ANTI BETTIE: Sielewi anataka nini, kila ninachovaa anadai sipendezi - VIDEO

Sunday March 10 2019

Mume wangu nahisi ananitafutia sababu, nikivaa suruali hataki, gauni anasema sijapendeza, nguo za vitenge anasema nimezeeka.

Nikisuka nakosea, nikichana hataki.

Anti kwa kweli sijui anataka nini?

Fanya hivi kwa muda wa mwezi mmoja mwambie akupangie nguo za kuvaa anazopenda yeye uone chaguo lake ni nini.

Siku nyingine muulize kijanja “Mume wangu unapenda mwanamke avae nguo za aina gani, au mwanamke anayekuvutia ni anayevaa nguo gani” jibu atakalokupa utajua anachokitaka.

Ila usijibane sana wakati mwingine ni bora kufanya kile kinachokupa raha ilimradi hakivunji sheria na kukutoa utu wako mbele ya jamii.

Tumekula tunda gizani kwa miaka mitatu

Anti habari! Naomba ushauri wako kwa sababu simuelewi mke wangu. Licha ya kujitahidi kwa kipindi cha miaka mitatu kumuelewesha kuwa nashindwa kukutana naye faragha gizani hanielewi.

Ili nifurahi kukutana naye faragha basi tuzime taa, ikiwa inawaka anajifunika maguo usoni na hajiachi ipasavyo.

Nifanyeje?

Miaka mitatu unakutana na mwenzako gizani? Unaniangusha. Unastahili lawama wewe kabla ya mkeo, unawezaje kukutana na mkeo gizani kwa miaka mitatu?

Sasa kulimaliza hilo tatizo ulilolifuga anza taratibu. Anzisha tabia ya kukutana naye faragha mchana, hakikisha kila unapopata nafasi ya kuwa nyumbani unafanya hivyo na anapaswa ajue siku hizi unapenda kufanya tukio muda huo.

Si mbaya hata ikiwa jioni ya saa 11 au 12 kwa sababu bado kunakuwa na mwanga wa kutosha, punguza kukutana naye usiku hii itamfanya azoee hali hiyo.

Lakini pia aking’ang’ania kujifunika nguo usoni jifanye umesusa na umuache, najua ni ngumu kuacha tonge mdomoni lakini jizuie ili umalize tatizo hilo.

Ukimuacha na kiu mara mbili, tatu atabaini hupendi mambo yake ya kujifanya kama mtoto mdogo, kataa kufanya mapenzi gizani kwa vitendo.

Hakatai lakini hafanyi

Habari, naomba ushauri labda utanisaidia kumaliza tatizo nililonalo.

Mume wangu kila ninachoona hakiko sawa na kumuomba asikifanye, anakubali lakini anakirudia.

Nifanyeje?

Usikae kimya. Huyo ni mumeo una haki ya kumwambia kila kinachokukera, kama amefikia hatua ya kutokukusikia washirikishe wasimamizi wenu wa ndoa katika hilo kwa sababu ipo siku utamkataza jambo la maana atakuitikia halafu atalifanya na kusababisha madhara. Acha kulalamika unapozungumza naye, jenga hoja, inawezekana unapomwambia unakuwa umeshakata tamaa.

Advertisement