NDANI YA BOKSI: Hukumuelewa Ommy Dimpoz utamuelewaje Dudu?

Any way. Shetani naye ana nguvu ingawa hana mamlaka. Ndio maana unakuta mtu mwenye kuzibia riziki za watu naye anapata wafuasi. Wanampenda na kusifiwa kuwa bila huyo hutoki kimaisha. Bila huyo utaendelea kuimbia chumbani kwako. Bila huyo hupati ‘air time’ wala ‘shoo’. Yaani anaongelewa kisifa sifa.

Utadhani kumbania mtu ni sifa njema mbele ya Mungu Baba Mwenyezi. Yaani nafasi ya kuzuia huyu apate na huyu asipate inatukuzwa na watu. Ina maana shetani kishakuwa mkubwa mbele ya Roho Mtakatifu? Kiasi kwamba kazi zake zinatukuzwa? Utasikia: “Ukitaka kutoka kisanii mshikilie fulani.” Hizi akili sasa zife.

Mtu anajipambanua na kila mtu anajua kuwa ni bingwa wa fitina. Yaani naye anajisifu kuwa humuwezi kwa lolote kwa sababu ‘gemu’ lote analijua na liko chini ya soksi zake. Anajua njia na mipango ya kufelisha mtu. Yaani anakuwa na uwezo mkubwa wa kumuumiza mtu kuliko kumsaidia. Anaona ni ushujaa na anajisifu kwa nyimbo na pambio.

Ni mfano tu nataka kutoa. Kuna mtu atakuambia eti bila fulani au fulani hutoki kimuziki. ‘Seriously’? Unaambiwa kwa kutishwa utadhani kazi ya muziki sijui ni kitu gani vile. Acha watu waseme pengine ni uongo kukutia ubaya na watu. Lakini wapo wanaojisifu kabisa kuwa ‘gemu’ liko mikononi mwao. Kinachokera kuna takataka zinazojiita binaadamu zinaunga mkono.

Kweli shetani wa maisha ya watu anakuwa shujaa? Shetani anayemnyima kula mtoto wa Juma Nature anakuaje shujaa? Mtu anayeziba njia ya kupata pesa za Fid Q au Maua Sama anakuaje shujaa? Na unahimizwa kabisa ulambe miguu ya fulani ili utoke kisanaa. Kipaji si dili tena siku hizi bali fitina na njia za panya ndio zinaendekezwa.

Mh Andrew Chenge, aliwahi kusema bilioni moja ni kama vijisenti tu. Kila mmoja aliona kama ni tusi. Magazeti yakaandika, midahalo ikaitishwa na kila mtu akamnyooshea kidole na kumuona ni adui wa wengi. “Anaita milioni elfu moja vijisenti wakati kuna Watanzania wanashindia mlo mmoja?“ Watu wakafura kwa hasira.

Kila mmoja alihukumu bila kupima wala kuchambua kwa kina. Unadhani kwa nini alisema vijisenti? Bila shaka anajua kuna mtu ana bilioni zaidi ya kumi, sasa kwa nini yake moja asiite vijisenti? Tulimhukumu na bado tuna muhukumu. Pole yake na yetu pia. Kumbe alikuwa sahihi, kwa mtazamo wa namba za sasa zinazopotea kupitia taarifa za CAG.

Uliwahi kusikia kuhusu Ommy Dimpoz mara baada tu ya kifo cha Ngwair? Alisema wasanii hawapaswi kufa masikini. Ni wachache waliokuwa upande wake baada ya kauli hiyo. Wengi walimtazama kwa jicho tofauti. Akanyooshewa vidole, wengi walimuona anakufuru. Unadhani ilipaswa Ommy ahukumiwe kwa kauli ile? Hapana.

Wabongo tulio wengi ni wa mapokeo tu. Hatujisumbui kufikirisha bongo zetu. Tunabeba jambo. Tunalitafsiri. Kisha tunahukumu kama lilivyoletwa. Inatia uchungu kusikia msanii fulani aliyewika sana kafariki hohehahe. Au kashindwa kumudu gharama za mambo muhimu katika maisha yake. Hakuna asiyejua kuwa muziki unalipa.

Kama alivyohukumiwa Chenge kwa kauli yake. Ndivyo Ommy naye alivyotundikiwa lundo la lawama kwa kauli yake. Hawakusumbua akili zao ili kumuelewa dogo. Ndio kwanza alikuwa anatoka kisanii wakati huo. Dogo akawa mdogoo kama tairi ya bajaji. Pipo hazikuelewa la muadhini wala mnadi swala. Wakaona dharau kwa kipenzi chao CowBama.

Toka kina Ngwair wanatoka na kuwa wasanii wakubwa. Muziki ulikuwa unalipa ndio maana Ommy ilimuuma. Tatizo ni zile konakona kibao kufikia pesa nyingi zilipo. Tofauti ya sasa na wakati ule, ni kwamba kampuni za biashara zilidhamini shoo na kufaidisha mapromota. Leo zinawekeza kwa msanii husika. Acha kina Nandy wasukume Benzi.

Joh Makini kwenye ngoma yake ya I See Me. Anakuambia: “Najiona mimi yanapoanza mabadiliko, fikra potofu badili hizo, ndoto siyo kuzikalia skani mkilialia, ndoto ni kuamka mbio kuzikimbilia, muziki una hela mwanzo unapoingia, hela nyingi zipo mwishoni hutozifikia, for Real hapo kati kuna kisu si una jambia?” Kina Ngwair hawakuzifikia pesa nyingi kule mwishoni.

Ommy alizidiwa na lawama na kuomba radhi. Kuna mambo yangetumika kabla ya hukumu. Kuyapima maneno yake, biashara ya muziki, pamoja na aina ya maisha ya wanamuziki wengi. Dogo alikuwa sahihi lakini kauli aliitoa wakati usio sahihi. Watu walilia na mengi kwa Ngwair, yeye akapigilia msumari wa moto.

Katika hayo kuna makundi mawili. Wanamuziki wenyewe na waliojiita na ambao bado wanajiita mameneja, pia baadhi ya vituo vya redio. Kuna wasanii ambao baada ya mafanikio fulani walijisahau kuwekeza katika mambo mengine. Matokeo yake walipopotea kisanii wakapotea katika mfumo mzima wa maisha.

Hawa mameneja (vituo vya redio). Ndiyo kirusi kikuu kwa wanamuziki wengi. Hujiona wana mamlaka ya kuamua nani awike na nani asiwike. Hapo bila kujali uwezo wa mhusika wala mvuto wake katika jamii. Hawaoni hatari kama msanii akishindwa kuelewana nao, wafanye kila hila kumzuia asifanikiwe katika sanaa yake.

Bosi anataka kumlipa msanii fedha kiduchu. Akikataa basi anafanya hila nyimbo zake zisipigwe. Tulisikia toka wakati ule hata kina Mb Doggy, Z. Anto walitoweka kwa namna hii. Na sasa tunasikia hata kwa kina Diamond. Usione kama vile hawana adabu, ni muziki na maisha yanayopelekea wageuke wendawazimu vile.

Watanzania wanavyoukubali muziki, ni haki msanii kufa masikini? Tuliacha kujadili kwa kina kauli ya Ommy, waja tukaponda na kuona ustaa unamtia wazimu. Kinyume na ukweli. Kilio cha WCB, Tale, Fella na Sallam na huyo Dudubaya. Ni yaleyale ya Vinega wa Anti Virus, na ndo hao hao walioona Vinega wachawi wa maisha yao.

Ommy ana mapungufu kama binadamu lakini katika hili, alikuwa sahihi. Kama sanaa ikisimamiwa vizuri na Serikali ikadhibiti unyonyaji pamoja na wasanii kuamka na kukataa kunyoywa. Sioni msanii akifa maskini. Siyo wanamuziki tu, ni pamoja na waigizaji. Bongo tunazalisha mastaa wenye majina na umasikini mkubwa.

Kama hawataacha usaliti kwa faida ya wachache. Naamini watapigika daima. Inavutia kuona ‘kombinenga’ ya FA na Jide, wamepatana baada ya miaka kadhaa. Waliungana, kutengana, kisha kupatana kwa sababu ya biashara ya muziki. Muziki ni biashara kubwa inayokosa akili kubwa kuiendesha.