Utafiti: Wanawake walio ndani ya ndoa wanaongoza kwa kutoa mimba

Sunday November 18 2018

 

By Waandishi Wetu, Mwananchi

Ipo dhana kwamba mabinti wadogo au ambao hawajaingia katika ndoa ndio wanaoongoza katika matukio ya utoaji mimba.

Utafiti uliofanywa mwaka jana na taasisi ya Nigeria inayojihusisha na masuala ya uzazi ya Global Sexual And Reproductive Health Advocacy ulibaini kuwa wanawake waliokatika ndoa wanaongoza kwa kutoa mimba.

Utafiti huo unasema wanawake 36 kati ya 1,000 walio katika ndoa wanatoa mimba kila mwaka ikilinganishwa na 25 kati ya 1,000 wasio kuwa katika ndoa.

Asilimia 60 ya watu duniani wanaishi katika mataifa yanayoruhusu utoaji mimba ikiwamo China ambayo katika kipindi cha mwaka mmoja mimba milioni 10 hutolewa.

Kwa wastani asilimia 90 ya mimba hutolewa katika nchi zilizoendelea huku zinazoendelea zikiwa na asilimia chache kutokana na kuwa na sheria kali zinazozuia vitendo hivyo.

Utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la The Lancet, unaonyesha kuwa idadi ya mimba zinazotolewa barani Afrika umeongezeka.

Utoaji mimba duniani

Mmoja wa watafiti, Akinrinola Bankole anasema kati ya mwaka 1990 na 1994 wastani wa mimba 4.6 milioni zilitolewa wakati kati ya kipindi cha 2010 na 2014 wastani wa mimba 8.4 zilitolewa.

Utafiti huo ulibaini kuongezeka kwa utoaji mimba lakini ulitoa angalizo kwamba umetokana na ongezeko la idadi ya watu walio katika umri wa kuzaa kati ya miaka 15 na 44.

Utafiti mwingine kuhusu utoaji mimba uliowahi kuchapishwa katika jarida hilo hilo mwaka 2012, ulitoa angalizo kwamba hakuna uwiano kati ya kupungua kwa utoaji mimba na sheria kali za nchi.

Bankole anaeleza: “Kwa mfano Ethiopia haina sheria inayokataza utoaji mimba moja kwa moja lakini idadi ya vitendo hivyo ni ndogo ukilinganisha na Nigeria yenye sheria kali lakini mimba zinazotolewa ni nyingi sana.”

Kwa nini wanatoa mimba?

Kwa mujibu wa utafiti huo, mahitaji ya kuwa na familia ndogo yanachagiza vitendo vya utoaji mimba hasa katika maeneo yanayoendelea.

Unazitaja sababu mbalimbali kuwa chanzo cha wanawake ndani ya ndoa kutoa mimba kuwa ni madhara yatokanayo na njia za uzazi wa mpango, kutojua kalenda, mwanamke kutokuwa na uwezo wa kufanya maamuzi na ulevi.

Utafiti huo unapendekeza kuwekeza katika huduma za uzazi wa mpango hasa kwa kuwa wanawake wengi huzikimbia kutoka na madai kwamba zinawaletea madhara.

Pia, unapendekeza wanawake wapewe elimu ya uzazi wa mpango na kufuata kalenda wakiwa na waume zao ili washirikiane tofauti na sasa jukumu hilo humuelemea mwanamke.

Msukumo ni mkubwa

Mtaalamu wa saikolojia nchini, Modesta Kamongi anasema kwenye uhusiano wowote lazima kuwepo na kutokukubalina jambo ambalo hujitokeza pia kwa wanandoa.

Katika hili anasema itakuwa mmoja wa wanandoa hayupo tayari kwa kipindi hicho kubeba ujauzito, hivyo inapogundulika tayari ipo kunakuwa na mabishano na mmoja akimuona mwenzake ana hoja basi huamua kuitoa.

Sababu nyingine ni kuwapo kwa kutokuelewana ndani ya ndoa, hii ikiwa ni pamoja na mwanamke kujikuta akinyanyasika ndani ya ndoa ikiwemo suala zima la kupigwa, kutotunzwa yeye pamoja na watoto aliokwishawazaa.

“Hivyo inapokuja kugundulika kabeba ujauzito anaona bora autoe ili kujiweka katika hali salama zaidi ya kupambana na hayo ambayo yanamkabili kuliko kuongeza kiumbe kingine ambacho mwisho wa siku anajua kitakuja kupitia madhila wanayoyapata. Jingine ni mwananmke kutokuwa tayari kupata ujauzito kwa kipindi husika.”

Mwanamke kuelemewa

“Hili ni tofauti kidogo na lile kutokukubaliana kwani kama mnavyojua mbeba mimba ni mwanamke na sio mwanaume, hivyo kama yeye hayupo tayari anaweza kutafuta njia yoyote ya kuondoa kiumbe aliyepo tumboni mwake hata kama mwanaume ataitaka.

Pia, lipo suala la baadhi ya wanawake huogopa kupoteza mvuto pindi watakapozaa, hivyo anaona njia pekee ya kuutunza mvuto wao ni kuitoa mimba.

“Kuna wanaozaa na bado wanakuwa vilevile na mvuto wao kutegemeana na vyakula wanavyokula, mazoezi na mambo mengine ambayo watashauriwa na wataalamu kuyafanya mara baada ya kujifungua,” anasema.

Mwanasaikolojia na mhadhiri wa saikolojia na utafiti katika Chuo Kikuu cha SAUT-Archbishop James University College, Noverty Deograthias anasema: “ pointi yangu kimsingi inajikita kwenye kuelezea namna hali hiyo ilivyo ya kwaida katika kundi mojawapo la umri wa ndoa (ndoa za changa-miaka 0 hadi mitano, ndoa za kati-miaka mitano hadi 20 na ndoa kongwe-miaka 20 na kuendelea.”

Anafafanua kuwa: “Kwa vyovyote vile, utafiti ungebainisha sampo. Hapo ndo tunaweza kusema, kwa mfano, wanawake katika ndoa changa hutoa mimba kwa sababu mbalimbali kama: hisia za kuonekana tofauti baada ya kubeba mimba na kujifungua.”

Pia, Wakati mwingine, baadhi ya wanandoa hutoa mimba kwa sababu ya kutojiandaa kimalezi kwamba kimsingi, mimba haipaswi kutokea tu, ni mpango wa wanandoa.

Kwa akina mama wengine hujikuta wametoa mimba kwa vile hawajawa tayari kulea kiumbe kipya. Na hii huchangia pia baadhi ya akina mama kuzaa na kutupa vichanga kwa vle malezi kwao ni mzigo.

Ugomvi unachangia

Anasema kama tunaangazia na makundi mengine kwa mujibu wa umri wa ndoa, sababu nyingine zinazotajwa kuchochea utoaji mimba katika ndoa ni pamoja na magomvi katika ndoa.

Wapo baadhi ya akina mama mara baada ya kugundua uhusiano wao unasumbua hupenda wasizae/watoe mimba.

Hii hutokana na imani kuwa wanaweza kuanzisha mahusiano kwingine kwa watu wengine.

Pia, sababu za kiafya kwani wapo wanaougua kiasi kwamba usalama wao hutegemea kutopata ujauzito. hata hivyo, hii ni sabubu ya kiafya zaidi.

Advertisement