Muswada wa vyama vya siasa umesononesha wengi kwa mengi -1

Sunday February 10 2019

Mwenyekiti wa Chama cha Chaumma, Hashimu Rungwe

Mwenyekiti wa Chama cha Chaumma, Hashimu Rungwe akisoma tamko la vyama vya upinzani nchini linalopinga muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa wakati wa mkutano wa vyama hivyo na  waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.Picha ya Maktaba 

By Deus Kibamba

Nilikuwa mmoja wa wadau waliokaribishwa na Bunge la Tanzania wiki mbili zilizopita kwa ajili ya kutoa maoni kuhusu muswada wa marekebisho ya Sheria ya vyama vya siasa, ambayo ipo tangu mwaka 1992 mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa rasmi.

Kwa wasiofahamu, mfumo wa vyama vingi vya siasa ulikuwepo nchini wakati wa Uhuru hadi baada ya Uhuru 1961 mpaka ulipofutwa rasmi kwa mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1965.

Ingawa Sheria ya vyama vya siasa imeshawahi kufanyiwa marekebisho na mabadiliko kadhaa miaka iliyopita, muswada wa sasa ulilenga kuleta mabadiliko makubwa katika sheria.

Imenisononesha kwamba mchakato ulivyokwenda hadi kufikia kupitishwa kwa muswada huo umekuwa na chenga, figisufigisu na mizengwe mingi kiasi cha kuipata sheria ambayo haijafurahisha watetezi wa masuala ya demokrasia na ukatiba nchini na duniani.

Kutokana na hilo, nimeamua kujadili mchakato na maudhui ya sheria hiyo mpya kwa lengo la kujenga hoja ya kwamba ingefaa Rais aahirishe kuusaini muswada huo kuwa sheria ili kutoa fursa ya kurejea na kurekebisha maeneo yenye mapungufu makubwa.

Kama ilivyo ada ya utungaji sheria katika nchi yetu, kuna namna mbili za kupeleka muswada bungeni – ama kwa hati ya kawaida au kwa hati ya dharura. Kwa bahati nzuri, muswada huu ulifuata utaratibu wa kawaida. Hii ndiyo maana ulisomwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwaka mwaka 2018 na kufikishwa bungeni kwa ajili ya mchakato wa upokeaji wa maoni ya wadau. Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala iliratibu mchakato wa kupokea maoni. Nilishuhudia idadi kubwa ya watu, mashirika, asasi, idara za serikali, vyama vya siasa na wadau wengine wakifurika Dodoma kutoa maoni katika ukumbi wa Pius Msekwa, Dodoma.

Mimi nilijiunga na jopo la wataalamu wa masuala ya demokrasia ya Katiba waliosafiri chini ya mwavuli wa Jukwaa la Katiba Tanzania ambao walilenga zaidi kuliangaliza Bunge juu ya maeneo ya muswada ambayo yanakinzana na ibara za Katiba ya Tanzania, 1977 na Katiba ya Zanzibar ya 1984.

Kama kichwa cha habari kinavyosema, muswada huu umesononesha wadau walio wengi kwa mambo mengi. Kwanza, muda ambao muswada umepelekwa bungeni ulikuwa ni muafaka kuhakikisha kuwa matatizo makuu yanayohusu uendeshaji vyama vya siasa nchini yanawekwa mezani na kutafutiwa suluhu.

Kwa mfano, watu wengi tuliamini kuwa huu ndio ulikuwa muda muafaka kutafuta dawa ya vyama kutimua wanachama ambao walikuwa na nafasi za kuchaguliwa kama ubunge na udiwani kupoteza nafasi zao kwa sababu ya masharti ya kikatiba na kisheria, kuwa hakuna mtu anaweza kushikilia nafasi ya kuchaguliwa pasipo kuwa mwanachama na mdhamini wa chama cha Siasa.

Sambamba na hilo, kumekuwa na wimbi la wanasiasa kuhama vyama vyao na kuhamia chama hiki au kile huku wakileta usumbufu mkubwa kwa Tume ya Uchaguzi na wapiga kura kutokana na kuhitajika kurudiwa kwa uchaguzi katika majimbo au kata husika.

Hili limewakera na linaendelea kukera wananchi wengi, wachambuzi, watafiti na wapenda maendeleo nchini huku likibaki bila suluhu yoyote. Kutokana na hamahama na kukosekana njia mbadala ya kuziba mapengo yanayoachwa na waliohama, kumekuwa na uchaguzi unaoitishwa kila uchao kufuatia kujiengua kwa mwanasiasa katika ngazi ya ubunge, uwakilishi au udiwani.

Hili lilipaswa kutafutiwa ufumbuzi kupitia muswada huu. Ni masikitiko kwamba hakukuwa na jaribio hata la kupendekeza chochote kuhusu tatizo hilo.

Kuhusu nia ya kuuleta muswada huu wakati huu, muswada uko kimya. Kisheria, nia na ya kutungwa kwa sheria fulani huonekana katika maeneo mawili ya muswada. Kwanza na muhimu kuliko yote ni jina la muswada wenyewe kwa kirefu yaani kwa kizungu cha kisheria – Long Title. Kwa mshangao, muswada huu haukuwa na Long Title. Hii ilipelekea wadau kuishi kwa hisia tu kuhusu lengo na madhumuni haswa ya kupelekwa kwa muswada huu bungeni.

Penginepo, nia ya kutungwa kwa sheria fulani huweza kuonekana katika sehemu ya mwisho ya muswada husika ambayo huwa ni mahsusi kwa ajili ya madhumuni na malengo ya sheria.

Hapa napo kulikuwa na shida kwa sababu kukosekana kwa jina la muswada kulimaanisha kuwa hata walioandika madhumuni walipata ugumu wa kueleza nia ya kutungwa kwa sheria hii.

Kwa ujumla, kumekosekana uelewa wa pamoja wa wadau juu ya nia, sababu, madhumuni na malengo ya muswada huu hadi sheria inapitishwa bungeni.

Katika wakati fulani pale ukumbi wa Msekwa, Mwanasheria Mkuu wa zamani na mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge walijitahidi kueleza kuwa wanaona mambo fulani katika muswada ule ila yamefichwa, hayawezi kuonwa na kila mtu.

Hii ndiyo inaifanya sheria hii kupungukiwa sifa ya uzuri, kwa vile sheria nzuri hupaswa kuepuka utata na vificho kama vilivyokuwa vikionwa na kuzungumzwa na Chenge pekee ambaye ni mwanasheria gwiji. Kinyume chake, sheria nzuri inapaswa kusomwa na kueleweka na mtu yeyote. Na hii ndiyo sababu nyingine nimeona nilete mjadala wa malengo na maudhui ya muswada huu ili Watanzania wajue yaliyomo na yanayokosekana, hoja kwa hoja; kifungu kwa kifungu kama nitakavyofafanua katika makala ijayo.

Deus Kibamba ni mtafiti, mchambuzi na mhadhiri katika masuala ya siasa, uchumi na uhusiano wa Kimataifa. Ameshiriki uchambuzi wa miswada mingi ya Sheria tangu 1999. Simu: 0788 758581; email: [email protected]

Advertisement