Matumizi sahihi ya simu janja, laptop yanavyoweza kukuinua kitaaluma

Mwaka mpya wa masomo umeanza, ni wakati wa kurudi shuleni sasa. Je wewe ni mwanafunzi aliye katika mazingira ya kupata huduma za simu, laptop au kompyuta? Kama jibu ni ndiyo jiulize unaitumiaje katika masomo yako?

Ni wazi kuwa watu wengi wamebobea katika matumizi ya mitandao ya kijamii je umewahi kujiuliza ni kwa kiasi gani unaweza kutumia teknolojia kwa ajili ya masomo.

Katika makala haya wiki hii tunakueletea nyenzo muhimu za teknolojia hasa katika matumizi ya simu janja na kompyuta zinazoweza kuwa msaada kwenye masomo yako mwanafunzi wa sekondari.

Nyezo hizo zitasaidia kuyafanya maisha yako ya shule kuwa rahisi na yenye mafanikio na kuupa nafasi ubongo kuchangamka wakati wote.

Muhimu kuliko vyote hakikisha simu au kompyuta unayotumia ina uwanja wa kutafutia (search engine), inayotumika zaidi ni Google. Hii itakusaidia kutafuta matini na kujifunza masuala ambayo yanakutatiza.

Kupitia Google unaweza kuona picha, video na hata kupata maelezo ya kina kuhusu kitu unachokitafuta.

Nyingine ni Bookrenter.co. Hii inakuwezesha kupata vitabu kwa gharama nafuu ikilinganishwa na gharama za kununua kitabu chenyewe kutoka dukani. Baada ya kufungua shule na kujua ni vitabu gani vitatumika kwa muhula mzima unaingia kwenye tovuti hii na kuviazima kwa kuvilipia gharama ndogo na unakuwa huru kuvisoma muda wowote.

Ukishakuwa na kasi katika kuandika basi jifunze namna ya kuandika nyaraka ambayo itaeleweka na kusomeka mbele ya macho ya mtu mwingine bila matatizo. Hii inahusisha kupangilia maneno kama ambavyo ungeandika kwenye karatasi, inapotakiwa herufi kubwa ikae kubwa na kwenye kituo kiwepo. Programu ambayo inahusika zaidi katika hili ni Microsoft Word, huu ndiyo uwanja utakaojimwaga kuandikia ‘assignments’ zako.

Endapo utakosea neno au kitu kompyuta inakupa uwezo wa kurekebisha na kuhifadhi ulichoandika ili kisipotee.

Dragon Dictation hii ni app ambayo unaweza kuitumia kama unasoma kitu na huwezi kuandika kwa haraka kile unachojifunza au kukisikia.

Hii inakupa fursa ya kuongea nayo ikaandika kile unachokisema kwa haraka zaidi, kisha ukapitia na kusoma utakapopata wasaa.

Hapa unaweza kuandika insha kwa kusema kile unachotaka kuandika nayo ikasikiliza itaandika kama utakavyotaka iwe.

Kwa wale wavivu wasifikiri hii ni mkombozi kwani haikufanyii kazi zako kwa kuielekeza bali inasikiliza kile unachokitamka na kukiandika kama kilivyo.