Msuva: Sina papara kabisa kwenda Ulaya

Monday October 1 2018

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Msimu mpya wa Ligi Kuu Morocco, ‘Batola Pro’ umeanza kwa mshambuliaji wa Tanzania, Saimon Msuva kafungua akaunti yake ya mabao, Septemba 17 kwenye mchezo wao wa pili tu dhidi ya Khouribga.

Huu ni msimu wa pili kwa Msuva kuichezea Difaa El Jadida ambayo msimu uliopita aliipigania kuwania ubingwa wa Batola Pro ambapo hata hivyo walijikuta wakiteleza mwishoni na kumaliza nafasi ya tano.

Ndani ya msimu wake wa kwanza, Msuva alipachika mabao 11 ambayo yalimfanya kuwa kinara wa mabao kwenye klabu yake na hata upande wa wachezaji wote wa kigeni ambao walikuwa wakicheza Batola Pro kwa msimu huo wa 2017/18.

Spoti Mikiki imezungumza na Msuva kuhusu malengo aliyojiwekea kwenye msimu wake wa pili wa Batola Pro, mchakato wake wa kwenda Ulaya ulipofikia na maisha yake kiujumla yalivyobadilika Morocco.

“Natamani kuwa mfungaji bora wa ligi na sio wa klabu kama ilivyokuwa msimu uliopita, sina shaka na ubora wangu kwenye ufungaji kwa kiasi kikubwa nimekuwa nikiimarika kwenye umaliziaji tofauti na Msuva wa miaka mitatu hadi minne nyuma.

“Kila siku nimekuwa nikiamini hatua moja ni msingi wa kupiga nyingine, iliwezekana kwenye msimu wangu wa kwanza kuwa mfungaji bora wa klabu basi pia naweza kuwa wa Ligi,” anasema mshambuliaji huyo.

Hesabu za Msuva anasema kuwa ni kufunga zaidi ya mabao 10 kwenye duru la kwanza la msimu ili katika duru la pili arejee na nguvu nyingine wakati huo akiwa sehemu nzuri ya kuwania kiatu cha ufungaji bora wa Batola Pro.

Licha Msuva ‘Mane wa Morocco’ kuwa na shauku ya kucheza soka la kulipwa Ulaya anasema hana papara ya ofa alizowekewa mezani na klabu kadhaa kutoka barani humo.

Msuva ambaye muda mwingine amekuwa akicheza kama namba tisa, anasema kuondoka kwake Difaa kunategemea na uamuzi ya waajiri wake ambao anamkataba nao unaomalizika 2020.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, anaipenyezea Spoti Mikiki kuwa miongoni mwa ofa walizonazo mezani ni kutoka kwa miongoni mwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’.

“Kuna ofa kama tatu na miongoni mwa taifa ambalo na lenyewe tumepokea ni Hispania, bado ninamkataba na Difaa kwa hiyo siwezi kusema ni timu zipi ambazo zimeonyesha nia ya kunihitaji.

“Ofa ya Hispania ni timu ambayo ipo Ligi Kuu. Difaa ndo wenye maamuzi ya mwisho ya wapi pakuniuza ambako kutakuwa na maslahi kwao na kwangu, lakini binafsi natamani kucheza La Liga,” anasema Msuva.

Mshambuliaji huyo anasema kinachomfanya kutamani kucheza soka la Hispania ni namna yao ya uchezaji ambayo haina tofauti sana na Morocco ambako wamekuwa wakicheza soka la kuvutia.

Aidha Msuva anasema kama itakuwa tofauti na matarajio yake haitakuwa sababu ya kumfanya ashindwe kwenda kwingine atakapopata nafasi kuonyesha makali yake. “Tunachowaza wanadamu muda mwingine huenda tofauti maana yangu ni kwamba mipango sio matumizi. Kama nitaenda kwenye mataifa mengine nitahakikisha naendana na soka lao kwa muda mfupi kama ilivyokuwa Morocco,” anasema

Upande wa maisha yake namna yalivyo Morocco, Msuva anasema yamebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuzoeana na Wamorocco ambao mwanzoni alikuwa akipata tabu kwenye mawasiliano.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, anasema asilimia kubwa ya anapokaa majirani zake wanaongea kiarabu kwa hiyo ilimbidi kujua baadhi ya maneno muhimu ya kiarabu ili aweze kufanya nao mawasiliano.

Nyota huyo, anasema japo amekuwa na mwenyeji ambaye humsaidia katika masuala mbalimbali akiwa nyumbani lakini amekuwa na utaratibu huo wa kuongea na majirani zake ili kujenga nao mahusiano mazuri.

“Naweza kusalimia kwa kiarabu kwa hiyo nachofanya ni kusalimiana nao,” anasema Msuva.

Advertisement