Tunapoelekea tutaogopa kuwatambulisha watoto wetu

Sunday July 8 2018

 

Hatuwezi kuishi nyuma ya muda, labda tukiamua. Na kama mmoja wetu akiamua hivyo basi kuna mawili, kwanza huenda maisha yakawa mazuri kwake binafsi lakini yenye kuwakera watu wake wa karibu.

Pili huenda maisha yakawa yanamkera yeye binafsi na kumkera zaidi kila anayemzunguka.

Nyuma ya muda huu tulionao sasa sehemu pekee ya kuhifadhi kumbukumbu za picha ilikuwa ni kwenye albamu. Kila familia ilikuwa na ya kwake. Ukitembelea, ukipewa, ukaitazama utakutana na sura zote humo zilizonaswa katika nyakati tofauti — Baba, mama, watoto na zaidi.

Lakini katika muda huu tulionao mambo yamebadilika. Picha hatuziweki tena kwenye albamu, badala yake kwenye mitandao ya kijamii. Hii imetoa fursa kwa watu wapya hata tusiowafahamu wajue maisha yetu — japo sio kwa uhakika,

Japokuwa kwa kupitia picha mbili tatu tunazoziweka kwenye akaunti zetu za mitandao ya kijamii wanapata taswira fulani hivi.

Ukiweka picha ya ‘kagari kako’, watu watajua ushaacha kutembea umesimama siku hizi. Ukiweka ya mkeo wataelewa kwamba kumbe jamaa sio bachela tena. Ukiwaweka watoto watu watafahamu kuwa kumbe fulani ni baba.

Sasa hivi, wengi wanaotumia mitandao hii hawana woga wa kuchapisha picha za familia. Yaani mtu aliyeoa na ana watoto haoni shida kuchapisha picha ya familia yake kwenye mitandao yake ya kijamii —lakini tunapolekea hili litakatika na badala yake kama kuchapisha tutakuwa hatuweki kabisa picha za watoto wetu.

Hili litafika ukomo kwa sababu kwa kweli wanawake wanatuchanganya. Wanatukosesha amani na watoto wetu kwa kiasi kwamba usipokuwa na moyo mkubwa na mgumu, moyo wa kiume wenye kustahimili kweli kweli unaweza ukafa kwa ‘stress’ tena mapema kabla ya ahadi.

Tunakosa amani kwa sababu kiwango cha kumilikishwa watoto ambao si wetu kimekuwa kikubwa mno. Mwanamke anakwambaia ujauzito ni wako, unahudumia miezi tisa, anazaliwa mtoto, unalea miaka 6 halafu linaibuka jitu tu kutoka lisipojulikana linakwambia mtoto ni damu yake.

Inatisha, na hii itatufanya tuwe na wasiwasi na tuache kujivunia watoto wetu. Unaweza ‘ukapost’ picha yako uko na unayeamini kuwa ni mwanao kwenye mitandao ya kijamii halafu jitu likaja kuandikwa kwa chini. “Asante kwa kunilelea mwanangu.”

Wanaume tuna mioyo ya uvumilivu sana lakini kwenye matukio magumu ya namna hii mioyo yetu inashindwa. Inashindwa kwa sababu kwanza ni fedhea.

Ulishajinadi na mtoto miaka nenda rudi ukiamini ni mwanao na hata Jamhuri inafahamu hilo — yaani kila sehemu jina lako linatumika kama la baba wa moto, shule, hospitali na kila linapohitajika, lakini kumbe muda wote huu unamilikishwa mzigo wa mwenzio.

Kwa hali hii tutashindwa kuwatambulisha watoto wetu popote pale.

Advertisement