Mbatia aungana na Kakobe kutaka meza ya maridhiano

Mjadala wa wanasiasa na wadau wa siasa nchini kwa sasa unaanza kueleka katika kusaka maridhiano baina ya serikali na vyama vya siasa ili kutuliza joto la lililojaa malalamiko.

Siku chache baada ya Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe kushauri Rais John Magufuli kukaa meza moja na wanasiasa, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia ameibuka na kauli inayoshabihiana.

Kakobe alitoa ushauri huo wiki iliyopita wakati Rais Magufuli akipokea ndege ya pili aina ya Airbus na Rais akasema kuwa yuko tayari lakini kuna wanasiasa ambao wamekuwa wanatoa lugha za vitisho kuwa watamchinja.

Wakati hali ikiwa hivyo, wiki hii Mbatia ameweka msisitizo akisema “Suluhisho pekee la hali ya kisiasa nchini kwa sasa ni Rais Magufuli kukubali kukaa meza ya maridhiano na vyama vya siasa ili kunusuru hali isiwe mbaya zaidi.

Mbatia ambaye ni mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD) kinachoungwa vyama vyenye uwakilishi bungeni, anasema kwa upande wake amejaribu mara kadhaa kumshawishi kiongozi huyo kuona umuhimu wa kukutana na wapinzani ingawa mpaka sasa hilo halijafanikiwa.

“Bado hatujakata tamaa, tunaendelea kumshawishi; naamini ipo siku ataona umuhimu wa kufanya hivyo, meza ya maridhiano ndiyo njia bora ya kujenga demokrasia,” anasisitiza Mbatia.

Mbunge huyo wa Vunjo akiwa katika mahojiano maalumu alipotembelea cha habari cha magazeti ya Mwananchi Communications Limited, anasema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, hivyo kwa kushirikiana bila kukata tamaa kutawezesha mkuu wa nchi ataona umuhimu wa kufanya nao mazungumzo kwa lengo la kupata suluhisho.

Mbatia ambaye mwishoni mwa mwaka jana alikutana Ikulu na Rais Magufuli, anasema hata wakati huo ujumbe wake mkubwa ulikuwa ni kutaka maridhiano.

“La msingi ni meza ya usuluhishi; meza ya maridhiano na ndiyo maana mimi sikujikita kwenye masuala binafsi. Hata nilipohojiwa na waandishi pale Ikulu nilisema nimekuja kwa mambo ya msingi ya Taifa na ndiyo msimamo wangu mpaka kesho,” anasema.

Alipoulizwa walikubaliana nini na mwenyeji wake, Mbatia anasema Rais Magufuli aliahidi kulifanyia kazi suala hilo.

“Yeye ni taasisi na alisema ataangalia the best way (njia bora) ya kulifanyia kazi hili jambo,” alisisitiza Mbatia.

Kuhusu Rais kulalamikia vitisho vya wapinzani, Mbalia anasema kitendo hicho hakileti taswira nzuri na badala yake akamshauri awe mvumilivu na huo hauwezi kuwa msimamo wa vyama vya siasa.

“Mimi siamini kama kweli anasema ametishiwa, hii sasa sheria ichukue mkondo wake. Yeye ni amiri jeshi mkuu, nani amtishe? Lakini akumbuke kuwa ukubwa ni jalala aangalie akina Trump wanafanyiwa nini. Ukiwa kiongozi lazima haya mengine uvumilie,” aliongeza.

Mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi alisema matukio yanayoendelea nchini hayatoi picha nzuri na wapinzani vimekuwa vikilalamika kubanwa kufanya shughuli zao ikiwa ni pamoja na mikutano ya hadhara na maandamano kwa mujibu wa sheria, huku viongozi wake wakipishana mahakamani kwa tuhuma za kufanya makosa mbalimbali na baadhi yao wakitumikia vifungo.

“Ukandamizaji wa vyama vya upinzani utaipeleka nchi pabaya katika chaguzi zinazokuja,” alisema Mbatia na kutahadharisha kuwa hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kunusuru hali hiyo.

“Unasikia watu hawajaruhusiwa kufanya mkutano, hawaruhusiwi kujumuika. Haki ya msingi iliyoko kwenye Katiba ibara ya 18, haitekelezwi. Kwa hiyo kama Katiba hii inakanyagwa, ndiyo maana nasema naona giza nene mbele ya safari,” anaeleza Mbatia.

Kuhusu chama chake kupungua nguvu kutokana na viongozi wakuu kuondoka, Mbatia anasema hilo halimpi shida kwani anaamini ukubwa wa chama ni falsafa na si muundo pekee.

“Bado tupo na falsafa yetu ya utu, yaani kusimamia wananchi wawe na uhuru wa kufanya mambo yao bila kuingiliwa.

Alisema tangu awali lengo kuu la NCCR-Mageuzi ni kuwa na Katiba ya umma na kwamba wao ndiyo waanzilishi na waasisi wa mageuzi, hivyo watahakikisha hilo linatekelezeka ingawa imechukua muda mrefu kutokana na ubinafsi wa baadhi ya watu kujiona bora kuliko wengine.

Mwenyekiti huyo mwenza wa Umoja wa katiba ya Wananchi (Ukawa) anasema kwa sasa nchi inaongozwa kwa mazingaombwe huku kila mmoja akiangalia maslahi yake na kwamba matatizo ni yaleyale.

“Kama hatuna Katiba mpya hata hivi vyama vyetu ni mazingaombwe matupu, swali la kujiuliza ni je, tunatokaje?

“Hapo ndio unapoona umuhimu wa kuwa na Katiba mpya ambayo itapatikana baada ya meza ya maridhiano ili kutoka hapa tulipo.”

Kwa mtazamo wa Mbatia ni kwamba mambo mengi yanakwama kutokana na ubinafsi.

Anasema hata ushindani uliopo kuhusu Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa ni ubinafsi unaoipeleka nchi kwenye giza na inazidisha chuki.

Hatima ya kuondoa ubinafsi na kufanya maridhiano ya kisiasa yatatupeleka kwenye Katiba mpya ambayo kwa kiasi fulani ingetoa kauli ya Watanzania wanataka viongozi wa aina gani na nchi inakwenda wapi.