Pasua kichwa na kidhibiti tendo

Muktasari:

  • Basi baada ya kunyagika, huku nikijiimbia nyimbo zangu za Kinyamwezi ili nizame usingizini moja kwa moja, nikashtuka nimenyanyuliwa kama vile napelekwa kulimishwa (na kitambi hiki)? Jamani! Nikajaribu kupaza sauti lakini wapi.

Ndoto zingine Bwana, zinatisha. Mimi nilifikiri kwamba nikibugia nyagi ya kutosha kama mzalendo (hata kulewa, ni muhimu tulewe kizalendo), nitaweza kusahau jinamizi zote za hali halisi ya maisha kumbe jinamizi za mchana zinaungana na za usiku hadi unajua unaota lakini hujui utaamkaje na utakuta nini hata ukifanikiwa kuamka. Dah!

Basi baada ya kunyagika, huku nikijiimbia nyimbo zangu za Kinyamwezi ili nizame usingizini moja kwa moja, nikashtuka nimenyanyuliwa kama vile napelekwa kulimishwa (na kitambi hiki)? Jamani! Nikajaribu kupaza sauti lakini wapi.

Badala yake nikakuta nimevalishwa nguo za kidaktari na kusimamishwa kwenye chumba cha upasuaji. Kule alikuwa amelala mtu amepasuliwa kichwa kisha madaktari, badala ya kutoa uvimbe ambao unaweza kumletea madhara, walikuwa wanamjazilia vitu kibao humuhumu. Sikuweza kuvumilia.

‘Jamani mnafanya nini? Mtamwua huyu mtu?’

‘Inakuhusu nini? Kwanza liangalie. Shepu kama mbuzi dume. Tukujazilie kidhibiti tendo na wewe?’

‘Hapana jamani, huyu ni mama yetu. Ametulea, na kutuonesha jinsi ya kuishi pamoja. Bila yeye tusingepata akili ya kutafakari, na kuhoji na kuchambua?’

‘Akili gani hiyo? Unajua akili nyingine ni hatari sana? Hizi ndizo akili za kutuzuia tusipate maendeleo.’

‘Lakini huyu ni mama yetu sisi sote.’

‘Mmmh! Kwani mama hawezi kukosea? Baada ya kutambua kwamba mama yetu ni chanzo cha hayo yote, imebidi tumwekee kidhibiti tendo ili asitupotoshe. Unajua kwamba amegombana sana na baba yetu? Unakubali kweli?’

‘Lakini mimi naona baba hajamwelewa mama. Bila mama, sisi sote hatutapata maendeleo ya kweli. Mama anatusikiliza na kutupatia nafasi.’

Duh! Walivyoniangalia huku wakishika visu vyao vya upasuaji, nikaamua kuchuchumaa na kujificha nyuma ya meza ya zana za upasuaji. Bahati nzuri, kuona hivyo madaktari walicheka sana.

‘Achana na huyu. Mwoga kama wale wote wengine. Hakuna haja ya kupasua kichwa chake. Tuendelee na kazi zetu.’

Basi wakati naangalia, walikuwa wanaendelea kumshindilia vitu kwenye kichwa.

‘Hiki kidhibiti tendo ni kiboko yake. Hafurukuti tena nakuambia,’ alisema daktari mmoja. Mwenzie akajibu.

‘Na iwe hivyo maana ni sijui mama amekuwaje. Tumempasua na kushindilia mara ngapi lakini bado hataki kutulia. Sijui ni kichaa cha aina gani.’

Ghafla yule mgonjwa akatoa yowe kali sana. Mwili wake ulitetemeka mara ya kwanza … mara ya pili … mara ya tatu … kisha hakutingishika tena. Madaktari walishtuka. Mmoja akasema.

‘Jamani tumemwua mama yetu!’

Mkuu wao akajibu.

‘Hakuna kumwua. Tutamwuaje huku tumesema kwamba tunampa uhai zaidi? Yu hai nakuambia.’

Akacheza ngoma na wenzie huku akiimba

‘Yu hai, jamani mwe, yu hai.’

Kisha akaendelea kushindilia vitu vingine huku mgonjwa akaonekana hapumui tena. Baada ya kumaliza kushindilia, wakamshona tena. Kisha wakamwacha pale bila dalili yoyote ya uhai na kutoka nje. Mimi niliwafuata kimyakimya na kuona watafanya nini.

Kumbe huko nje, ulikuwepo umati mkubwa wa watu wakisubiri kusikia hali ya yule aliyepasuliwa. Kundi lile la madaktari walipokelewa kwa vigelegele, vifijo na hoihoi. Daktari mkuu akanyanyua mkono.

‘Napenda kuwaarifu kwamba tumefanikiwa sana. Mama yetu yu hai!’

Watu wakapiga vigelegele sana.

‘Ndiyo! Sote tulikuwa na wasiwasi sana juu ya mama yetu, kwa nini hataki kufuata ya baba tu. Na watu wasiojua udaktari walitusingizia eti kushindilia vitu kichwani ili kudhibiti matatizo yake ya kutembea mwenyewe hata kama anaelekea mtaroni na kuumia, na matatizo ya kujiamulia mambo bila kusikiliza hekima za baba na wahenga wengine, na matatizo ya kubwabwaja hovyo aonekane kichaa, kumwekea kidhibiti tendo hiki kikubwa kutakuwa ni kumharibu au hata kumwua. Walikosea. Walikosea kwamba hawana imani na sisi na utaalam wetu hata kidogo.’

Watu walianza kuzomea kwa nguvu sana.

‘Vibaraka hawa. Waende wakatafute hospitali zao kwingine. Mama yetu yu hai!’

Daktari mkuu aliwanyamazisha kwa kupunga mkono.

‘Lakini tumeonesha kwamba hawajui wasemalo. Leo tumeshindilia kidhibiti tendo kikubwa kabisa hivyo kwa sasa ataweza kutembea, na kusema, na kufanya maamuzi sahihi bila kusumbuliwa na kitu chochote. Ndiyo aina ya mtu tunayemtaka.’

Wacha watu washangilie kwa nguvu zote. Lakini sauti moja ikasikika kutoka nyuma.

‘Tuoneshe mama yetu basi.’

Daktari akashtuka kidogo. Akajibu kwa hasira iliyochanganyikana na kejeli.

‘Baada ya operesheni kubwa namna hii, unategemea ataamka tu na kutembea. Anapumzika.’

Hapo mimi nilishindwa kuvumilia.

‘Siyo kweli. Amekufa. Nimeshuhudia kwa macho yangu. Wamemwua mama yetu kipenzi. Hawezi kuamka tena.’

Ujinga wangu! Madaktari wote wakanigeukia.

‘Mpumbavu unajua nini? Wewe ni daktari? Wewe unajua ubaya wa kuwa na mama asiyetii baba? Ndiyo maana tumemwekea kidhibiti tendo?’

‘Lakini katika kumdhibiti umemwua.’

Daktari mmoja akacheka.

‘Hujui. Lakini hatuwezi kukataa kwamba kuua ni kudhibiti moja kwa moja. Mama ukimruhusu kuendelea kuwa huru bila kudhibitiwa, anawaambukiza watoto wake wengi hadi wanampinga baba bila heshima wala hekima.’

Mwingine akadakia.

‘Tumshughulikie huyu. Haelewi kwamba mama akidhibitiwa, basi na wana wadhibitiwe pia.’

Wakanishika na kuanza kugongagonga kichwa changu huku wakitaka kukipasua na visu vyao. Wacha nipige yowe. Nikishtuka kwamba niko kitandani.

‘Msinipasue. Msinipasue. Hamwezi kumfanyia mama hivyo. Ataamka tu.’

Mke wangu akabaki ananishangaa.

‘We Bwana vipi?’