Rais Magufuli akutane na viongozi wa vyama vya siasa

Muktasari:

  • Siku hiyo, Rais alikutana na viongozi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na wale wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ikiwa ni miaka miwili tangu waombe kukutana naye 2016. Ningependa kushauri mlango kama huo ufunguliwe pia kwa viongozi wakuu vyama vya siasa nchini.

Agosti 7, 2018 Rais John Magufuli alikutana na viongozi wa dini ya Kikristo Ikulu na kubadilishana mawazo.

Siku hiyo, Rais alikutana na viongozi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na wale wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ikiwa ni miaka miwili tangu waombe kukutana naye 2016. Ningependa kushauri mlango kama huo ufunguliwe pia kwa viongozi wakuu vyama vya siasa nchini.

Kama mtakumbuka, Septemba 1, 2016, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilipanga kuendesha maandamano yasiyo na kikomo nchi nzima kueleza hisia zao kuhusu mambo mbalimbali wasiyokubaliana nayo.

Uamuzi huo uliibua sintofahamu kubwa hadi Jeshi la Polisi likalazimika kufanya mazoezi ya utayari kwa ajili ya kuwakabili.

Hata hivyo, ni kutokana na maombi ya viongozi hao wa dini ya Kikristo na wale wa Kiislamu, Chadema ilisitisha maandamano hayo, baada ya viongozi wa dini kuomba kumuona Rais Magufuli.

Japo kile walichokijadili faragha hatukifahamu kwa ujumla, nilifarijika kwa hatua hiyo ya Rais kukutana na viongozi hao licha ya kwamba ilikuwa baada ya miaka miwili tangu waombe kukutana naye.

Kabla ya kukutana na viongozi hao, Julai 3, 218 Rais alikutana na viongozi wakuu wastaafu, wakiwamo marais wastaafu, mawaziri wakuu wastaafu, majaji wakuu wastaafu na maspika wastaafu.

Katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine, wakubwa hao walihimiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa utawala wa sheria na kujenga taasisi imara.

Machi 19,2018, Rais Magufuli alikutana na wafanyabiashara na wawekezaji na akasikiliza kwa kirefu kero wanazozipitia na zile zilizokuwa na maelekezo ya moja kwa moja, alitoa maagizo.

Nimetangulia kuonyesha mtiririko wa matukio hayo, ili niweze kujenga hoja ya kwa nini sasa ni muhimu kwa Rais kukutana na viongozi wakuu wa vyama vya siasa nchini.

Hakuna ubishi kwamba kumekuwepo na msuguano wa takribani miaka miwili sasa, kati ya Serikali ya CCM na vyama vya upinzani, hasa namna Serikali inavyoendesha shughuli za kisiasa nchini.

Kiini cha msuguano huu ni amri ya kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa hadi 2020, na kuruhusu tu mikutano ya wabunge na madiwani.

Lakini amri hii inaonekana kukata upande mmoja tu wa upinzani, kwani viongozi wa chama tawala wameendelea kufanya mikutano hii, pasipo kushughulikiwa na polisi kama walivyo wapinzani.

Mathalani, katika chaguzi ndogo zinazoendelea, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vyenye mamlaka, vinanyooshewa kidole kwa madai ya kukandamiza upinzani.

Viongozi wa kisiasa na wananchi waliotumia haki yao ya kikatiba kutoa maoni yao dhidi ya utendaji wa Serikali walijikuta matatani wakishitakiwa kwa uchochezi au makosa ya mtandao.

Ibara ya 3(1) ya Katiba ya mwaka 1977 inasema wazi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Hitaji hilo la kikatiba lilisiribwa kwa kutungwa kwa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992, ambayo inaruhusu vyama vya siasa kunadi sera zao kupitia mikutano na pia haki ya kuandamana.

Si hivyo tu kanuni za Maadili ya vyama vya siasa ya mwaka 2007, kama zilivyotangazwa katika gazeti la Serikali (GN) namba 2015 ya Oktoba 12 mwaka 2007 nazo zinatilia mkazo jambo hilo.

Kifungu cha 4(1) (b) kimeainisha haki za vyama vya siasa ni kutoa maoni ya kisiasa kadri itakavyoona inafaa, ili kutekeleza sera zake, kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ya 1992 na katiba ya nchi.

Ndiyo maana namsihi Rais wangu mpendwa, asione nongwa kukutana na viongozi wakuu wa vyama vya siasa ili wamweleze dukuduku lao na awaeleze kile anachokiona juu yao.

Wala viongozi hao wa kisiasa wasifikiri Rais kukutana nao watakuwa wameshinda, la hasha, Rais ni baba wa Watanzania wote na anatambua mkono wa mtoto ukichafuka haukati bali anausafisha.