Mwanamke ni SIEIJII, kwa nini asijue mshahara wako halisi

Sunday April 14 2019

 

By Kelvin Kagambo

Je, mke wako anastahili kufahamu ukweli wa kipato chako? Yaani mfano kama ni mwajiriwa, ajue unalipwa mshahara kiasi gani kwa mwezi.

Asilimia kubwa ya wanaosema ndiyo ni wanaume ambao wanajaribu kuishi maisha ya uhalisia lakini uhalisia unawakataa. Hao ndio ambao wake zao wanafahamu wanaingiza kiasi gani, kwa hiyo kwa sababu mwanamke yuko vizuri zaidi ya mwanaume kwenye kupanga bajeti za nyumbani, basi anaupigia hesabu mshahara wote kwenye chakula, ada za watoto, umeme, kodi, nauli na kila kitu, isipokuwa pesa ya kumpa mwanaume kwa ajili ya matumizi yake binafsi.

Kwa hiyo mwanaume anakabidhisha pesa zote kwa mwanamke kwa sababu anafahamu ni kiasi gani na sasa anakuwa kama mwanafunzi, kila asubuhi anaomba pesa ya nauli kutoka kwa mama.

Hawezi kwenda baa kwa sababu pesa ya hizo habari haikuwa kwenye hesabu za mama, hawezi kumpa pesa mdogo wake wa kike anunue wigi jipya kwa sababu waziri wa fedha hakuweka hilo kwenye daftari lake la matumizi, hawezi kununua shati jipya analopenda, hawezi kufanya chochote ambacho kinahitaji pesa na hakihitaji sana mwanamke ajue – hana pesa binafsi, mshahara wote uko chini ya uangalizi wa SIEIJII.

Wanaume wa hivi ndiyo huishi kama wanacheza filamu za Bongo Movie au vichekesho vya marehemu King Majuto. Utakuta baada ya wiki moja mbili tangu alipwe mshahara anarudi kwa mke wake mikono nyuma na kuanza kuazima pesa, kwamba atairudisha siku mbili tatu. SIEIJII akiuliza pesa inakwenda wapi anaweza akadanganya kwamba, Rafiki yangu Meshaki kapata tatizo kidogo, nataka nimuazime.

Sasa kwa nini pesa yako mwenyewe ikuendeshe kiasi hiki. Ukweli ni wanawake wanapenda sana tuwaambie kila ukweli kuhusu sisi, lakini ubaya ni kwamba sisi pia ni binadamu, tunafanya upuuzi na ujinga, kwa hiyo tukisema wajue kila ukweli wetu tutatukuwa tunaharibu badala ya kujenga namaanisha kuna nafasi ya kufanya uongo kidogo. Sasa kama hiyo ipo, kwa nini tusidanganye na kamshahara hapo. Yaani ukapungua hata kalaki au kalaki mbili kulingana na uhitaji wako, kisha yeye akawa anajua unalipwa kiasi fulani, na kweli ukampa hiko anachojua, kumbe mzee una kiakiba chako kimekaa chonjo kwa ajili ya katatizo kokote binafasi katakachotokea.

Au kama maisha ya uongo huyawezi kabisa kabisa, kwanini usiwe mkweli kwa mwenzio kwamba bwana, pesa ni hii, lakini mimi mwenzio kuna wakati nakuwa na vimatumizi vyangu vya ajabu ajabu, kwahiyo kama unaweza viweke kwenye dafatari lako au uwe unanipa tu kiasi fulani kwenye kila mshahara nitakaowakilisha, ili haya mambo ya kukopa jasho lako mwenyewe yasiwepo.

Chaguo ni lako, njia ya uongo au ya kuwa mkweli – zote zinafanya kazi ila inategemea na aina ya SIEIJII uliyenaye.

Advertisement