Mbinu za kupunguza msongo wa mawazo

Sunday March 10 2019

 

Usijimalize na kujichosha kwa kufanya kazi ngumu na majukumu mengine mazito muda wote. Jifunze kupunguza majukumu yako ya kila siku, panga ratiba na muda wa kuwa na familia, marafiki na wanaokuzunguka na kushiriki shughuli zinazofanya akili na nafsi yako ifurahie.

Kwa kufanya haya utajihisi kuongeza ufanisi wako, uwezo wako wa kuzalisha au utendaji wako utaongezeka pia. Hali yako ya kiafya na hisia itakuwa bora zaidi. Kufanya kazi kwa bidii ni jambo jema lakini baada ya hapo jipe muda wa kupumzika na kurejesha nishati yako iliyopotea wakati ukiwa unafanya kazi au majukumu mazito.

Hakikisha unaupa kipaumbele muda wako wa kupumzika kama wa kazi nyingine na kuweka uwiano huu mzuri wa kazi na nyakati za michezo au furaha itakusaidia kudhiti msongo wa mawazo.

Nawirisha mwili wako

Kuwa na nidhamu na uheshimu mwili wako katika vile unavyokula na kunywa. Jihadhari kula vitu vya sukari na vya mafuta. Vitu hivi vinaweza kuathiri virutubisho vya mwili wako na kukufanya uwe na miyumbo ya kihisia (mood swing), uwe na vipindi vya msongo wa mawazo na pia kuwa na upungufu wa nishati ya mwili.

Sukari nyingi mwilini itakufanya uwe na hamu ya kula kila mara na huongeza kiwango cha sukari kwenye damu yako, hivi vyote pia vinaweza kukusababishia matatizo ya hisia na msongo wa mawazo. Jitahidi kula mlo wenye uwiano bora wa virutubisho. Protini, matunda, mboga mboga, maji mengi ili kukufanya uongeze nishati ya mwili na kukabiliana na msongo wa mawazo kwa ufanisi.

Unaweza pia kutumia virutubisho vya ziada kama vitamini B (Vitamin B complex) na virutubisho vingine mbadala vya chakula. Hapa unaweza kupata msaada zaidi wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa afya na wa lishe.

Kizazi hiki kinasumbuliwa na kiwango kikubwa cha msongo wa mawazo kuliko vilivyopita, hali hii inatuathiri kiafya na kiakili. Kwa hiyo hauna budi kuchukua jitihada za kuuweza msongo wa mawazo kwa kumaanisha na kufanya kila uwezalo ili kuhakikisha unaimudu hali hii. Kwa kufanya hivyo si tu utaishi kwa furaha na kuwa mwenye ufanisi, pia itakuhakikishia kuepuka magonjwa ya hatari ambayo yanaweza kupoteza maisha yako.

Pata muda mzuri kulala

Kulala ni kati ya hitaji la muhimu la binadamu yeyote na ni dawa ya kupunguza msongo wa mawazo. Kukosa muda wa kulala au kulala muda mchache hukuacha kujihisi uliyechoka mwili na akili na uliyeishiwa nguvu.

Kwa kufurahia usingizi kwa muda mrefu kutakufanya ujisikie kuhuishwa na kurejeshwa kwa nguvu zilizopotea na mwili wako unakuwa tayari kukabiliana na heka heka za maisha ya kila siku.

Kawaida binadamu uhitaji saa saba hadi nane za kulala ‘usingizi wa kweli’ kila usiku ingawa unashauriwa pia kutafuta muda wa zaidi wa kulala au kupumzika na kufumba macho unapokuwa na msongo wa mawazo hata kama siyo usiku.

Jifunze kushirikisha hisia zako

Kwa kuzirundika hisia na kuficha maumivu yako ya moyo na kuacha msongo wa mawazo ulipuke kila mara hakutakusaidia lolote zaidi ya kukuongezea athari. Badala yake jifunze kuwatumia marafiki, ndugu na wanafamilia au wafanyakazi wenzako kukusaidia kukupa mrejesho wa vile ulivyo, unavyoongea, unavyofanya na kuweza kukusaidia kuyatazama mambo katika mtazamo tofauti.

Kwa kuwashirikisha wengine unavyojisikia itakusaidia pia kuzimudu hisia zako na kulitazama jambo linalokutatiza katika mtazamo mzuri. Ni vyema pia uwashirikishe wengine au kuomba msaada pale unaona umebanwa na kuzidiwa na majukumu. Utashangaa kuona jinsi kila mtu alivyo tayari kukusaidia pale unapokuwa na uhitaji, kama tu wewe utakuwa na ujasiri wa kuuliza au kuomba usaidiwe. Kuongea na mshauri wa kisaikolojia (counselor) pamoja na tabia ya kuandika hisia zako kwenye kijitabu kila siku jioni au usiku husaidia pia.

Wenzetu wa nchi za mashariki wanawafundisha watoto wao kuanzia wakiwa wadogo kuandika hisia zao na jinsi siku ilivyokwenda kila siku jioni kabla hawajalala. Hili unaweza kulifanya pia wewe na litakusaidia kupunguza fukuto zito la hisia hasi ndani yako linalosababishwa na msongo wa mawazo.

Advertisement