Siri shule za jinsi moja kutamba kidato cha nne

Muktasari:

Katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2017 na 2018, nusu au zaidi ya shule zilizofanya vizuri zaidi ni za wasichana pekee.

Wasichana wanaweza. Hakuna zaidi ya kauli hii ambayo mtu yeyote anaweza kuitoa hasa anapotazama matokeo ya mitihani ya kidato cha nne nchini.

Kila yanapotangazwa matokeo hayo na kutajwa shule kumi bora, majina ya shule zenye wasichana pekee hazikosekani katika orodha hiyo.

Kwa mfano, mwaka huu katika matokeo yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), shule tano ikiwamo iliyoongoza kitaifa ni shule za wanafunzi wasichana pekee.

Shule hizo ni St Francis Girls, Marian Girls, Bright Future Girls, Canossa na Bethel Sabs Girls.

Katika matokeo ya mtihani wa mwaka 2017 shule hizo zikatia fora kwa kutoa shule sita ambazo ni Feza Girls, Marian Girls, St Francis Girls, Bethel Sbas Girls, Anuarite, Canossa

Siri ya ufaulu wa wasichana

Mkurugenzi wa Taasisi inayojishughulisha na maswala ya Kisaikolojia (REPSSI), Edwick Mapalala anasema kiuhalisia ni rahisi kuwadhibiti wanafunzi wa kike wakiwa peke yao kwenye shule zao kuliko za mchanganyiko na hiyo ndiyo sababu ya ufaulu wao.

“Walimu wenyewe wanasema wanapowafundisha wanafunzi wa kike peke yao usikivu wao darasani huwa unakuwa mkubwa zaidi, kwa sababu tayari wanakuwa wameshapewa mafunzo mengi ya kujitambua, maadili, kujitunza, kuheshimiana na mengine mengi,” anasema.

Anasema kisaikolojia, mwanafunzi wa kike anapojitambua na kuwekeza nguvu kwenye kile anachofanya matokeo yake huwa makubwa.

Anasema kiuhalisia macho ya jamii, Serikali, mashirika na taasisi zisizo za Serikali yanawatazama watoto wa kike kama kundi maalum linalohitaji kuangaliwa kisaikolojia kuhakikisha wanafanya vizuri.

Mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia Frank John anasema utafiti mwingi aliopitia unaonyesha kuwa wavulana hata wakiwa peke yao shuleni, huwa ni wasumbufu zaidi kuliko watoto wa kike.

Anasema matokeo ya hivi karibuni yanaonyesha wasichana wanafanya vizuri darasani, kwa sababu wanajituma zaidi ikilinganishwa na wavulama.

“Sababu kubwa ya wasichana kufanya vizuri ni usikivu darasani unaotokana na malezi wanayopata shuleni hasa wakikaa bwenini.

‘‘Hata huko kwenye jamii wasichana wapo karibu zaidi na mama zao sasa kama mtoto ana mama mwenye weledi na maadili, huyu lazima afaulu tu,” anasema.

Anasema kwenye mikoa yenye shughuli nyingi za kiuchumi, wavulana huipa kisogo elimu kwa kukimbilia kwenye biashara na kuwaacha wasichana wengi zaidi darasani.

“Kiukweli, wavulana wana mambo mengi zaidi wakati wasichana wasiporubuniwa na kupata ujauzito, wakitulia wanafanya vizuri sana darasani,” anasisitiza.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Dk Jimson Sanga anasema ni ukweli usiopingika kuwa mtoto wa kike akipata mazingira salama ya kusoma, asipokutana na vishawishi na kupewa mahitaji yake yote muhimu, ana uwezo mkubwa wa kufaulu masomo yake darasani.

Anasema shule nyingi zilizofanya vizuri ni zile za mashirika ya dini ambazo, moja ya suala muhimu ni maadili.

“Katika shule za seminari za wasichana, suala la maadili ndio jambo namba moja, mtoto akiwa kuwa mwenye maadili kufanya vizuri kwenye sekta nyingine ni rahisi zaidi kwa sababu atakuwa msikivu,” anasema.

Anasema malezi hafifu kwa wasichana huwafanya washindwe kujiamini na kujikuta wakitumbukia kwenye mikono ya walaghai na mwisho wake kuacha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo mimba.

Mratibu wa Elimu Tanzania (Tenmet), Cathleen Sekwao, anasema vikwazo vya wanafunzi wa kike vinapoondolewa shuleni kinachotokea ni ufulu mzuri darasani.

Ili shule iwe na ufaulu mzuri anasema lazima iwe na walimu mahiri, mazingira bora ya kujifunzia na uhakika wa wanafunzi kupata vifaa vya kujifunzia na vinavyohusu miili na maisha yao.

Mzazi athibitisha

Anitha Kondya ambaye ni mama wa watoto sita watatu ambao wote ni wasichana, anakiri kuwa hata wakiwa nyumban watoto wake wake wana muda wa kujisomea zaidi kuliko wa kiume.

“Wakati mwingine utaona wa kiume wapo kwenye michezo na wasichana wanafanya kazi za nyumbani baadae kujisomea. Watoto wa kiume mpaka uwaambie ndio watafanya lakini sio kwa wao wenyewe kuamua,” anasema.

Wavulana nao

Tofauti na shule mchanganyiko, wavulana nao wakiwa peke yao wana uwezo wa kufanya vizuri. Ukiondoa shule za wasichana kutamba katika matokeo, baadhi ya shule za wavulana pekee kama Marian Boys, Feza Boys na Shamsiye nazo zimekuwa zikichuana na shule za wasichana katika kundi la shule 10 bora.

Kwa mfano, katika matokeo ya mwaka huu, shule ya wavulana Marian ya mkoani Pwani imepambana vikali na kuwa shule ya tatu katika orodha ya shule 10 bora iliyotawaliwa na shule za wasichana.

Hata matokeo ya mwaka 2017, shule za wavulana pekee hazikukosa kuingiza mguu katika orodha ya shule bora.

Shule hizo zilizofanikiwa kupenya zilikuwa ni Feza Boys, Shamsiye Boys na Marian Boys.