uhuru mkubwa kwa sekta binafsi kujikuza kiasi cha kuongeza ajira na ukuaji wa biashara. Serikali yake ililaumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha, lakini hakukuwa na maumivu makali kwa sababu sekta binafsi ilikuwa imeshiba.

Awamu ya tano

Sasa amekuja Rais John Magufuli. Kwa kipindi cha mwaka mmoja aliokaa madarakani tumeshuhudia akitangaza kuwa hataki siasa hadi mwaka 2020. Kwamba vyama vya siasa vya upinzani vikifanya mikutano ya hadhara na maandamano ambayo ni halali kisheria, yatamchelewesha kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.

Je, huku siyo kupiga marufuku siasa za ushindani alikofanya Mwalimu Nyerere mwaka 1965?

Mwaka mmoja tu tumeshuhudia Serikali ikizuia Bunge kuonyeshwa moja kwa moja kupitia televisheni. Sababu hazieleweki, mara gharama kubwa, mara hivi mara vile.

Tumeshuhudia vituo vya redio na magazeti yakifungiwa na sasa kuna sheria yenye utata ya huduma za habari. Sheria hii itawafunga mikono waandishi wa habari na itawanyima haki na uhuru wananchi wa kutoa maoni yao kwa Serikali. Tunarudi nyuma.

Wakati huohuo, Sheria ya Makosa ya Mitandao inaendelea kuwaminya watu haki ya uhuru wa kutoa maoni. Rais mwenyewe alishasema anatamani malaika waje waizime mitandao ya jamii. Wakati hayo yakitokea, hali ya uchumi ni mbaya. Rais Magufuli anasema ameongeza makusanyo ya kodi kwa kubana matumizi ya Serikali.

Ni kweli amepunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri, amekataa mialiko ya safari za nje, amefuta baadhi ya sherehe za kitaifa na sasa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeongeza makusanyo. Hata Rais mwenyewe ameshalalamika kuwa fedha hazipo kwenye mzunguko. Fedha ziko wapi?

Kumbe amesahau utendaji wa sekta binafsi ambazo ndizo zilikuwa zinastawisha ajira, biashara na mzunguko wa fedha umefifia.

Elias Msuya ni mwandishi wa gazeti hili. [email protected]