Ukisikia presha za kujitakia ndio hizi sasa

Saturday May 25 2019Julie Kulangwa

Julie Kulangwa 

By Julieth Kulangwa

Taifa moja liliiteua siku ya Ijumaa kuwa ya mapumziko. Ilikuwa ni kosa la jinai kufanya kazi katika siku hiyo ikiwamo wanafunzi kwenda shuleni. Lakini iliiteua nusu siku ya Jumamosi kuwa siku ya kazi ili kufidia Ijumaa.

Kwa sababu wanafunzi wengi walikuwa wakimiliki seti moja ya sare za shuleni, ilikuwa rahisi kumjua mwanafunzi namna anavyofanya mambo yake kwa wakati.

Wanafunzi wanaofanya kazi kwa wakati walifika asubuhi Jumatatu wakiwa nadhifu.

Huenda waliitumia nusu siku ya Jumamosi kufanya usafi wa sare za shule na pengine Jumapili kwa ajili ya kupiga pasi na kusafisha viatu.

Wale wazembe wanaofanya kila kitu kwa presha, walifika shuleni wakiwa na sare ambazo hazikunyooshwa au mbichi kwa sababu walitumia Jumapili kufanya usafi.

Pengine mwanafunzi anayependa kufanya kazi zake dakika za majeruhi alifua nguo jioni na mvua ikanyesha. Hapo lazima aende shule na nguo ambazo hazikukauka vizuri au kunyooshwa zikiwa mbichi na hivyo kuzifubaza.

Advertisement

Ni kawaida kuandaa sherehe ya harusi kwa zaidi ya miezi minne lakini maandalizi muhimu kama gauni na suti yakawa hayajakamilika mpaka siku tatu kabla ya tukio lenyewe.

Januari kila mtu anahaha kutafuta ada ya mtoto ambayo aliifahamu tangu Januari iliyopita lakini hakuchukua jukumu la kuiandaa.

Huu ni kama ugonjwa wa kuambukiza kwa sababu hata Serikali inaweza kuanza maandalizi ya uchaguzi mkuu kwa presha ilihali iliufahamu utakuwepo tangu ulipoisha uchaguzi mkuu mwingine.

Si tabia njema kwa sababu haileti matokeo chanya. Kila kitu kinafanyika kwa presha kubwa matokeo yake huwa na gharama.

Kwa mfano huyo mwanafunzi ni dhahiri sare zake zitafubaa au kuchakaa kwa sababu hazipiti katika hatua sahihi wakati wa kufanyiwa usafi.

Sherehe zetu zimeleta migongano kwa ndugu na jamaa kwa sababu ya kukimbizana kukamilisha mipango.

Advertisement