Usichojua kuhusu kilimo cha Chia

Saturday February 9 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Kwa walio wengi kilimo cha chia kinaweza kuwa kigeni machoni na masikioni. Lakini ni aina ya kilimo ambacho kama mtu atakichangamkia kina manufaa lukuki.

Chia ni aina ya mmea unaotaka kufanana na zao la ufuta huku ukiwa na mbegu zinazotaka kufanana kama vile za mchicha. Ni zao linalotumika kama kirutubisho cha afya ya akili na mwili.

Simulizi ya mkulima Hindoo Yusuf

“Nilivutiwa na kilimo cha Chia baada ya kutembelea maonyesho ya bidhaa za Chia nchini Kenya, nilishangaa sana nilivyoziona maana zinafanana kama ulezi au mbegu ya mchicha, hivyo nikavutiwa na nikataka kujifunza ziadi juu ya Chia” anasema Hindoo Yussuf , ambaye ni mkulima wa zao la Chia.

Anasema yeye alianza kilimo hicho mwaka 2007, kwa kuanza na eneo la robo heka kwa majaribio katika wilaya ya Muleba na alivyoona mambo mazuri, alihamishia kilimo hicho katika wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

“Kwa kweli maonyesho ya Chia yalinivutia sana na nikawauliza wale waliokuwa wanauza bidhaa hiyo, wakaniambia kuwa wao wananunua kutoka Uganda lakini hata Kenya, maeneo ya Meru wanalima”anasema.

Baada kurudi nchini alianza kulima na kutafuta soko japokuwa ilimuwia ngumu kuweza kupata soko la uhakika kutokana na zao hilo kuwa geni kwa watu.

“Hivyo nilianza kuwaelezea Chia ni kitu gani na ina manufaa gani, hapo nikaanza kufungasha Chia katika makopo yenye ujazo wa gramu 100 kwa bei ya Sh 5000, gramu 250 kwa Sh 10,000 na gramu 500 kwa Sh 15,000” anasema Yussuf.

Anasema kuwa katika ekari moja ya Chia, mkulima anaweza kuvuna gunia mbili hadi tatu, huku kilo moja ikifikia kuuzwa kwa Sh 10,000 kwa bei ya sasa.

“Kwa sasa naendelea kujifunza na nimeanza kushirikiana na kampuni ya mmoja iliyopo Berlin nchini Ujerumani, ambayo ni wao wanauza bidhaa hii nchini huko” anasema Yussuf, ambaye pia analima mchaichai.

Anasema malengo yake ni kuwa mzalishaji mkubwa wa kilimo cha Chia hapa nchini na kufungua kiwanda ambacho kitaweza kuzalisha bidhaa inayotokana Chia badala ya kuuza mali ghafi nje ya nchi.

Kilimo cha Chia

Kwa mujibu wa Dickson Tumgonze ambaye naye analima zao hili, mikoa inayostawisha zao hilo ni Morogoro, Tanga eneo la Handeni , Moshi, Mbeya maeneo ya Tukuyu pamoja na Kigoma.

“Mikoa yenye ukamwe mwingi na ardhi iliyochoka zao la Chia halikubali hata kidogo, lakini hata mikoa yenye barafu kama Njombe, zao hili halikubali kuota pia” anafafanua Tumgonze.

Anasema kwa kawaida udongo unaohitajika katika zao la Chia ni udongo tifutifu ila usiwe na mfinyanzi, kwani udongo unapokuwa na mfinyanzi, unasababisha jua likiwaka mizizi inashindwa kupenya vizuri kwenye ardhi.

Anafafanua kuwa kilimo cha Chia huchukua siku 90 tangu kupandwa hadi kuvunwa kama zao hilo litapata jua la kutosha. Likikosa jua la kutosha, basi Chia haikauki kirahisi na pia inaongezeka matawi na hivyo, huweza kuchukua muda wa miezi minne badala ya siku 90.

Faida ya Chia

Eusebia Nyamwiza ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Organic Chia Seed, anasema Chia zimekua zikitumiwa kama chakula na dawa ya magonjwa mbalimbali kwa makabila ya Aztecs na Mayans kutoka Amerika ya kusini.

Anasema mbegu za Chia zinasaidia mwili kuwa na mizania ya kiwango cha Lehemu pamoja na kuupa mwili nguvu huku zikiimarisha mifupa.

Mbegu za Chia zina madini muhimu ya Omega 3, hivyo ni viungo ambavyo mpishi yeyote hawezi kuacha kutumia lakini pia mbegu hizo hupunguza makali ya hedhi kwa kwa wanawake.

Rosemary Mpanju ambaye ni mkulima na muuzaji wa zao hilo anafafanua kuwa unaweza kuchanganya vijiko viwili vya mbegu za Chia katika uji, juisi au chakula chochote kile na baada ya dakika 10 hadi 30, unaweza kula chakula chako ambacho huwa na muonekano wa kuvutika kama mlenda.

Anasema ulaji wa mara kwa mara wa mbegu hizo husaidia kuimarisha afya ya mwili na kuukinga na magonjwa mbalimbali.

“Vile vile hulainisha ngozi na kupunguza uzee, mbegu za chia zina kiwango kikubwa cha nyuzinyuzi na hivyo husaidia katika kumeng’enya chakula na zaidi husaidia kupunguza uzito kwa watu wenye uzito uliopita kiasi” anasema Mpanju ambaye pia anajihusisha na usindikaji wa bidhaa zinazotokana na ngano

Mbali na faida hizo, Chia husaidia kuongeza kumbukumbu na hiyo ni kutokana na kusheheni madini mbalimbali kama chuma ambayo ni mazuri kwa afya , kalshiamu, Manganizi, Magneziamu, Fosforasi pamoja na Vitamin A,B,D na E.

Changamoto ya masoko

Kwa mujibu wa Mpanju, changamoto wanayokabiliana nayo ni uhakika wa masoko,

“Hatuna masoko ya kudumu hiyo, tunaziomba mamlaka husika ziweze kutusaidia ili tuweze kuwa na masoko ya uhakika, ili na sisi tuuze bidhaa hii nje ya nchi” anasema.

Advertisement