GOZI LA NG'OMBE: Taifa liwaombe Simba vitabu walivyotua navyo

Kupata somo ni jambo moja na kujifunza ni jambo jingine. Unaweza kupewa somo na bado likawa gumu kwako na ndio imekuwa asili yetu Watanzania. Tulishajikuta kwenye vizingiti vingi, changamoto kubwa na matukio ambayo yalipaswa kutuweka kwenye akili iliyonyooka lakini bahati mbaya katika namna nyingi, somo lilikuwa gumu kuingia katika akili zetu.

Msimu wa mwaka mmoja kabla ya leo unaposoma makala hii, klabu ya Simba ilikuwa inaelekea kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, wakati huohuo ilikuwa kwenye mchakato wa kubadili aina ya umiliki na uwekezaji kwenye klabu hiyo. Kwenye kilele cha ubora wake, kulikuwa na sauti iliyokuwa inapazwa juu ambayo iliwakilisha Simba ni nani, iliitwa Haji Manara.

Huyu aliamua kusema na haikuwa jambo baya, aliamua kuongoza imani ya mashabiki na ilikuwa kwa kila lenye kheri kabisa na pia aliamua kuwa mtu wa kuongeza hamasa klabuni, jambo jema na linalovutia.

Kwenye majira ya kiangazi kipindi cha usajili, ni yeye pia aliyeshika hatamu kuliko hata mafanikio ya klabu na alitangaza usajili unaokadiriwa kufikia bilioni moja za Kitanzania. Fedha nyingi kwelikweli ukiwa unazungumzia soka letu, hasa kama mpinzani aliyepanda daraja ni Alliance, Biashara na JKT Tanzania.

Moja kati ya watu ninaowapenda kwenye usimamizi wa soka pamoja na udhaifu wake, bwana Lawrence Mulindwa pamoja na kumiliki klabu ya Vipers nchini Uganda na kuwa katika mipango ya muda mrefu ikiwemo kumiliki uwanja wa kisasa, bado anaamini katika kujifunza na “role model” wake mkubwa akiwa ni Moise Katumbi na namna alivyoifikisha mbali TP Mazembe.

Mulindwa anaamini kuwa klabu yake bado ipo katika hatua za kujifunza kipi cha kufanya na kipi cha kuacha. Nimemkumbuka huyu kwa sababu ni vyema siku zote kuamini katika kuhitaji kufahamu yale ambayo wengi hawayafahamu na ndilo somo ambalo Simba inatakiwa kuwa imelipata ikiwa katika nchi za DRC Congo na kisha kwenye jiji la Alexandria pale nchini Misri.

Huku kote walipata adhabu ya mabao matano huku ya Misri ikiwa mbaya zaidi kwani Al Ahly walienda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakishika simu na kusalimia wake zao ama wapenzi wao kwa sababu kazi walishaimaliza.

Katika mechi zote mbili, Simba ilichezesha wachezaji wa zaidi ya saba wa kigeni na wote walionekana ni wachezaji wanaojifunza soka, wakapewa kozi maalumu iliyokuja kama adhabu. Inawezekana hii ilikuwa dhihaka kwa Simba lakini inabidi iwe dhihaka kwa Taifa, kwa sababu sioni klabu yenye kikosi ambacho kingeweza kusimama kiume dhidi ya klabu hizo.

Wakati Simba ikiwa imevunja rekodi ya usajili Tanzania kwa kile kilichoitwa bilioni moja, klabu ya Al Ahly wao walisajili mchezaji mmoja ambaye aliwazidi Simba kila kitu kwenye mchezo wao, Hussein El Shahat kwa kiasi cha bilioni kumi za Kitanzania. Kwa tafsiri nyingine ni kuwa Al Ahly wana uwezo wa kununua mchezaji mmoja kwa thamani mara kumi ya kikosi cha Simba.

Sahau kuhusu uwezo wao wa kumchukua Ramadhani Sobhi kutoka Huddersfield inayoshiriki Ligi Kuu ya England kwa mkopo, klabu zetu inabidi zitambue safari bado ni ndefu. Al Ahly inatoa somo la kujifunza uwekezaji na kuvipa thamani klabu zetu ili kupata wadhamini sahihi na kuendana na idadi ya wapenzi wa soka waliopo nchini, jambo ambalo tumeamua miaka yote kulisusia kwa makusudi.

Wakati Al Ahly wakitufundisha kuhusiana na uwekezaji, AS Vita wao wanaishi katika dunia anayoishi TP Mazembe na maisha yanaendelea. Wakati TP Mazembe ikiwa na msuli wa kusajili mastaa kutoka sehemu mbalimbali, AS Vita wao sio tabia yao. Kwenye kikosi cha wachezaji 30, kuna watano pekee wa kigeni huku kikosi cha kwanza mara nyingi akiwa mmoja tu naye ni kipa Nelson Lukong kutoka Kameruni.

Hawa wanaishi katika kusaka vipaji sahihi na kuviweka pamoja na wanaendelea kuishi katika mashindano ya Kimataifa na ndani ya nchi yao. Klabu zetu hazina yote haya, hazifahamu kuskauti wachezaji sahihi na hazifahamu kufanya na kutumia uwekezaji mkubwa wa soka.

Al Ahly na AS Vita zimeonyesha kuwa sisi ni wajuaji katika elimu ambayo hatujaipata. Tunajiita wanasayansi na hatufahamu tafsiri ya teknolojia. Wametupatia vitabu viwili vya mafunzo kupitia Simba, kama Taifa tuwapokee na tuwaombe watugawie vitabu hivi kwa pamoja tujifunze elimu ya maendeleo ya soka. Sisi bado ni “wajinga”, tunahitaji kuelimishwa kwenye hili.