Ruge ameondoka, ameacha deni kuhusu sera ya kiuchumi kwa nchi

Muktasari:

  • Ukuu wa Ruge upo kwenye maeneo mengi. Kubwa zaidi ni jinsi alivyoshirikiana na swahiba wake, Joseph Kusaga, kuanzisha kituo cha redio Clouds FM. Redio hiyo ikawa ndani ya ‘kachumba kadogo’ jengo la Kitega Uchumi, Samora Avenue.

Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji, Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba, tayari ameshaitikia wito wa Mungu. Alifariki dunia Februari 26, mwaka huu, ikiwa ni miezi miwili na siku mbili kabla hajatimiza umri wa miaka 50. Ruge alizaliwa Mei Mosi 1970.

Ukuu wa Ruge upo kwenye maeneo mengi. Kubwa zaidi ni jinsi alivyoshirikiana na swahiba wake, Joseph Kusaga, kuanzisha kituo cha redio Clouds FM. Redio hiyo ikawa ndani ya ‘kachumba kadogo’ jengo la Kitega Uchumi, Samora Avenue.

Ruge na Kusaga wakaikuza Clouds FM hadi kuwa taasisi kubwa yenye vyombo kadhaa vya habari. Inamiliki redio tatu, televisheni mbili. Wamewekeza mpaka Dubai. Walitoka kufanya kazi kwenye kichumba kidogo hadi kuwa na majengo makubwa pamoja na kuajiri mamia ya Watanzania.

Ruge ni sehemu ya mwamko wa kuona burudani ni biashara. Kampuni yao tanzu ya Prime Time Promotion huratibu matamasha makubwa ya muziki. Ruge akaanzisha taasisi ya kukuza vipaji na kuviendeleza ya Tanzania House of Talent (THT).

Matamasha ya Fiesta huzunguka nchi nzima kutoa huduma ya burudani. Ruge akaona burudani pekee si afya kwa Watanzania. Akaanzisha mradi wa Fursa ili kila Fiesta inapofanyika, yanakuwepo makongamano ya kuwapa maarifa watu na kuwahamasisha kuchangamkia fursa zinazowazunguka ili wafanikiwe kimaisha.

Mpaka hapo unapata nini? Kwamba Ruge amekuwa kitovu cha ajira nyingi. Kupitia yeye, kuna waliopata ajira na kuanzisha makampuni na kuwaajiri wengine. Amekuwa chachu ya ukuaji wa pato kwenye tasnia ya burudani na leo Tanzania ina wanamuziki matajiri. Ruge hawezi kunyimwa haki ya mapinduzi hayo ya kiuchumi.

Ruge ameacha deni

Wakati Novemba mwaka jana Serikali ilizuia tamasha la Fiesta kufanyika Dar es Salaam, chini ya saa 24 kabla ya kilele chake na kusababisha hasara kubwa kwa waandaaji, kuna suala la kisera kuhusu watu na uchumi lazima liangaliwe.

Zuio la Fiesta lilikuwa na maumivu mengi. Waandaaji wenyewe, maana walizuiwa wakiwa ukingoni. Wanamuziki walikosa mapato. Wajasiriamali waliojipanga kuuza bidhaa kwenye tamasha hilo na ambao walikuwa wameshafanya manunuzi, walipata hasara kubwa. Wapo waliokopa na kudaiwa marejesho na kadhalika.

Nchi inahitaji sera nzuri za kuwafikia watu, kutambua vipawa vyao na kuviendeleza ili vitumike kuiponya jamii iliyo kubwa. Ruge ni mfano kuwa yeye peke yake, ameweza kuamsha watu wengi na kubadili maisha yao. Vipi nchi ikiwa na akina Ruge laki moja?

Serikali lazima iwe na mipango mahsusi ya kutambua vijana wenye kutoa ahadi njema kwa nchi. Pindi wanapochipuka, basi watambuliwe, wawezeshwe ili vipawa vyao vitumike kuijenga jamii iliyo pana.

Kuna vijana wabunifu wa teknolojia. Uvumbuzi wao unaweza kuifaa sana nchi kama watawezeshwa. Hata hivyo, wamekuwa wakihangaika mitaani ili kuyafanya maarifa yao yazae matunda, yawafae wao na Watanzania wengine. Hatudhani kuwa nchi inaweza kuwa na akina Bill Gates, Mark Zuckerberg na matajiri wengine wa dunia, waliotajirika kwa teknolojia.

Nchi inaweza kupiga hatua haraka kama tutakuwa na kundi kubwa la watu kwenye sekta binafsi linalotengeneza ajira mamia kwa maelfu. Kwanza litaondoa tatizo la ajira. Pili, ni kukuza idadi ya watu wanaozalisha. Tatu, Serikali itanufaika kwa kodi.

Tusome Qatar

Ukisoma maudhui ya Mkakati wa Maendeleo ya Taifa (NDS) kwa Qatar mwaka 2011-2016, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Qatar kuelekea mwaka 2030, unapata msingi kwamba uchumi wa wananchi ni ule ambao unaratibiwa kwa sera inayothamini mchango wa kila mwananchi.

Serikali inapobeba dhamana ya kuendesha nchi lazima ijipe wajibu wa kuratibu maisha ya watu, na ihakikishe kwamba kipindi taifa linapiga hatua kwa maendeleo ya kiuchumi, hakuna mwananchi anayebaki nyuma.

Umuhimu wa sensa siyo kujua tu idadi ya watu na kutangaza kama mapambo, bali Serikali inatakiwa ijue idadi ya watu wake kisha iweke mipango ya kuwahudumia kijamii, vilevile kuwatumia kama chanzo kikuu cha uzalishaji ili nchi isonge mbele.

Qatar ni nchi ya 47 kwa GDP (pato la taifa) lakini inashika nafasi ya sita kwa GDP per capita (pato la mtu) kwa mujibu wa Benki ya Dunia. Hoja inaweza kutoka kuwa nchi hiyo ina idadi ndogo ya watu, vilevile utajiri wake wa mafuta ni mkubwa. Hata hivyo, msingi wa kuiheshimu nchi hiyo ni namna ilivyojiwekea mkakati wa kuhakikisha kila mwananchi anazalisha.

Ni kupitia mkakati huo wa Qatar, ndiyo maana jamii ya watu wasiojiweza, mayatima, wazee na wajane, wanafikiwa kwa urahisi na kupata huduma muhimu za kijamii. Kila mwananchi kwa maisha yake, anajiona kabisa anafanana na pato la taifa linalotengenezwa na nchi.

Muhimu zaidi ni kuwa wale wanaoonekana kuwa na mawazo pamoja na maarifa makubwa, wanawezeshwa na kujengewa uwezo kwa matumaini kwamba Taifa lenye raia wengi wenye uwezo, ndilo huwa na wastani bora wa kipato.

Hivyo basi, tayari Ruge amelala. Watu watamlilia na atakumbukwa sana. Hata hivyo, ameacha deni kuhusu sera ya kiuchumi yenye kutazama vipawa vya watu. Mtaani kuna akina Ruge wengi. Wasiachwe wafe bila kuokoa mamia ya Watanzania. Wajengewe uwezo ili maarifa yao yalifae Taifa. Kufanya hivyo ndiyo kumuenzi Ruge.