Unatakiwa kufanya hivi mara unaposalitiwa na Mke/ Mume

Mambo vipi wapenzi wasomaji wa Makala ya MAPENZI! Bila shaka mko poa na mmeanza mwaka 2020 mkiwa na afya njema.

Katika ulimwengu wa mapenzi, wanandoa na hata wasio na vyeti vya ndoa wamekuwa wakisalitiana, na wapo wengine wanapofumania huchukua maamuzi mkononi na tena ya hatari! Uamuzi huu wa ghafla, wakati mwingine mfumaniaji huendeshwa na hasira, wivu na kupaniki.

Mara nyingi anaweza kumdhuru mwenza wake, kujidhuru mwenyewe kwa kujiua, kupambana na mgoni wake au kutoa talaka kwa hasira.

Jambo la kumdhuru na talaka ni zito sana, hasa unapoangalia mkeo/mumeo kuwa tayari mna watoto na wanahitaji huduma ya wazazi wote na malezi ya karibu. Ila niseme tu kwamba, kuachana na mtu unayempenda, mke au mume/mzazi hili la kumfumania lina maumivu makali sana. Hakuna kitu kibaya kama kugundua unayemjali na kumpenda kutoka rohoni hajatulia, anampa mtu mwingine hazina ya pumziko lako.

Je, ufanyeje unaposalitiwa na mke/mume wako? Hili ni swali zito sana.

Utamsamehe na kuendelea na maisha yenu ya ndoa? Na inawekana ukasahau yote yaliyotokea? Sio rahisi kusahau kama kweli unampenda na unamjali. Hata hivyo, naweza kukupa ushauri wa baadhi ya mambo ya kufanya ili kuendelea na uhusiano na kutengeneza dunia mpya ya mapenzi na kusahau yaliyopita.

Lakini naamini kabisa ndugu msomaji utakuwa unajiuliza au bado moyo wake utakuwa na mengi ya kuhifadhi. Unafikiri upata nafuu ya maumivu ya kusalitiwa na mumeo/mkeo baada ya kujua anakusaliti?

Je, uaminifu kwako kuhusu uhusiano wenu utakuwepo tena? Utakapopata sababu ya kwanini alikusaliti; inaweza kukusaidia kumrudisha na kummiliki upya? Nafahamu wazi kuna wakati utakuwa unasumbuliwa na picha halisi ya tukio zima la usaliti. Inawezekana ukasumbuliwa na msongo wa mawazo wa tukio hilo na ukaendelea kuteseka na kukosa usingizi kabisa.

Kwa hisia zako za siri, inawekana bado ukawa na wasiwasi huyo msaliti wa mkeo/mumeo akawa bora kitandani zaidi yako na kumfanya sweetie wako kumkumbuka na kukusahau licha ya kuishi naye nyumba moja? Chumba kimoja na kitanda kimoja? Unawaza huenda wasiwasi na mawazo juu ya usaliti wake ukawachanganya watoto? Hivi umeshawahi kufanya uchunguzi kwanini mumeo/mkeo wako anakusaliti? Na cha kushangaza ni kwamba unajitahidi kumfanya awe na furaha, kumpa kila anachokitaka chini ya jua na mwezi.

Ukweli ni huu, hakuna ndoa bora duniani. Na pia hakuna mwanaume wala mwanamke bora duniani. Ninachoamini ndoa ni ahadi na vyeti vilivyopo katika maandishi ambavyo mtu anapewa bila hata kupata mitihani ya kufaulu au kufeli. Ila inaonekana amefalu pale anapokuwa amefunga pingu za maisha.

Kama mambo hayaendi vizuri katika ndoa, hupaswi kutoka nje ya ndoa yako tukufu na kumsaliti mwenza wako. Pia, haijalishi ni matatizo gani makubwa ndani ya ndoa yako. Mkeo ana nafasi ya kuhakikisha anatatua tatizo hilo ambalo ameliona na sio kuchagua kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine. Hili ni kosa kubwa sana.

Hivyo, usijichoshe mwenyewe kwa kuanza kuudanganya moyo wako na kutafuta suluhisho nje ya ndoa. Iwapo mumeo/ mkeo ana mapungufu, kaa na zungumza naye kwanza na sio kutafuta mbadala wa kimyakimya.

Iwapo hakufikishi kileleni katika ulimwengu wa kimapenzi, sio tiketi ya kuanzisha uhusiano bandia. Kufanya hivyo ni kosa kubwa.