Raia makini na dhana nzima ya demokrasia na ushiriki wa watu

Muktasari:

  • Kwa wachambuzi na watu wanaoguswa na uhai wa taifa letu ni lazima watakuwa wanajiuliza maswali mengi: Ni mvuto wa mtu, ni mvuto wa chama, ni umasikini, ni rushwa, au ni elimu ndogo juu ya demokrasia na ushiriki wa watu katika uongozi wa taifa lao.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa tumeshuhudia chaguzi ndogo nyingi na wanasiasa wameweka rekodi mpya ya kuhama vyama. Fedha zinazotumika kurudia chaguzi hizi ni hasara ambayo tutaijua mbele ya safari. Tutake tusitake ni lazima ituguse na kutuumiza tu.

Kwa wachambuzi na watu wanaoguswa na uhai wa taifa letu ni lazima watakuwa wanajiuliza maswali mengi: Ni mvuto wa mtu, ni mvuto wa chama, ni umasikini, ni rushwa, au ni elimu ndogo juu ya demokrasia na ushiriki wa watu katika uongozi wa taifa lao.

Dhana ya Demokrasia

Pia, mtu mzushi anaweza kuuliza kama kweli raia ni makini? Katika hali ya kawaida, raia makini ni lazima atambue dhana nzima ya demokrasia na ushiriki wa watu. Akishafahamu hilo, hawezi kukubali kurudia uchaguzi wa mtu yuleyule ambaye anahama chama na kuomba kugombea tena kwenye chama kingine kwa uwakilishi uleule, Bunge na halmashauri ileile.

Katika maana yake pana, demokrasia ni njia ya kutawala kwa msingi wa kupata ‘ridhaa ya watu’. Katika demokrasia, mawazo ya watu yanazingatiwa katika kufanya maamuzi yote. Raia wote wana haki ya kushiriki katika kuamua jinsi nchi inavyoongozwa. Raia wanashiriki katika uongozi wa dola kwa kupitia viongozi wanaowachagua na wanathibitisha imani kwa viongozi wao kupitia uchaguzi.

Demokrasia ni mfumo wa utawala ambapo watu huwachagua viongozi wa serikali yao wenyewe na kuainisha jinsi inavyopaswa kufanya kazi. Demokrasia hukuza ustawi wa watu wote. Kila raia ana haki ya kushiriki katika uendeshaji wa shughuli za umma na katika mambo yote yanayoathiri maisha yake. Katika kujishughulisha na masuala ya uraia, raia wanaiwajibisha serikali. Viongozi wanawasikiliza wapiga kura wao kabla ya kufanya maamuzi kwa niaba ya watu.

Hata hivyo kuna vikwazo vinavyojitokeza katika chaguzi za kidemokrasia. Vikwazo vikubwa kwa uchaguzi wa kidemokrasia vinajumuisha umaskini, ukosefu wa usawa, ujinga, rushwa katika uchaguzi, chaguzi mbovu, siasa isiyo na maadili, kukata tamaa kisiasa, woga, utamaduni wa kisiasa uliolazimishwa, ubaguzi, kushauriwa na uongozi wa mabavu.

Kwa maneno mengine demokrasia ni njia ya kutawala ambayo mawazo ya watu wote hufikiriwa katika kufanya maamuzi ya umma. Ina msingi wake katika imani ya ‘utashi wa watu’. Hivyo, demokrasia husimamia ustawi wa watu wote, kwa manufaa ya watu wote.

Demokrasia pia inahusu kujitolea kwa raia wote. Raia wana wajibu mkubwa katika jamii inayojenga demokrasia. Kwa maana hiyo ndio kusema demokrasia inaweza kufanya kazi pale tu ambapo wananchi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa na masuala ya umma. Kwa kuzingatia hilo, demokrasia ni kile wanachokifanya wananchi na si kile wanachofanyiwa.

Hivyo basi demokrasia hukuza uhuru, usawa na haki kwa wote. Pia, inasimamia ukuzaji wa ushiriki wa moja kwa moja na wa uwakilishi kwa watu wote katika shughuli za umma. Katika jamii ya leo, demokrasia ya moja kwa moja inadhihirika kwa njia ya kushiriki katika uchaguzi. Pia, inajidhihirisha katika ushiriki wa raia katika utawala kwenye ngazi ya kijiji na Serikali za Mitaa.

Maana ya mamlaka

Katika demokrasia, wananchi ndio wenye mamlaka. Serikali ni mtumishi wa wananchi. Uhusiano kati ya wananchi na serikali ni wa mkataba. Yaani, viongozi na wawakilishi wengine wanafanya maamuzi kwa niaba ya mwananchi ambaye ni raia. Ufanyiwe mapitio kipindi hadi kipindi, kwa kutumia chaguzi. Kwa upande wao, raia lazima waheshimu sheria zilizotungwa. Pia washiriki katika shughuli za umma na kukubali au kukataa jinsi serikali inavyofanya kazi yake.

Tunaposema kwamba raia ndio wenye mamlaka, maana yake ni kwamba raia wanapowachagua viongozi wa kuwawakilisha, hawajivui mamlaka hayo. Wawakilishi waliochaguliwa wanawajibika kwa raia, yaani wanawajibika kwa wapiga kura wao.

Na tunaposema ‘mkataba wa kijamii’ maana yake ni namna ya kuelezea uhusiano uliopo katia ya raia na dola au serikali. Dola au serikali imekuwepo kutokana na haja ya kuanzisha na kudumisha utawala wa sheria. Ili kuweka utaratibu wa aina hiyo, raia wana wajibu wa kutekeleza kwa serikali na pia serikali ina wajibu wa kuwatendea raia.

Hivyo basi viongozi wa kidemokrasia huwasikiliza wapiga kura wao kabla ya kufanya maamuzi kwa niaba yao. Hivyo ndivyo inapaswa kuwa, ingawa wakati mwingine inakuwa kinyume. Uongozi wa kidemokrasia uko wazi. Hauna chochote cha kuficha. Unapaswa kutoa taarifa jinsi unavyofanya shughuli zake na kuwa tayari kujibu maswali yatokanayo na ushauri wa raia pamoja na matatizo yao.

Raia kwa upande wao wanapaswa kuvumilia tofauti zilizopo kati yao. Maana ya uvumilivu wa kisiasa ni mtu kuwatambua wapinzani wake kisiasa, na kutambua kwamba wapinzani hao wana mawazo na maoni tofauti, na kuwa wana haki ya kuyatetea mawazo na maoni yao katika mchakato wa kisiasa. Hii inapunguza uhasama unaojitokeza katika vyama.

Taifa linakuwa na watu wenye maoni tofauti, lakini wenye lengo moja la kujenga na kuleta maendeleo. Hivyo haina maana yoyote mtu kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine kama mtu huyo yuko kwenye mfumo wa uongozi unaotambuliwa kisheria. Anayemshawishi na yeye anayekubali, wote wanahitaji shule.

Uongozi wa kidemokrasia unatambua utawala wa kisheria. Unatambua kwamba watu ndio wanaoshika hatamu. Unajumuisha watu wote kufanya mashauriano na kufuata kanuni za demokrasia. Kinyume na uongozi wa kidemokrasia ni uongozi wa mabavu ambao huwafanya viongozi washike hatamu.

Uongozi wa mabavu

Uongozi wa mabavu haushauriani na wananchi. Daima unawaweka raia pembezoni na hauna uvumilivu kwa mawazo pinzani na haukubali kukosolewa.

Hivyo raia makini ni lazima afahamu ubora wa demokrasia na ushiriki wa watu. Pia, atambue ubaya wa uongozi wa mabavu. Maana raia anatakiwa kutambua kwamba ni wajibu wa serikali kutoa na kusimamia huduma za jamii, kama vile elimu, afya na maji, vilevile kwamba serikali ina haki ya kukusanya kodi kutoka kwa raia ili kuhimili utoaji wa huduma.

Wajue kwamba kwa upande wao, raia wana wajibu wa kulipa kodi, kupeleka watoto wao shule na kuzilinda mali za umma dhidi ya uharibifu au wizi na kwamba pia, wana haki ya kuiwajibisha serikali kwa matumizi mabaya ya fedha za umma zilizotengwa kuhudumia huduma za jamii.

Je, wananchi wanafahamu kwa kina maana ya uchaguzi na kura yao, maana ya demokrasia na ushiriki wao, maana ya utawala wa kidemokrasia, je, wanafahamu misingi ya katiba, haki za raia na utawala bora? Haya ni maswali ambayo yanahitaji majibu hasa kwa wakati huu.

Haitoshi tu mtu kupiga kura. Ni lazima mtu afahamu ni kwa nini anapiga kura. Ni muhimu mtu kufahamu ni kitu gani kinafuata baada ya kupiga kura. Ni jambo la msingi mtu kufahamu uwezo na nguvu ya kura yake.

Mazingira ya kijamii na ya kisiasa ya Tanzania, yanadhihirisha viwango vya chini vya ufanisi wa uraia; utamaduni wa kutoshiriki kikamilifu katika chaguzi; ongezeko la matukio ya fujo za uchaguzi; na mfumo wa siasa wa vyama vingi ambao kwa ujumla ni dhaifu. Hivyo elimu ya uraia ni msaada mkubwa wa kuboresha stadi za wananchi ili kuwafanya wawe raia makini na wanaowajibika.

Uanzishwaji wa demokrasia ya vyama vingi umechochea ushindani mkali wa kisiasa, umeongeza haja ya kuwa na elimu ya upigaji kura. Elimu hii itamsaidia mpiga kura kuwa na maarifa na ufahamu kuhusu masuala ya mchakato wa uchaguzi ili aweze kuwa makini kwenye uchaguzi. Elimu hii inampatia habari kumwezesha raia kuelewa vyema haki na wajibu wake katika mchakato wa uchaguzi, inajenga pia uelewa kwa raia kwamba mustakabali wake unategemea kura yake.

Elimu ya uraia inasaidia kuondoa mawazo ya uhasama unajitokeza katika vyama. Kwa sababu ya kutokuwa na elimu juu ya mambo haya watu wamekuwa wakichukiana na wakati mwingine kugombana kwa vile wako kwenye vyama viwili tofauti. Na wanasiasa wamekuwa wakishambuliana badala ya kuelezea sera zao kwa wananchi. Matokeo yake vinakuwa si vyama vya kisiasa tena bali ni makundi ya watu wanaotaka kuingia madarakani.

Kawaida ni kwamba vyama vyote vinalenga kutoa huduma kwa raia. Chama chochote kinachofanikiwa kushinda, kinaunda serikali iliyowekwa madarakani na raia, na serikali hii inawajibika kwa wananchi. Tanzania inatumia mfumo wa uchaguzi ambao mgombea anayepata kura nyingi ndiye mshindi.

Pia, Tanzania inatumia uwakilishi wa nusu uwiano katika uchaguzi wa wawakilishi wa wanawake katika Bunge.

Hivyo baada ya kupata elimu ya kupiga kura raia aliye makini anafahamu ampigie kura nani, apige kura kwa maswala gani na anakuwa anajua jinsi ya kuwawajibisha viongozi wake, maana yeye ndiye anakuwa amewaweka madarakani.

Raia makini

Raia makini ni lazima ajue na kutambua kwamba madhumuni ya uchaguzi ni kuwawezesha watu kuchagua wawakilishi na viongozi ambao watasimamia shughuli za umma kwa masilahi ya wapiga kura.

Na kwamba wakishindwa kusimamia vizuri masilahi ya wapiga kura wanaweza kuondolewa. Mpiga kura akijua hivyo hawezi kuuza kura yake na kulazimishwa kumchagua mtu ambaye hafai, akifanya hivyo akakubali kuuza kura yake anakuwa anajua kwamba kwa huru wake mwenyewe anajitia kitanzi.

Raia makini ni lazima atambue kwamba chaguzi ni muhimu kwa kuchagua viongozi wazuri, kuhakikisha utawala bora, kuwajibisha serikali kwa matendo yake, kuunda serikali inayopendwa na watu na kuboresha mfumo wa kisiasa na kwamba Tanzania imekuwa ikifanya Uchaguzi mkuu kwa kuzingatia Katiba na Sheria ya Uchaguzi.

La msingi hapa ni kusisitiza kwamba wakati tunaelekea kwenye chaguzi ndogo ambazo zinalazimishwa na raia ambao si makini, ni muhimu kutambua kwamba kila raia anawajibika kuwa makini na kila raia aliyejiandikisha kupiga kura ni kuhakikisha anatumia kura yake kwa busara, maana kazi haishii katika kupiga kura, kazi inaanza baada ya kupiga kura.

Padri Privatus Karugendo. +255754633122