USHAURI WA DAKTARI : Kutokwa uchafu katika chuchu

Muktasari:

  • Kwa kawaida uchafu huu unaweza kuwa ni maji maji yenye rangi ya njano/ugoro, ute ute, maziwa, damu damu au usaha. Hata kwa wale wanawake waliofikia ukomo wa hedhi uchafu huu si lazima uwe ni kiashiria cha ugonjwa.

Uchafu katika chuchu za mwanamke wa rika lolote ni jambo ambalo linaloweza kuwa ni la kawaida au kiashiria cha uwepo wa tatizo. Mara nyingi hali hiyo hutokea kwa ziwa moja.

Inaweza kutokea kwa wanawake (sio lazimwa wawe wanaonyonyesha) kutokwa na uchafu ulio kama majimaji ukitoka au ukachuruzika kupitia tundu zilizopo katika chuchu.

Kwa kawaida uchafu huu unaweza kuwa ni maji maji yenye rangi ya njano/ugoro, ute ute, maziwa, damu damu au usaha. Hata kwa wale wanawake waliofikia ukomo wa hedhi uchafu huu si lazima uwe ni kiashiria cha ugonjwa.

Ieleweke kuwa uchafu wowote unaotoka katika chuchu ni lazima kila mwanamke achukulie kama ni kitu cha kuwa na tahadhari nacho na ashitakie mapema katika huduma za afya. Kufanya hivyo kunawezesha kujihami endapo ni tatizo la kiafya hatua madhubuti zichukuliwe mapema kabla ya ugonjwa kupiga hatua.

Taarifa za kitabibu zinaonyesha kuwa chini ya asilimia 10 ya wagonjwa wanaobainika kutokwa na uchafu katika chuchu huwa chanzo ni kuugua saratani ya matiti.

Vyanzo vingine vya kupata hali hii ni pamoja na matatizo ya mfumo wa tezi zinatoa vichochezi (hormons) na uwepo wa uvimbe usio wa saratani katika vifuko vya kuhifadhia maziwa.

Matatizo ya vichochezi ni pamoja na uwepo wa kiwango kikubwa cha kichochezi kijulikanacho kitabibu kama Prolactin, hali hii husababisha kutokwa na maziwa katika matiti yote mawili.

Uwepo wa shambulizi la bakteria ndani ya juu yaa ngozi ya chuchu, vifuko, vifereji vya kutiririsha maziwa pia vinaweza kusababisha hali hii.

Vilevile kupata vijeraha au vimichubuko vinavyoweza kuchangiwa kwa kujigonga au kukwaruzwa na nguo ikiwamo sidiria.

Ni muhimu kufika katika huduma za afya kushitakia tatizo hili kwa ajili ya uchunguzi, matibabu na ushauri. Matibabu hutegemeana na chanzo kilichobainika.

Tarajiwa kufanyiwa uchunguzi maalum wa matiti yote mawili na mtoa huduma lengo ni kubaini kama kuna uvimbe wowote au ni shambulizi la mlipuko wa kinga katika matiti.

Utokaji wa maziwa yote mawili kwa yule asiye nyonyesha ni ishara ya uwepo wa kiwango kikubwa cha kichochezi cha Prolactin. Dawa za matibabu hutolewa kurekebisha tatizo hili. Kama ni uambukizi wa bakteria dawa za antibiotiki hutolewa.

Kipimo maalumu cha picha ya xray kijulikanacho kama mammography hufanyika kutazama kama kuna uvimbe.

Uchafu wenye damu damu huenda ikawa ni ishara ya saratani ya matiti inayosambaa. Wakati wakutomasa matiti kama daktari hakugusa uvimbe wowote na kipimo cha mammography kikiwa ni kawaida maana yake hakuna uwezekano wa uwepo wa saratani.

Fika mapema katika huduma kwa ajili ushauri, pamoja na kupata elimu ya afya ya kujichunguza matiti unapokuwa mwenyewe.