Makosa saba ya kuepuka wakati wa usaili wa kazi

Ikiwa umeitwa kwenye usaili wa kazi, maana yake umevuka kihunzi cha kwanza katika ushindani mkubwa wa soko la ajira. Wapo wengi walioomba nafasi hiyo lakini kwa sababu moja au nyingine, maombi yao yamekwama.

Ingawa usaili ni sawa na kuchungulia mlango wa ofisi uliyoomba, bado kuna makosa endapo utayafanya, safari yako ya kuomba ajira inaweza kuendelea kuwa ndefu. Hapa ninakupitisha kwenye makosa saba yanayoweza kukugharimu.

Kuchelewa kufika

Unapokwenda kwenye usaili huku ukiwa umechelewa, unajaribu kuwaambia wanaokusaili kuwa hujali muda wao na huenda una tatizo la kupangilia mambo yako. Gharama ya uchelewaji ni pamoja na kupunguzwa kwa muda uliopangwa kukusaili, hivyo kukunyima muda wa kujieleza.

Jipange kuwahi na ukadirie muda utakaotumia kufika kwenye eneo la usaili kwa kuzingatia na sababu zilizo nje ya uwezo wako ikiwa ni pamoja na foleni, matatizo ya usafiri na mambo kama hayo.

Kama imetokea kweli umechelewa, wasiliana na wahusika na waeleze kinachoendelea.

Kutoonekana nadhifu

Mavazi yanaongea kwa sauti kuliko kile unachozungumza. Wakati mwingine vile unavyoonekana ndivyo watu watakavyokuchukulia.

Epuka kuvaa upendavyo. Mavazi unayojua watu wanayachukulia kama ukosefu wa heshima, achana nayo. Nenda kwenye usaili ukiwa nadhifu. Chunguza kampuni ina utaratibu gani kuhusu mavazi kisha onekana vile unavyotajiwa kuonekana. Ikiwa wafanyakazi wa kampuni huvaa tai, usiiache. Kama gauni refu ndiyo vazi rasmi, usiende na gauni fupi.

Kumchafua mwajiri aliyepita

Maswali ya usaili yanaweza kukuchokoza ukajikuta unajitetea kwa kumsema vibaya mwajiri wako wa zamani. Mfano unaulizwa sababu za kuacha kazi iliyopita ndani ya muda mfupi. Usipofikiria vizuri unaweza kuishia kumchafua mwajiri aliyepita.

Kumbuka maofisa waajiri wanaweza kuwasiliana na mwajiri wako aliyepita na wakati mwingine wanaweza kuwafahamu vizuri hao unaowasema vibaya. Epuka kuzungumza lugha mbaya dhidi ya mwajiri wako aliyepita hata kama unaamini anastahili kuchafuliwa.

Unapomsema vibaya mwajiri, unawaambia wanaokusaili kuwa una tabia ya kinyongo na huna uwezo mzuri wa kutatua matatizo yako. Ukiulizwa sababu za kuacha kazi yako iliyopita, eleza kwa namna inayoonyesha ilikuwa ni sehemu ya kukua kwako kikazi. Mwajiri angependa kuajiri mtu anayeonyesha ukomavu hata pale anapotendewa isivyo haki. Maswali mengine yanalenga kugundua hilo kwako.

Kutokuwa makini

Umakini ni ile tabia ya mtu kuzingatia kile anachokifanya. Mtu makini hazungumzi akiwa anafikiri mambo mengine. Katika usaili umakini unapimwa kwa kiwango chako cha kufuatilia maswali ya wasaili kwa kina. Unapokosa umakini wakati wa usaili, unawapa wasiwasi wasaili wako utakavyoweza kuwa makini na kazi utakayopewa.

Kampuni zinapata maombi mengi ya watafuta kazi na wanaoitwa kwenye usaili ni wale walioojaribu kuonyesha umakini kwenye nyaraka walizotumia kuombea ajira. Wakati wa usaili, mwonyeshe mwajiri wako kuwa hajafanya kosa kukuita kwenye usaili. Fuatilia kila unachoulizwa kwa umakini. Mwangalie machoni kila anayekuuliza swali. Kuacha akili ikiranda randa nje wakati wa usaili kunaweza kusababisha ukajibu usichoulizwa.

Kutomfahamu mwajiri

Kutokumfahamu mwajiri wako ni kosa. Majibu ya baadhi ya maswali yanategemea kiwango chako cha uelewa wa kampuni unayotaka ikuajiri.

Usiende kwenye usaili na hujui mwajiri wako mtarajiwa anajishughulisha na nini. Fahamu historia ya kampuni, dira yake, shughuli zake, mikakati yake na mambo kama hayo. Fuatilia tovuti, kurasa za kampuni kwenye mitandao ya kijamii na ukiweza zungumza na watu wanaoifahamu kampuni.

Kutokuonyesha thamani yako

Mwajiri makini huajiri thamani siyo mtu. Huwezi kuajiriwa kama huonyeshi una nini cha ziada wasichonacho wengine. Thamani yako ni ule uwezo, ujuzi na uzoefu ulionao unaoweza kumnufaisha mwajiri wako mtarajiwa.

Jitahidi kujua changamoto kubwa zinazoikabili kampuni katika utoaji wa huduma au uendeshaji wa biashara zake. Jaribu kufahamu fursa ambazo kwa sababu moja au nyingine, kampuni bado haijazitumia vya kutosha. Kisha nenda hatua moja mbele kwa kuthibitisha kuwa unao mkakati unaoweza kuleta ufumbuzi kwa kampuni.

Kudanganya

Katika jitihada za kujenga taswira chanya hata pale usipostahili, unaweza kujikuta unajaribiwa kutoa taarifa za uongo. Mfano ni kusema uliwahi kupewa nafasi fulani kwenye kampuni iliyopita kwa lengo la kukazia madai yako kuwa unatosha kwa nafasi unayoomba. Usijaribu kufanya kosa hili.

Uongo haudumu. Uongo unaweza kukusaidia leo unapoomba kazi, lakini ukakugharimu katika kazi hiyo kesho. Fahamu waajiri wengi hufanya utafiti wanapofanya uamuzi wa kukuajiri. Historia yako inaweza kupekuliwa kwa mawasiliano na waajiri wako waliopita. Wakati mwingine mchakato wa kukufahamu unaweza kufanyika hata baada ya kuwa umeshaajiriwa. Usidaganyike kutumia uongo.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754870815, twitter: @bwaya