Reli ya kisasa isibezwe, ni historia inaandikwa

Wednesday August 8 2018Peter  Elias

Peter  Elias 

Watanzania wamekuwa mahiri kwa ukosoaji wa mambo mbalimbali, yawe mazuri au mabaya. Bahati mbaya wengi wa wakosoaji hao wamekuwa hawatoi njia mbadala ya nini kifanyike ili nchi hii iweze kupiga hatua kimaendeleo.

Ninatofautiana na wengi kwenye ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambao ni utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli. Hakuna asiyejua umuhimu wa usafiri wa treni kwa maendeleo ya nchi yoyote.

Binafsi nimetembelea na kujionea kasi ya ujenzi wa reli hiyo ambayo baada ya muda mfupi Watanzania wataanza kuona matunda yake. Itakuwa ni mkombozi kwa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kwa wadogo.

Usafiri huo utarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kwa gharama nafuu zaidi. Itakuwa na kasi kubwa ambayo itaokoa muda wa wananchi katika uzalishaji wao.

Reli hiyo inatoa ajira kwa Watanzania wengi kuanzia wakati wa ujenzi wake mpaka uendeshaji wake itakapokamilika. Itachochea sekta nyingine za uchumi kama vile biashara, kilimo na huduma nyingine za kijamii.

Wataalamu wa reli hiyo wanasema kuanzia Septemba mwaka huu, wataanza kutandika mataluma kwenye tuta la reli lililojengwa. Ujenzi wake unafanyika usiku na mchana ili ifikapo Novemba, 2019 awamu ya kwanza ya ujenzi huo kutoka Dar – Morogoro iwe imekamilika.

Serikali ina dhamira ya dhati kukamilisha mradi huo haraka, makandarasi nao—kampuni ya Yapi Merkezi inatekeleza majukumu yao kwa kasi kubwa. Kweli, reli hiyo itabadilisha mfumo wa maisha na sura ya nchi.

Wanaojua historia watakumbuka reli ya kati iliyojengwa na Wachina miaka ya 1970 ilivyokuwa chachu ya maendeleo kwa Taifa hili. Iliitoa Tanzania kutoka sehemu moja kwenda nyingine na mpaka sasa iko hapa.

Inayojengwa itakuwa ni ya kisasa zaidi ya hiyo. Uendeshaji wake, ufanisi, uwezo na ustahimilivu wake ni rahisi zaidi. Kwa nini watu hawalioni hili kama jambo kubwa ambalo likikamilika kila mwananchi anatakiwa kutembea kifua mbele.

Nchi zote zilizoendelea duniani zinatumia usafiri wa treni. Wao wamekwenda mbali zaidi kwa kujenga treni za chini ya ardhi maarufu kama Metro. Walianza zamani kutumia usafiri huo, hawakumbatii teknolojia moja wakati zinabadilika kila kukicha.

Kwanini Tanzania tuendelee kutumia reli ya zamani? Kwanini hatuoni na kuthamini jambo hilo la kihistoria? Utakuwa mtu wa ajabu kama unapingana na historia inayoandikwa katika nchi hii kwa sababu zako binafsi.

Kitu ambacho baadhi ya watu hawakijui ni kwamba reli hii itaunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi na Uganda. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) nayo itapata urahisi reli hiyo ikifika Kigoma.

Ni jambo la kujivunia kuona viongozi wa ukanda huu wana utashi wa kisiasa katika kutekeleza majukumu waliyopewa na wananchi. Ni wajibu wa wananchi kuwatia moyo viongozi wao wanapofanya mambo ya maendeleo bila kujali tofauti za kisiasa.

Tanzania ni yetu sote na kila mtu ana wajibu wa kujivunia nchi yake anaposimama mbele ya watu wa mataifa mengine. Kama nchi haina kitu cha kujivunia basi Watanzania wataendelea kuwa wanyonge mbele ya wenzao wa nchi zilizopiga hatua.

0763891422

Advertisement