Mjadala wa ubora wa elimu ulivyotawala mwaka 2018

Wadau wengi wanapigania kuwapo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa sekta ya elimu .Picha ya maktaba

Muktasari:

Ni mwaka ambao pamoja na mambo mengi, ulitawaliwa na hoja ya kuwapo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa elimu nchini

Mwaka 2018 unakwisha huku mjadala mkubwa uliotawala kwa wadau wa elimu na jamii kwa jumla, ukihusu ubora wa elimu, hatma ya mpango wa elimu bila malipo, uhaba wa miundombinu, vifaa na walimu.

Ni mijadala iliyowainua watu wengi wakiwamo viongozi wastaafu, na wabunge na imekuja wakati Serikali ikitekeleza mpango wa elimu msingi bila malipo ulioanza mwaka 2016.

Hata hivyo, kumekuwa na maoni tofauti kuhusu utoaji huo wa elimu ambapo baadhi ya wadau wamesema, licha ya uandikishaji wa wanafunzi wa shule za msingi kuongezeka, ubora wa elimu kwa jumla hauzingatiwi nchini.

Miongoni wa vigogo walihoji ubora wa elimu ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye Machi 18 mwaka huu alisema kuna janga katika elimu nchini na kushauri kuitishwa kwa mdahalo wa wazi, utakaoshirikisha makundi yote ya jamii kwa ajili ya kujadili suala hilo.

Akizungumza katika hafla ya kumuaga aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Idris Kikula, Mkapa alisema:

“Ninaamini kabisa kwamba tuna crisis (janga) ninasoma katika magazeti, ninaletewa presentation (mawasilisho) kutoka sekta binafsi, walimu, private university (vyuo binafsi). Napata pia minong’ono kutoka kwa vyuo vya umma kwamba kuna (crisis) katika elimu,” alisema.

Mkapa ambaye pia ni mkuu wa chuo hicho, alisema aliwahi kuwa mhariri wa magazeti ya chama (Uhuru na Mzalendo) na baadaye ya Serikali (Daily News na Sunday News) na kwamba njia moja ya kujua mwenendo wa mambo ni kusoma barua kutoka kwa wasomaji.

“Nimeendelea kusoma magazeti sana mpaka mke wangu ananilalamikia. Lakini nyingi (barua za wasomaji) zinalalamika zinasema hivyo hivyo. Zinasema elimu yetu ina mushkeli,” alisema.

Alisema ni vyema kukaitishwa mdahalo wa uwazi ambao utashirikisha makundi yote na kusikia maoni yao, badala kuwaachia wanataaluma pekee ambao wanaegemea kwenye ujuzi.

Kitabu chawapoteza wanafunzi miaka 10

Wakati Mkapa akitoa yake ya moyoni, wadau wengine hawakuwa nyuma kueleza udhaifu uliopo katika elimu. Mtaalamu wa kujitegemea wa uhasibu Robert Chiwango alifanya uchunguzi katika baadhi ya vitabu na kugundua udhaifu mwingi.

Kwa mfano, alisema kitabu cha somo la Hisabati cha kidato cha tatu kina makosa yanayosababisha wanafunzi kufeli mtihani wa somo hilo tangu kilipoanza kutumika mwaka 2008.

Chiwango alitaja mada inayohusu uhasibu (Accounting) akisema imekosewa na husababisha wanafunzi kufeli swali Na.14 linalotoka kwenye mtihani wa kidato cha nne likiwa na alama 10.

Alitaja makosa yaliyomo kwenye mada hiyo kuwa ni pamoja na matumizi ya maneno na kukosekana kwa kanuni za kihasibu na hivyo kuwapotosha wanafunzi.

“Tukianza na vilivyokosewa ni jina la mada yenyewe, imeandikwa ‘Accounts’ kimsingi ilitakiwa iandikwe ‘Accounting’

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk Aneth Komba alisema walimu wa somo hilo hawalazimiki kukitumia, kwa sababu sera inaruhusu kutumia hata masomo yaliyomo kwenye mitandao ya intaneti. Naibu Waziri wa Elimu, William Ole Nasha alisema suala la vitabu vyenye makosa limeshajadiliwa na Serikali imechukua hatua ya kuviondoa kwenye mzunguko.

Suala la makosa kwenye vitabu vya kufundishia limeshalalamikiwa na Mbunge wa Vunjo, James Mbatia mara kadhaa bungeni na kuifanya Serikali kuchukua hatua.

Matokeo darasa la saba yafutwa

Mapema Oktoba mwaka huu Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilifuta matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa baadhi ya shule nchini kwa sababu za udanganyifu.

Shule hizo zilizofutiwa matokeo zilikuwa katika Wilaya za Kondoa jijini Dodoma, Kinondoni na Ubungo katika jiji la Dar pamoja na Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza

Katibu Mtendaji Necta, Dk Charles Msonde alisema uongozi wa Idara ya Elimu ya Chemba kwa kushirikiana na waratibu na walimu wakuu ulipanga kwa makusudi kufanya udanganyifu wa mtihani

Hata hivyo, wanafunzi hao walipangiwa tarehe ya kurudia mitihani hiyo na kuifanya upya.

Wasichana wanaopata mimba marufuku kuendelea kusoma

Kauli kuhusu wanafunzi wa kike wanaopata mimba kutorudi shuleni, nayo ilizua mjadala ndani na nje ya nchi.

Rais John Magufuli alitoa kauli hiyo wakati akihitimisha ziara ya siku tatu mkoani Pwani Juni 2017. Hata hivyo, Ilani ya CCM fungu la 52 (ii) imezungumzia suala hilo ikisema, “ Wasichana wote wa Elimumsingi wanaoacha shule kwa sababu ya kupata ujauzito wataendelea na masomo.”

Licha ya kuzua mjadala miongoni mwa wananchi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alitoa ufafanuzi akisema CCM inaunga mkono kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo iliigusa Benki ya Dunia ambayo ilizuia msaada wa Dola 300 milioni kwa Tanzania hadi suala hilo litakapowekwa vizuri.

Baada ya kuzungumza na Serikali, makamu wa Rais wa Benki ya Dunia (WB) Kanda ya Afrika, Dk Hafez Ghanem alisema kuna masharti wamekubaliana kabla Tanzania haijapewa mkopo wa Dola 300 milioni za Marekani (Sh680.5 bilioni) kwa ajili ya kuboresha elimu nchini.

Lakini akizungumza na televisheni ya BBC Focus on Africa, Waziri wa Mambo ya Nchi na Ushirikiano wa Kikanda, Balozi Augustine Mahiga alisema benki hiyo ilikubali kuachia fedha hizo baada ya Serikali kuihakikishia kuwa inabuni njia mbadala ya kuwapatia elimu wasichana watakaopata ujauzito shuleni.