Msuguano Serikali na KKKT umezalishwa, unakuzwa bila busara

Sunday June 10 2018

 

By Luqman Maloto

Februari 22, 1986, aliyekuwa Kardinali na Askofu wa Kanisa Katoliki, Jiji la Manila, Ufilipino, Jaime Sin, kupitia redio ya Kanisa hilo, Veritas for Filipinos, aliwatangazia waumini wa madhehebu hayo kujitokeza mitaani kuandamana kumwondoa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Ferdinand Marcos.

Tamko hilo la Kardinali Sin, ndilo lililosababisha maelfu ya Wafilipino kukusanyika kwenye makao makuu ya polisi, Camp Crame na makao makuu ya jeshi, Camp Aguinaldo, hivyo kuwa mwanzo wa mapinduzi ya watu wa Ufilipino (EDSA), yaliyohitimishwa Februari 25, 1986 kwa Marcos kung’oka.

Kabla ya tamko la Kardinali Sin, Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Ufilipino, lilitoa tamko kupitia kwa Rais wa baraza hilo, Askofu wa Jiji la Cebu, Kardinali Ricardo Vidal. Tamko hilo lilisema:

“Serikali inaposhindwa kuwa na uhuru wa kujisahihisha yenyewe juu ya maovu iliyowatendea watu, ni wajibu wetu wa msingi kama watu, kuifanya Serikali ijisahihishe.”

Tamko hilo la Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Ufilipino, liliendelea: “Kila mwanachama mtiifu wa Kanisa, kila jamii ya waumini, tengenezeni hukumu yenu kuhusu uchaguzi wa Februari 7, 1986.

“Muda umefika wa kutoa sauti. Ni muda wa kusahihisha makosa. Makosa yalikuwa ya kimfumo uliopangwa. Hivyo, masahihisho lazima yafanyike. Lakini, kama ni kwa uchaguzi wenyewe, unaotegemea ushiriki kamili wa watu; juu ya wanachodhamiria na wanachotaka kutenda.”

Historia ya mapinduzi ya watu wa Ufilipino (EDSA), inatambua nguvu ya Kanisa Katoliki katika kuhamasisha wananchi kumwondoa Marcos, aliyekuwa anajaribu kufanya udanganyifu ili abaki madarakani hata baada ya kushindwa na mpinzani wake, Corazon Aquino ‘Cory’ katika uchaguzi wa Februari 7, 1986.

Hata mapinduzi ya Ufilipino yaliyoung’oa utawala wa kikoloni wa Hispania Juni 12, 1898, chanzo chake ni Kanisa kupitia nadharia inayoitwa Gomburza, ikimaanishwa tukio la wahubiri watatu wa Kanisa Katoliki, Mariano Gomez, Jose Burgos na Jacinto Zamora, walionyongwa na utawala wa Hispania, Februari 17, 1872.

Baada ya wahubiri hao kuuawa, mashujaa wa wakati wote wa Ufilipino, Jose Rizal na Andres Bonifacio walibeba agenda ya mapinduzi. Jeshi likauasi utawala wa Hispania. Mapambano yakachukua nafasi kwa zaidi ya miongo miwili na nusu mpaka Juni 12, 1898, Ufilipino ilipojitangaza kuwa taifa huru.

Mantiki ya historia

Kuyapata sawia maudhui ya historia ya Ufilipino, wananchi walipomwondoa Rais Marcos madarakani, vilevile wananchi walipouangusha utawala wa Hispania baada ya mapambano makali, inabidi kujielekeza kwenye maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuhusu Serikali na dini.

Mwalimu Nyerere katika hotuba zake, alirejea mara kwa mara maneno kwamba Tanzania ni Jamhuri ambayo Serikali yake haina dini. Hata hivyo, alitoa angalizo kwamba Serikali haipaswi kupuuza uwepo wa dini. Kurudia kwake mara nyingi bila shaka kulikuwa na maana ya kuweka msisitizo ili kuwepo na zingatio la hali ya juu.

Msingi wa maneno ya Mwalimu Nyerere ni kutambua kuwa Serikali kujipambanua kidini ni hatari, vilevile ikipuuza dini hakuna usalama. Kinachotakiwa ni Serikali kutofungamana na dini yoyote, lakini kamwe isipuuze uwepo wa dini, maana wananchi inaowatawala ni waumini kwenye madhehebu yao.

Ukiipitia vizuri nadharia ya Siasa za Dini (Political Religion), ndipo unaweza kuona jinsi ambavyo Sayansi ya Siasa inavyotambua nguvu ya dini kwenye nchi. Tafsiri ya Political Religion ni Serikali yenye nguvu kitamaduni na kisiasa kwa wananchi sawasawa na imani ya kidini.

Uchambuzi wa nadharia hiyo ni kwamba Serikali ambayo inaweza kujenga ushawishi kwenye maisha yao ya ndani kabisa kwa kuoanisha siasa na tamaduni zao, ndiyo ambayo hupata mafanikio yenye kushabihiana na imani ya kidini kwa watu.

Hapo ndipo unaona busara za Mwalimu Nyerere, kwamba Tanzania ni Jamhuri ambayo Serikali yake haiamini katika dini, lakini haipuuzi uwepo wa dini. Alitambua kuwa kupuuza dini ni tatizo kubwa. Imani za watu kwenye dini zao zina kina kirefu kuliko zile za Serikali.

Nchi ambazo bado zinafuata falsafa za Karl Marx na Vladimir Lenin (Marxist-Leninist States), pia huitwa Communist States, kama Cuba, China, Laos, Vietnam na kadhalika, zimekuwa na jitihada kubwa ya kupuuza dini, lakini kadiri muda unavyokwenda taratibu zinashindwa. Dini zinachomoza na kuanza kustawi.

Katika mkumbo wa nchi zenye kupuuza dini, ipo Korea Kaskazini yenye itikadi ya Juche kwa maana ya Kujitegemea Kijamaa, ambayo ni aina nyingine ya Ukomunisti. Ukitazama shabaha yao ni kutaka wananchi waiamini Serikali yao kuliko imani za kidini. Pamoja na jitihada nyingi, dini zinaendelea kuchanua taratibu.

Hata Urusi ambayo ilikuwa nembo ya Ukomunisti, ikiwa mwasisi wa falsafa za Lenin (Leninism) na mfano wa kuiishi misingi ya Karl Marx (Marxism), vilevile ikisimama kama kiranja wa nchi za Dola ya Kisovieti (USSR), iliyokuwa na sera za kukandamiza imani za kidini, hivi sasa imenywea.

Hapa haimaanishi kutetea dini kwamba ziachwe zitawale mataifa, la! Bali waumini wapewe ruhusa ya kuabudu. Dini zisiingizwe kwenye sifa za uongozi wa Serikali na nchi, ila madhehebu yasipuuzwe. Msingi wa kutamka kuwa nchi haina dini lazima izingatie na kuheshimu uwepo wa dini.

Suala la KKKT

Kuna harufu ya uchonganishi wa nchi, ama kwa mpango maalumu au upofu wa maono. Uchonganishi huo unafanywa kati ya Serikali na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Serikali. Chanzo kikiwa waraka wa Baraza la Maaskofu wa KKKT, kuelekea Sikukuu ya Pasaka mwaka huu.

Machi 15, mwaka huu, maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), walikutana na kuandika waraka kwa waumini wao na Watanzania kwa jumla. Waraka huo waliuita Ujumbe wa Pasaka wa Baraza la Maaskofu wa KKKT. Kilichomo humo ni maonyo juu ya mambo ambayo Kanisa liliona hayapo sawa.

Kabla ya KKKT, Februari mwaka huu, Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Februari mwaka huu, lilitoa waraka kuhusu hali ya kisiasa na kijamii ilivyo nchini na kugusia, vilevile kuonya yale mambo ambayo viongozi hao waliona yanahitaji masahihisho au utatuzi.

Ukipitia hoja zote za maaskofu wa Kanisa Katoliki na KKKT, unaona malengo yao ni kujenga usawa wa kitaifa. Anayehubiri usawa ndiye hustawisha upendo. Hakuna jamii yenye kupendana ikiwa watu wake hawajioni kuwa wapo sawa. Jamii iliyogawanywa haipendani.

Maaskofu wanataka Katiba iheshimiwe, maana hiyo ndiyo ilani kuu ya maisha ya watu kwenye nchi yao. Yeyote mwenye kutetea Katiba ndiye mlinzi wa utaifa. Anayetetea au kulinda utaifa huyo anataka usawa, kwa hiyo ndiye mwenye kuipigania jamii yenye upendo.

Mara waliibuka watu na kuwashambulia maaskofu. Kejeli zikawa nyingi. Hivi kweli maaskofu walifanya makosa kuagiza Katiba iheshimiwe? Walitenda dhambi kusema kwamba usawa na haki katika ufanyaji wa shughuli za kisiasa vinapokosea kutasababisha machafuko?

Viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri upendo, maana maandiko yanasema wasiopendana si miongoni mwa watu wa Mungu. Popote panapokosekana upendo basi na chuki huchipua. Maaskofu wanaona jinsi ambavyo chuki inainyemelea nchi. Je, ilikuwa sawa maaskofu wakae kimya na wanaona chuki za kisiasa zinastawi?

Mgogoro bila busara

Hivi karibuni ilivuja barua ya Msajili wa Vyama wa Wizara ya Mambo ya Ndani, iliyoandikwa Mei 30, mwaka huu, ikienda kwa Mwenyekiti wa Maaskofu wa KKKT. Barua hiyo ilihoji ukiukwaji wa katiba, uhalali wa uongozi na uhalali wa chombo kilichoandika waraka.

Barua hiyo ilionekana ni hatua ya Serikali kulishughulikia Kanisa la KKKT kufuatia uamuzi wa kuandika waraka wao. Ijumaa iliyopita (Juni 8), Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alifanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa barua ya msajili wa vyama kwenda KKKT ni batili.

Katika kuibatilisha barua hiyo kwenda KKKT, Mwigulu alitangaza kumsimamisha kazi msajili wa vyama. Hoja ikawa; kama barua haikuwa halisi, kwamba wahalifu wa mitandaoni waliamua kufanya uchonganishi, iweje msajili asimamishwe kazi?

Ukilitazama kwa jicho bora suala la Serikali na KKKT, ni wazi msuguano ulizalishwa tangu waraka ulipotoka, ila sasa unakuzwa pasipo matumizi sahihi ya busara.

Iwe kweli wahalifu wa mitandaoni wanaleta uchonganishi au Serikali yenyewe inakataa kukosolewa na kujaribu kutumia nguvu, ukweli ni kwamba migogoro ya dini na Serikali ni hatari.

Taarifa ya mwaka 2015 inasema KKKT wana waumini zaidi milioni 6. KKKT ipo kwenye Baraza la Makanisa yote Afrika lenye jumla ya waumini milioni 120.

KKKT ni sehemu ya Shirikisho la Ulimwengu wa Kilutheri lililo na waumini milioni 74. Idadi ya Walutheri Tanzania ni zaidi ya asilimia 40 ya waliopiga kura za urais, Uchaguzi Mkuu 2015. Tukemee uchonganishi huu!

Advertisement