UCHAMBUZI: Turekebishe Katiba kabla ya uchaguzi-Dk Malisa

Wednesday February 13 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Aliyekuwa mgombea uspika wa Bunge kupitia Chama cha Kijamii (CCK), Dk Godfrey Malisa amependekeza mambo matano yafanyike katika Katiba kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 ili kuijenga Tanzania ya kidemokrasia.

Katika andiko lake kwa gazeti hili, Dk Malisa ambaye kwa sasa yuko katika Chama cha Tanzania Labour (TLP), ameyataja mambo hayo kuwa ni: Mosi, iundwe Tume huru ya uchaguzi na mfumo wake upendekezwe na vyama vyote, pili, matokeo ya kura ya rais yaruhusiwe kupingwa mahakamani, Tatu, mshindi wa uchaguzi wa rais apate si chini ya asimilia hamsini ya kura zote, nne, uchaguzi wa marudio wa Rais ukishindwa kumpata mwenye zaidi ya asilimia hamsini, iundwe serikali ya umoja wa kitaifa na tano, pawepo wagombea binafsi katika ngazi zote za uchaguzi. Uchaguzi Mkuu wa 2020 hauko mbali na hata maandalizi yake yameanza kwenye baadhi ya vyama vya siasa.

Wengi wetu tumeendelea kupiga kelele kwamba Katiba tuliyo nayo hivi sasa ina mapungufu mengi yanayominya uhuru wa kuchagua kiongozi tunayemtaka. Kelele hizi ndizo zilizopelekea kuanzishwa mchakato wa kuundwa kwa Tume ya Jaji Warioba na hatimaye kuandikwa rasimu ya Katiba mpya ambayo mpaka sasa imekwama.

Ukifuatilia chaguzi zilizofanyika katika miaka mitatu iliyopita, utaona kwamba ni chama kimoja tu ndio kimekuwa kinashinda tena kwa asilimia 100. Hapa kuna shida kubwa, na kama tukiingia katika uchaguzi wa 2020 katika mazingira haya, vyama vya upinzani havitaambulia kiti hata kimoja.

Tulipoambiwa kwamba hakuna fedha za kura ya maoni kuhusu rasimu ya Katiba mpya, wengine tulisikia ambalo halikusemwa, kwamba ‘kupatikana Katiba mpya kabla ya uchaguzi kutakiweka chama tawala mashakani’. CCM haiko tayari kutengeneza mazingira ya kujitoa madarakani.

Kwa sababu hiyo wapenda demokrasia wajue kwamba tukitegemea hisani za watawala kutupatia Katiba mpya tutangoja mpaka siku ya kiama. Tusiendelee kupiga kelele za mpita njia ambazo hazimnyimi mwenye nyumba usingizi. Tuchukue hatua madhubuti za kudai haki ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki.

0716-810677

Advertisement