UCHAMBUZI: Ndugai angejipatia muda zaidi kutafakari

Spika wa Bunge, kwa mtazamo wangu, ni kiongozi mwenye dhamana ya juu ikilinganishwa hata mihimili mingine ya Serikali na Mahakama.

Hapa ninamaanisha kwamba, ili Mahakama itekeleze wajibu wake kwa ufanisi, inategemea zaidi Bunge katika uboreshaji wa sheria za nchi zinazotafsiriwa na mhimili huo.

Pia ili Serikali iweze kuwajibika ipasavyo kwa wananchi, inategemea zaidi uimara wa Bunge lenye wabunge walio na lugha moja katika masuala yote yanayohusu maslahi ya Taifa na wananchi, wakiongozwa na spika.

Huo ndiyo ujazo wa nafasi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye pia ni mbunge wa Kongwa, mkoani Dodoma. Mara kadhaa wabunge, hasa wa upinzani, wachambuzi wa duru za kisiasa na wanaharakati wamekuwa wakituhumu Bunge hilo kuwa ni dhaifu, kwa maana ya kufanya kazi ya kutoibana barabara Serikali.

Nakumbuka, mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe aliwahi kuhojiwa mbele ya kamati ya Bunge na kutoa utetezi wa hoja zake akieleza kwa nini anaamini Bunge hilo ni dhaifu. Pia John Mnyika aliwahi kueleza hivyo na wabunge wengine. Kwa hiyo hii ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Asaad si habari mpya.

Profesa Assad ni miongoni mwa watendaji ambao mara kadhaa amekuwa akilikosoa Bunge hilo kutokana na kutofanyiwa kazi mapendekezo mengi yanayotolewa kupitia ripoti za kila mwaka za ofisi yake. Hata hivyo, safari hii Spika Ndugai aliibua mjadala katika mitandao ya kijamii baada ya kumtaka Profesa Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili Januari 21, 2019 vinginevyo atafikishwa kwa pingu.

Kilichoshtua zaidi ni nino ‘pingu’. Binafsi sikuona upya wa kauli ya CAG ambayo amekuwa akiitoa, sikuona upya wa madai yaoe kwa kuwa yametolewa na wabunge mara kadhaa, tena kwa kueleza na sababu zao.

Muktadha wa mahojiano yaliyozaa sakata zima kati ya CAG na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, ulikuwa unampa fursa Spika Ndugai kujipatia muda wa kutafakari kuhusu Bunge analoliongoza na jinsi linavyotazamwa na watu wengine, ili kama kuna tatizo lirekebishwe.

Si lazima kila mtu alitazame Bunge sawa anavyolitazama Spika mwenyewe. Lakini hatua kung’aka kila Bunge linapokosolewa si utamaduni mzuri, maana unakatisha tamaa, kujenga hofu na kupokonya uhuru wa watu kukosoa na pengine kuingilia majukumu ya CAG.

Kwa mtazamo wa kisheria na kikatiba iko wazi kwamba hakukuwa na sababu wala uhalali wa Ndugai kutoa agizo hilo la vitisho kwa CAG. Hatua hiyo badala ya kuonyesha uimara wa Bunge limeonyesha dosari zaidi za kiuongozi.

Hadhi ya Bunge haiwezi kulindwa kwa pingu bali kwa kazi ambazo bunge hilo linazifanya kwa niaba ya wananchi. Lakini kitendo cha kupulizwa moto kinaweza ama kuuzima au kuuwasha zaidi. Spika angejipa muda zaidi wa kufikiri hata njia ya mawasiliano kati yake na CAG badala ya hii ya kutishia kupitia mkutano na wanahabari.

Nionavyo mimi ni muhimu kiti cha spika kufanyia kazi changamoto zinazoelezwa na wakosoaji badala ya kuwathibiti wakosoaji wenyewe.