Mgombea urais AFP aliyeingizwa serikalini atamani uana-CCM

Saturday December 8 2018

 

By Muhammed Khamis, mwananchi [email protected]

Zanzibar. Aliyekuwa mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia chama cha Wakulima (AFP), Said Soud Mohamed amesema baada ya kuteuliwa kuwa Waziri asiye na Wizara Maalumu amegundua Ilani ya CCM ni nzuri sana.

Pia, Soud ambaye ni mwenyekiti wa chama cha upinzani cha AFP, amesema wadhifa wa Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu kwenye Serikali ya inayoongozwa na CCM, imemuwezesha kushiriki maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.

AFP ni miongoni mwa vyama vitatu vya upinzani kwa upande wa Zanzibar, ambavyo viongozi wake wamepewa nafasi za uongozi kwenye Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein.

Wapinzani wengine waliomo serikalini ni Hamad Rashid Mohamed kutoka chama cha ADC ambaye ni Waziri wa Afya na Juma Ali Khatib kutoka chama cha ADA-Tadea ambaye ni Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu.

Soud alisema ukiwa mwanasiasa ni lazima ukubali kupata au kukosa nafasi ya uongozi, hivyo hata ikitokea amekosa katika uchaguzi ujao ataendelea kuunga mkono Serikali itakayoingia madarakani ili kusukuma gurudumu la maendeleo.

Pia, alisema ndani ya SMZ kumekua na ufanisi mkubwa wa uendeshwaji wa Serikali yenye ushirikiano kwa viongozi wote na wananchi wake, jambo ambalo alidai miaka ya nyuma halikuwepo.

Alisema uwepo wa mazingira hayo unatokana na utekelezwaji vyema wa ilani ya CCM katika Serikali na wananchi kwa ujumla.

‘’Kwa kiasi kikubwa ilani ya CCM imepangika vizuri sana kuliko ilani za vyama vyote na hapo awali kabla ya kuingia kwenye Serikali hii sikuwa nikilijua hilo ila kwa sasa nimeliona,’’ aliongezea Soud.

Soud alisema kuwa muundo mzuri na wenye kutukuka wa ilani ya CCM ambayo yeye anafanyia kazi kwa sasa imekua kivutio kikubwa kwake jambo ambalo wakati mwingine hutamani kujiunga na chama hicho, lakini hukwamishwa na dhamira yake ambayo alidai imejikita zaidi kuwatetea wananchi kwenye vyombo vya kutunga sheria.

Kuhusu uchaguzi ujao alisema ameanza kutangaza nia ya kugombea nafasi ya urais huku akiwa na matumaini atarudi tena kwenye Serikali ijayo kwa vile walio wengi wameona ukweli ulivyo.

Advertisement