Nandy alipowazidi maarifa madada Bongo Fleva ni hapa...

Muktasari:

  • Mpoto akaonekana kana kwamba alikuwa shina au nguzo ya Parapanda Art. Lakini ukweli ni kwamba alikuwa tone ndani ya bahari pale Parapanda Art. Naye ni miongoni mwa wasanii ambao hawastahili kusifiwa kwa kipaji chake bali kwa juhudi kubwa zilizofanywa na Ruge kumkuza. Ndivyo ilivyo atake asitake.

Hekima ni fikra inayotoka moyoni. Mungu ni mwingi wa hekima. Usijiulize kwa nini aliruhusu uwepo wa shetani. Uwepo wa shetani pia ni hekima za Mungu. Hii leo kuna shetani na mabwege kibao hawatambui uwepo na nguvu ya Mungu. Bila uwepo wa shetani maana ya uwepo wa Mungu kwa wengi wetu isingekuwa na maana.

Mrisho Mpoto ‘Mjomba’. Hapo mwanzo alikuwa Parapanda Art. Ndiko kilipoibuliwa kipaji chake. Chini ya Mgunga Mwamnyenyelwa nyakati hizo. Alipopata jina tu, kama kinda la ndege akatuama kwenye mbawa za Ruge Mutahaba. Jina likaanza kupaa na kupata michongo na ukwasi wa kutosha.

Wakati Mrisho anapaa. Kwa mialiko ya Ikulu na hafla za kiserikali. Mashirika na taasisi mbalimbali. Akigeuka rafiki mkubwa wa JK katika utawala wake. Akianza kubadilishana namba na Samwel Sitta, Lowassa na watu wa kariba hiyo. Parapanda Art ni kama walitoweka kwa kuwepo kama hawapo.

Mpoto akaonekana kana kwamba alikuwa shina au nguzo ya Parapanda Art. Lakini ukweli ni kwamba alikuwa tone ndani ya bahari pale Parapanda Art. Naye ni miongoni mwa wasanii ambao hawastahili kusifiwa kwa kipaji chake bali kwa juhudi kubwa zilizofanywa na Ruge kumkuza. Ndivyo ilivyo atake asitake.

Parapanda walitoweka. Kama ni mmea ulisinyaa kwa nguvu ya Ruge kwenye biashara ya burudani. Aliteka kila kitu kuanzia Clouds mpaka radio zingine. Kufeli hakika ulikuwa msamiati wa kijinga kwa msanii aliyesimamiwa na Ruge. Tatizo alipandishwa Mpoto mmoja na kuumiza kina Mpoto kibao waliobaki Parapanda.

Ilikuwa mgumu kuwa Mpoto huyu unayemuona bila kupitia mikono ya Ruge. Pamoja na kipaji na kujituma kwake. Lakini ilitumika nguvu kubwa sana kuondoa kiwingu cha wasanii wa sampuli yake ili abaki peke yake. Hili halifanyika kwa Parapand tu, hata kwa Jide wakati anachomoka. Kina Stara, na wengine wa kike walikiona cha moto.

Nandy? Nandy ni nani hata athubutu kuondoka kwenye mikono ya Ruge? Ndiyo, alijinyenyekeza. Alimtii na kufuata kila agizo alilopewa. Ndiyo maana hivi sasa ukitaja wanamuziki watano wa kike yeye anasimama katikati ya namba moja au mbili. Pamoja na nguvu ya Ruge, yeye kama yeye ana kipaji kikubwa sana.

Achana na kipaji cha sauti na uwezo wa kuimba. Nandy ni sehemu ya viumbe uzao wa kike wenye kiwango bora cha urembo. Hata mimi ningekuwa Ruge, siyo tu ningemsimamia. Ningevuka boda nje ya mipaka leo hii angeitwa mjane mdogo zaidi. Yes ni kazuri sana. Kazuri kuliko nyimbo zake kadhaa.

Nandy anakupa vitu vingi kwa wakati mmoja. Anakusisimua kwa sauti yake tamu. Mapigo ya moyo wako yatapigishwa kwata na urembo wake. Na uso wako utajaa nuru umuonapo kwenye runinga au jukwani. Anaanza kukuvutia kabla ya kumsikiliza. Muziki wa sasa unataka wasichana wa sampuli yake. Wanaouza kila kitu.

Mwanamuziki wa kike mwenye wajihi wa Nandy. Atapendwa na magazeti, runinga na kurasa za mitandaoni. Anakuwa rafiki wa vyombo vya habari kwa sababu anauza kwa mvuto wake. Huwezi kupata shida sana kumnadi kwa mashabiki. Dunia ya sasa huzingatia sana mvuto wa mtu ili kurahisisha kazi ya kumuuza kwa watu.

Kwa uzuri wake nakiri kuwa ningevuka kiwango cha kimataifa cha wivu kwa kukatuliza ndani. Na kukapiga ‘stop’ majukwani. Kakae ndani kama pambo. ‘Kanikisi’ niendapo ofisini na kanikumbatie nirudipo ‘homu’. Ruge ni tofauti. Alihusudu kipaji kuliko hisia za mwili nafsi na roho. Akaacha mtoto atimize ndoto na matamanio yake.

Ruge? Nandy anaanzaje kumkataa Mwamba aliyemtoa Jide. Aliyemtengeneza Ray C na kumuumba kisanii Mwasiti huku ‘akiwabrand’ kina Linnah na Recho? Kivipi amkatae ‘God Father’ wa Barnaba Boy na Amini. Nguzo ya Q Chilla na Ruta Bushoke? Nandy siyo kichaa alichofanya alikuwa sahihi zaidi kuliko asingefanya.

Kaanza kupata ufahamu analisikia jina la Ruge kwa kiwango na uzito ule ule wa radio Clouds. Ruge alikuwa ‘brand ndani ya brand’. Hakuna mtoto ‘levo’ ya Nandy ambaye angethubutu kutenda dhambi kijinga kwa kujicheleweshea mafanikio yake kimuziki.

Alidondosha ngoma baada ya ngoma. Kiburi alichostahili kuwa nacho kwa kudhibiti hisia za moyo wa mwenye muziki wake (Ruge), alikikosa. Ajabu hiyo sifa imefunga ndoa na Ruby. Kwamba pamoja na kipaji chake kikubwa pengine kuliko Nandy, kuna mahala hukwama.

Ruby kaanza kung’ara kabla ya Nandy. Alikuwa kila kitu pale THT. Na ukimsikiliza Nandy kwenye nyimbo zake za awali ukiwa na sikio la muziki. Utagundua alikuwa anapita njia za Ruby kwenye uimbaji. Lakini kimafanikio Nandy kamuacha Ruby mbali sana bila kuhitaji ushahidi wa akaunti zake. Nandy alijua kula na kipofu bila kumgusa mkono.

Kiburi na jeuri ni kipaji pia. Kosa la Ruby siyo kiburi wala jeuri. Hapana, hata Jide ana kiburi na jeuri sana, uliza wanaomfahamu. Tatizo la Ruby ameanza matumizi ya kipaji chake cha kiburi na jeuri mapema sana. Wenzake kina Jide walisubiri miaka zaidi ya kumi wafunguliwe dunia wakawa wanachotaka ndipo wakakiwasha.

Yawezekana alikuwa na haki zake za msingi. Lakini faida ya kiburi na jeuri yake ni ndogo sana ukilinganisha na hasara. Hata kaka zake hawakuwahi kuwa jeuri na kiburi kama Sugu kabla hawajafunguliwa dunia. Diamond Platinumz yule pale alisubiri afunguliwe dunia kabla hajaanza hizi tambo zake. Aliacha asimike mizizi yake.

kimuona Ruby jukwaani moyo unauma. Ni mgodi uliokosa muwekezaji. Kibaya zaidi watu wanaoweza kumpeleka mahala anapostahili ni wachache nchi hii. Kila mtu anawaza kutajirika zaidi ya kuendeleza kipaji. Halali njaa. Halii shida wala kuombaomba. Lakini kipaji na maisha yake ni tofauti kabisa. Anastahili kupata zaidi na zaidi.