Teknolojia kwa watoto wenye mahitaji maalumu

Muktasari:

  • Mtoto kwa hali yoyote aliyonayo anastahiki kupata haki ya elimu. Na kwa maendeleo ya teknolojia, hakuna mtoto anayepaswa kukosa fursa hiyo muhimu maishani.

Kuwa na mtoto ulemavu wa akili haina maana kwamba hawezi kuishi kwenye dunia wanayoishi watoto wengine na kufanya mambo kama wanayofanya wengine.

Watoto hawa wanakuwa katika kundi lenye mahitaji maalum, lakini wanaishi maisha kama wanayoishi watoto wa kawaida ikiwa ni pamoja na kupelekwa shuleni, kucheza na kufundishwa teknolojia.

Wanasayansi hawajalitenga kundi hili kwani nao wamewatengenezea teknolojia mbalimbali zinazoweza kuwarahisishia maisha wakiwa na hali zao.

Katika safu hii wiki hii tutaangalia namna ambavyo teknolojia inavyoweza kuwa msaada katika masomo ya mtoto mwenye mahitaji maalum na akaweza kufanya vizuri darasani na kuelewa kwa haraka anapofundishwa.

Teknolojia kwa watoto walemavu

Zipo Apps mbalimbali kwa ajili ya kundi hili ila kama wewe ni mzazi mwenye mtoto wa aina hii unaweza kupakua chache ambazo utazitumia kumsaidia anapokuwa nyumbani.

Learn with Rufus, hii ni programu inayomuwezesha mtoto kujitambulisha na kumuelekeza kuvifahamu vitu muhimu vinavyomhusu.

Walimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalum huitumia programu hii kuwaweka pamoja na kuwaunganisha watoto kuwa marafiki.

Nyingine ni Montessori numbers. Hii ni maalumu kwa ajili ya kuwafundisha namba na jinsi ya kuzitumia. Hapa atajifunza kuandika na kuhesabu kuanzia 1 hadi 1,000.

Kwenye kuhesabu atafundishwa kwa kutumia sauti, video na maandishi ili kumuwezesha ubongo wake kuzikumbuka namba. Programu hii pia itamfundisha hesabu za kujumlisha na kutoa.

Proloquo2Go, hii ni kwa ajili ya watoto ambao wanapata wakati mgumu kuzungumza kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya yakiwamo mtindio wa ubongo, uziwi na mengine mengi.

Kazi kubwa inayofanywa na programu ni kumpa mafunzo mbalimbali kwa njia ya sauti yanayolenga kumuwezesha mtoto kuanza kujifunza kutamka maneno.

Kwa wale wenye tatizo la kushindwa kusoma na kutamka maneno kwa usahihi The Sounding out Machine ndiyo programu inayoshauriwa.

Hii inamfundisha mtoto kutamka herufi moja moja na hatimaye kuunganisha neno hadi sentensi.

Programu hii pia ina uwanja wa kuandika ambapo mwanafunzi atajifunza kuandika neno analolitamka.

App hii pia ni msaada kwa mwalimu anayefundisha watoto wenye matatizo maalum.

App nyingine muhimu ni Super why, hii inalingana kidogo na hiyo ya hapo juu lakini imeongezwa vitu vingi ambavyo ni msaada kwa mtoto.

Mafunzo yake yanayolewa kwa njia ya michezo (games) ikijumuisha upangaji wa herufi, maneno, kutamka maneno, namba, midundo na hatimaye kumuongezea mtoto stadi za kusoma na kuandika.

Programu hii pia inatoa mazoezi mbalimbali ikiwemo kujaza nafasi zilizoachwa wazi, hii yote ni kumpa mtoto nafasi ya kuchangamsha ubongo.