Makosa ambayo wazazi au walezi hufanya kuadhibu

Muktasari:

  • Mama na baba wote wawe na msimamo mmoja, siyo mmoja anakuwa tayari kuadhibu na mwingine anatetea. Au mama anasema tu kuhusu kuadhibu na kuja kushitaki kwa baba, kama vile yeye siyo mzazi bali msaidizi wa kazi.

Kosa la kwanza ni huwa ni kudekeza. Hii inatokea pale mzazi au wazazi wanaposhindwa kusimamia adhabu waliyoiweka, mara nyingine wanasema kwa mdomo tu pasipo matendo na taratibu mtoto anawasoma wazazi wake kuwa ni mbwa wasio meno.

Mtoto hapa huweza kujitetea, kulalama na kupindisha pindisha sheria au amri zilizowekwa ili tu kukwepa adhabu, na mara nyingi hufanikiwa.

Mzazi/mlezi unatakiwa kuwa imara na mwenye msimamo kusimamia ulichokisema katika kuadhibu.

Mama na baba wote wawe na msimamo mmoja, siyo mmoja anakuwa tayari kuadhibu na mwingine anatetea. Au mama anasema tu kuhusu kuadhibu na kuja kushitaki kwa baba, kama vile yeye siyo mzazi bali msaidizi wa kazi. Kama umedhamiria kutoa adhabu, basi itolewe labda tu kuwe na msamaha ambao pia unaeleweka na utamsaidia anayesamehewa siyo ajione kuwa kasamehewa kwa sababu hakustahili adhabu.

Kosa la pili ni lile linalofanywa na baadhi ya wazazi kwa kusifia au kuchochea tabia isiyofaa bila wao kujua. Kwa mfano; mtoto anapofanya kituko, badala ya kumkaripia utakuta anatazamwa na watu wataitana kumuona anachofanya.

Mfano mwingine katika hilo ni pale mtoto anapoelezea kupigwa na mwenzake na mzazi/mlezi anamwambia “na wewe mpige”, “kunja ngumi” “mtukane na wewe” huku ni kumharibu kabisa mtoto. Mzazi/mlezi adhibu kila tabia mbovu na chochea au hamasisha kila tabia iliyo njema iendelee.

Ukali wa maneno matupu hili ni kosa la mzazi hasa pale wanapopayuka au kuropoka au kuongea sana wakati anapotaka kutoa adhabu. Mfano, mtu anasema “mimi nimeshasema, hapa hapatoshi leo, lazima nimwonyeshe adabu”. Huu siyo wakati wa kutunga mashairi ya adhabu ila ni wa kuadhibu. Tumia maneno machache pasipo mihemko mingi wakati unaadhibu, elezea kwa kifupi juu ya adhabu unayotaka kuitoa na msimamo wako na kumhimiza kutenda au kufanya kile kinachombidi.

Wakati wa kuadhibu kwa kitendo au kwa maneno usizidiwe na hasira au na hisia kali, jitahidi kutuliza hasira zako, maneno yako na sauti yako kwa mtoto au yule anayeadhibiwa yawe ya kawaida na yenye ujumbe wa kueleweka na sio vitisho vitupu. Kumaanisha kwa mzazi hakupimwi na jinsi unavyo mpayukia au kumropokea anayeadabishwa, pia hakupimwi na jinsi unavyomshika na kumtingishatingisha au kumsukuma na kumuahidi vitisho bali kwa maneno ya chini, utulivu na sauti inayothibitisha msimamo wako.

Adhabu

Adhabu ni tendo au neno lolote linalotumika au kutolewa kufuatia tabia isiyofaa kwa kusudi la kuipunguza au kukomesha tabia hiyo. Adhabu zimegawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni adhabu zinazoambatana na kupewa (anayeadhibiwa analizimika kufanya kitu fulani, kazi fulani, au anapokea maumivu kwa kuchapwa au kufinywa na kundi la pili ni zile adhabu zinazoambatana na kunyimwa.

Kwa mfano anayeadhibiwa ananyimwa kufanya kitu au vitu fulani anavyovipenda au vilivyozoeleka katika maisha yake ya kila siku kama kutembea, kuangalia Luninga, kuchelewa kulala au kunyimwa mlo.

Itaendelea.......