Tuufumue mfumo wa elimu tupate maendeleo ya kweli

Wednesday December 5 2018

 

By Padri Privatus Karugendo

Duniani kuna mambo ambayo ni muhimu kuyashughulikia. Mambo haya ni elimu, siasa, vijana na uchumi. Nchi ambazo zimezingatia mambo haya na kuyashughulikia kwa umakini, zimepiga hatua kubwa ya maendeleo. Zilizoyapuuza, ziko nyuma kimaendeleo.

Katiba ya Tanzania ibara ya 11(3) inasema, “Serikali itafanya jitihada kuhakikisha kwamba watu wote wanapata fursa sawa ya kutosha kuwawezesha kupata elimu na mafunzo ya ufundi katika ngazi zote za shule na vyuo vingine vya mafunzo.”

Serikali imejitahidi kiasi fulani kufuata Katiba kuhusu elimu. Tatizo linalojitokeza ni mfumo na ubora wa elimu inayotolewa ambayo baada ya uhuru iliendelea kutolewa kwa kufuata mfumo wa kikoloni.

Wakati wa ukoloni watu walielimishwa kuwatumikia wakoloni. Ilikuwa inaandaliwa nguvu kazi, hawakuwa na haja ya kuandaa watafiti, wagunduzi wala watu wa kuliendeleza Taifa. Mitaala iliyotengenezwa ilikuwa ikilenga kumfundisha mtu katika mtindo wa kukariri tu.

Lakini, ili Taifa liendelee, linahitaji wavumbuzi, watafiti, watu wenye fikira pevu ambao wanazama kwenye fikra na kuchambua mambo mbalimbali.

Pia, linahitaji wanafalsafa, wenye kuleta mawazo mapya na kuyachambua kwenye jamii. Na wafanye hivyo kwa uhuru na kwa kujiamini. Wafanye hivyo bila shinikizo au mahaba ya chama chochote cha siasa. Wawe huru kufikiri bila kushinikizwa na mtu au taasisi yoyote yenye madaraka au nguvu za fedha.

Kinachohitajika kwa sasa ni kutengeneza mitaala mipya ambayo italenga kutoa elimu ya kumkomboa mtu kifikra akawa na uwezo wa kuhoji na kufanya utafiti hadi kuelekea uvumbuzi wa vitu mbalimbali. Tunahitaji mfumo wa elimu utakaowaandaa vijana kuwa wanasiasa bora, ambao badala ya kuvitanguliza vyama vyao vya siasa, watalitanguliza Taifa. Vijana ambao watashiriki kutengeneza sera za vyama vyao zenye kulenga kuleta maendeleo ya Taifa zima. Siasa za kujenga uzalendo na mshikamano wa Taifa zima. Vijana ni kiungo muhimu cha kizazi na kizazi, ili Taifa liendelee na kustawi. Bado kuna uhaba wa walimu na maandalizi yao si mazuri. Pia, walimu hawana motisha wa kufundisha maana walio wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu na wakati mwingine stahili zao zinacheleweshwa. Shule nyingi majengo yake yamezeeka, ingawa Serikali inafanya jitihada ya kukarabati shule bado jitihada kubwa inahitajika.

Ili kuboresha uchumi wetu kuna haja ya kuiboresha kwanza elimu yetu na kuwaandaa vijana wetu waweze kuukabili ulimwengu huu unaobadilika kila siku ya Mungu. Jambo hili linahitaji msimamo wa kitaifa. Ni lazima liwe jambo ambalo litaheshimiwa na wanasiasa wote. Vyama vyote vinavyotengeneza sera na kujiandaa kuingia madarakani ni lazima vizingatie kitu hiki. Bila elimu bora na kuwaandaa vijana vizuri ni vigumu kujikwamua kiuchumi.

Padri Privatus Karugendo +255 754633122

00000000

Kutokana na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia yanayojitokeza hivi sasa kijana ndiye mwenye nafasi kubwa ya kujifunza na kuonyesha ujuzi wake katika Taifa hivyo kuleta maendeleo nchini na uvumbuzi katika nyanja mbalimbali. Mambo ya kujiuliza ni kwamba je, kijana huyu ana nafasi gani ya kupata ujuzi, kuuendeleza na kuutumia? Mitaala yetu ya shule za msingi na sekondari inasaidiaje kumwandaa kijana kupambana na hali hii?

Kuna hatari kubwa ya kuwa na taifa dhaifu lenye hali mbaya katika nyanja zote – kiuchumi, kisiasa na kijamii endapo kijana wa sasa hakuandaliwa ipasavyo kushika nafasi za kusimamia masuala hayo. Aidha kijana huyu anapaswa kuandaliwa kwa kupewa elimu bora itakayombadilisha fikra na mtazamo wake kimaisha ili kumwezesha kupambana na changamoto muhimu za kimaisha kikanda na kidunia. Haya yote yanafanikiwa endapo tu kijana ataandaliwa kupata elimu.

Ili kuboresha uchumi wetu kuna haja ya kuiboresha kwanza elimu yetu na kuwaandaa vijana wetu waweze kuukabili ulimwengu huu unaobadilika kila siku ya Mungu.

Jambo hili linahitaji msimamo wa kitaifa. Ni lazima liwe jambo ambalo litaheshimiwa na wanasiasa wote. Vyama vyote vinavyotengeneza sera na kujiandaa kuingia madarakani ni lazima vizingatie kitu hiki. Bila elimu bora na kuwaandaa vijana vizuri ni vigumu kujikwamua kiuchumi. Elimu yenye kufaa ipewe kipaumbele na yeyote aliye na nia njema na taifa letu.

Padri Privatus Karugendo

+255 754633122

Advertisement