Mwaka mmoja kabla ya uchaguzi 2020 CUF bado wararuana

Muktasari:

  • Ikiwa imesalia mwaka mmoja Tanzania iingie tena kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020 haijulikani Chama cha Wananchi (CUF) kitakuwa na hali gani kutokana na kuwa na pande mbili zinazokinzana. Katika mahojiano, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Mohamed Habib Mnyaa (pichani) anayeunga mkono upande wa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, anaeleza mambo mengi yanayoashirika kuwa mambo bado si shwari. Endelea...

Mwananchi: Ni karibu miaka miwili na nusu sasa mna mgogoro ndani ya chama, jambo linaloonekana kukidhoofisha, je, hamjaona sababu na namna ya kumaliza tofauti zenu?

Mnyaa: Ni kweli mgogoro kwenye chama chetu upo na unakihujumu sana chama katika maeneo yote ya Tanzania bara na visiwani katika kipindi ambacho tulitakiwa kujipanga ili kuja na mikakati mengine imara zaidi.

Mwananchi: Unafikiri kutokana na mgogoro huo, kweli mtaweza kushiriki uchaguzi mkuu ujao na kushinda?

Mnyaa: Hili ni nadra sana kutokea kwa sababu siasa ni mipango ambayo inatakiwa kuratibiwa mara tu uchaguzi unapomalizika ili mjipange kwa uchaguzi mwingine. Kwenye chama chetu kwa sasa hilo halipo badala yake kila siku tunakwenda mahakamani na kurudi, tahamaki miaka imemaliza na uchaguzi umefika.

Kwa kweli itakuwa kama miujiza ikitokea chama chetu kushinda na hata kupata idadi kubwa ya wabunge na wawakilishi kama tulivyozoea.

Hivyo ukweli chama chetu kitazidi kushuka na kupoteza wafuasi wengi kwa mfano hivi sasa nasikia kuna makundi ya vijana wameanza kuhama Chama na kujiunga na CCM jambo ambalo ni wazi kwamba wamechoshwa na migogoro iliopo.

Mwananchi: kwa kuwa mgogoro huu unakidhoofisha chama, hamjaona kuwa ipo haja ya kukaa na kumalizia hili nje ya mahakama?

Mnyaa: Sisi upande wetu unaongozwa na Profesa Lipumba hatuna shida na hilo na kwa mara kadha tumejaribu kutaka kumaliza jambo hili na kutumia watu wakubwa wenye nafasi zao katika dini kuzungumza na upande wa pili unaongozwa na Maalim Seif, nao hujifanya kuwa tayari lakini kila ukifika muda wa kukutana wenzetu hawaji na hatujui sababu ni nini.

Nikiri kweli kwamba ipo haja ya kumaliza tatizo hilo nje ya mahakama kwa sababu siku zote mahakama ikiamua jambo ndio imeshaamua, jambo ambalo naamini linaweza kuwa na madhara kwa upande wowote ule, kwani kila upande una wafuasi wake. Hivyo kukwepa hili bila shaka nia kuwa kitu kimoja tukaendeleza chama chetu.

Mwananchi: Bado mwaka mmoja Tanzania iingie tena kwenye uchaguzi mkuu je, ukiteuliwa na chama chako kugombea urais utakuwa tayari?

Mnyaa: Muda bado wa kulisema hilo ukizingatia kwa sasa mimi ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, natakiwa kuwekeza nguvu zangu zaidi kule hadi pale nitakapomaliza ukomo wangu mwaka 2022, hivyo kwa sasa sitaweza kusema kitu ingawa lolote linawezekana kwenye siasa.

Kwa vile lolote linawezekana kwenye siasa, basi wanachama wa chama chao ambao wao ndio wenye mamlaka wakiamua kunifanya mimi kuwa mgombea wa uraisi basi nitakuwa tayari muda ukifika.

Mwananchi: Licha ya CUF kushikilia majimbo yote 18 Pemba tangu mwaka 1995 lakini hakuna maendeleo, unafikiri sababu ni nini?

Mnyaa: Kwanza nikiri kwamba tatizo hilo lipo la uwajibikaji kwa wabunge na hata wale waliokuwa wawakilishi wanashindwa kufanya majukumu yao ya kuleta maendeleo kama walivyoahidi wakati wakiomba kura.

Ni kwamba wengi wao hujisahau na kuamua kuhamisha hata makazi maeneo mengine na kukimbia kwenye majimbo yao, jambo ambalo limekuwa likiwakosesha imani wananchi.

Mwananchi: Umesema wabunge wa CUF Pemba wanashindwa kutekeleza wajibu wao, je, kuna tofauti yoyote kati ya majimbo ya CUF na CCM katika maendeleo?

Mnyaa: Ndiyo kuna tofauti kubwa ambazo hazitaki kutumia akili nyingi kuitambua. Kwa mfano pita karibu majimbo yote ya Unguja uone wana magari maalumu ya kutoa huduma za wagonjwa, jambo ambalo halipo kwenye majimbo ya Pemba.

Pia majimbo yanayoongozwa na CCM si rahisi kukuta changamoto ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama na ndio maana kila muda unaona usambazwaji wa mabomba.

Mwananchi: Umesema wawakilishi wa Pemba hawatekelezi wajibu wao, je, ni muda wakati tunaweza kuwabebesha lawama hii na Serikali inalibeba jukumu muda gani?

Mnyaa: Kila mtu ana wajibu wake, nafahamu Serikali ina wajibu wa kuleta maendeleo kwa wananchi lakini pia wawakilishi na wabunge nao wana wajibu wao.

Licha ya kuwa wakati mwingine wanashindwa kutekeleza majukumu hayo lakini hushindwa hata kutetea bungeni.

Hata hivyo Serikali nayo inapaswa kufanya jukumu lake wasitumie vigezo vya uwepo wa viongozi wengine wa vyama vya siasa na kushindwa kutekeleza wanayopaswa kuwafanyika wananchi.

Mwananchi: Unadhani ni kwa nini tangu kumalizika kwa uchaguzi mwaka 2015 wabunge wengu hawafanyi mikutano na wananchi wakati haijakatazwa?

Mnyaa: Haya ndio yaleyale ambayo niliyasema huko nyumba kwa sababu wabunge hao hawatendi wajibu wao hushindwa kurudi kwa wananchi ikiwemo kufanya mikutano hio wakiamini kwamba wanaweza kuadhibiwa.

Uwepo wa mazingira haya ni wazi kuwa hata hawa wabunge wa chama chetu wamekuwa wakikihujumu chama kwa maslahi yao. Hivi ni mwananchi wa aina gani atakayekuwa tayari kuona mtu aliyemchagua anashindwa kutenda wajibu wake kisha mtu huyohuyo awe tayari kupiga tena kura kumchagua kwa awamu nyengine.

Bila shaka wabunge wanapaswa kujitathimini upya vinginevyo wanakwenda kukimaliza chama chetu hata huko Pemba ambako nako wananchi wameanza kuamka na kuona kuwa waliowapa dhamana hawawatendei haki badala yake huweka mbele zaidi maslahi yao.