Uhusiano wa William Ruto, Obado ni zaidi ya urafiki

Sunday November 25 2018

Makamu wa Rais, William Ruto akizungumza na

Makamu wa Rais, William Ruto akizungumza na Gavana wa Migori, Okoth Obado. Picha ya Maktaba 

By Dorothy Jebet

Kuna msemo unaosema siku ya kufa kwa nyani miti yote huteleza. Msemo huu huenda unamlenga Gavana wa Migori, Okoth Obado ambaye kwa mara nyingine wiki iliyopita alifikishwa kizimbani.

Obado ambaye baadhi ya Wakenya katika mitandao ya kijamii wamempa jina la utani Obado Okwisha kwa matatizo mengi ya kisheria yanayoweza kuzima maisha yake ya kisiasa, alinaswa na makachero Novemba 14 katika chumba cha chini ya ardhi (basement) katika Hoteli ya kifahari ya Hilton, jijini Nairobi.

Duru za kuaminika zinasema mwanasiasa huyo alikuwa anajaribu kutoroka lakini mkono mrefu wa sheria ukamfikia.

Siku moja kabla ya kukamatwa kwake, makachero walikuwa wamevamia nyumba zake jijini Nairobi na Migori ambapo walipata bunduki nane. Alifikishwa mahakamani na kuwekwa rumande.

Gavana huyo alikuwa anahudhuria mkutano ambao pia ulihudhuriwa na Makamu wa Rais, William Ruto katika hoteli hiyo.

Makamu wa Rais ni rafiki mkuu wa Obado na wawili hao wameanza kushirikiana katika mbio za urais 2022. Ruto alizuru Jimbo la Migori wiki iliyopita mara mbili kusaka wafuasi, pia waliandamana hadi jimbo jirani la Homa Bay ambapo walifanya mikutano ya hadhara iliyofana.

Hata hivyo, wabunge na maseneta wa chama cha Raila Odinga cha ODM walipuuza mikutano hiyo ya Ruto.

Inaeleweka kwa nini ODM haitaki kuhusishwa na Ruto na Obado. Kwa miaka kadhaa, gavana huyu ameendelea kujitenga na Raila na kuchora picha ya mwanasiasa muasi katika eneo la Nyanza ambapo Wajaluo wanaishi.

Katika sehemu hii ya Kenya, Raila ndiye mfalme. Neno lake ni kama sheria na wanaompuuza hupuuzwa. Ana ufuasi mkubwa na wanasiasa wachache wangetaka kumpinga ama kwenda kinyume na siasa zake.

Lakini Obado alienda kinyume na Raila 2013 alipowania ugavana kwa tiketi ya chama kidogo cha PDP. Na alimshinda mgombea wa ODM ambaye hakuamini angeshindwa. Alienda mahakamani akitaka ushindi wa Obado ufutiliwe mbali lakini aliambulia patupu.

Katika uchaguzi mkuu wa 2017, Obado aliwatetemesha tena maadui zake kwa kushinda ugavana kwa mara ya pili mfululizo licha ya kuwa alikuwa anajifanyia kampeni bila usaidizi wa walio karibu na Raila.

Wafuasi wa Obado wanaamini kwamba kiongozi wao anasulubiwa kwa sababu ya kukataa kufuata nyayo za Raila. Pia wadadisi wa siasa wanasema mwanasiasa huenda anaadhibiwa kwa kushirikiana na Ruto ambaye ana maadui wengi haswa wanaopinga siasa zake za 2022.

Kiongozi huyu alikuwa nje kwa dhamana ya Ksh5 milioni (Sh111 milioni za Tanzania) baada ya kuhukumiwa kwa mauaji ya kikatili ya mpenziwe na mtoto aliyekuwa tumboni Septemba mwaka huu.

Wadadisi wa siasa wanasema ushirikiano kati ya Ruto na Obado si mzuri kwa sababu gavana huyo anatuhumiwa kwa mauaji ya mpenzi wewe Sharon Otieno ambaye alikuwa na mimba ya miezi saba.

Obado amekiri kwamba ni yeye aliyempa mimba msichana huyo wa Chuo Kikuu cha Rongo katika jimbo la Homa Bay. Mwili wake na wa mtoto wake ilipatikana ndani ya msitu mapema Septemba.

Wakenya wanashangaa kwa nini Ruto anashirikiana na Obado ilhali anafahamu fika kwamba gavana huyo ni mtuhumiwa mkuu wa mauaji. Makachero na maofisa wa polisi waliochunguza mauaji ya Sharon na mwanaye walipata ushahidi wa kumweka Obad kizimbani.

Advertisement